Sunday, April 20, 2008

Chenge ajiuzulu


SIKU chache baada ya kuandamwa na tuhuma za kumiliki mabilioni ya shilingi katika akaunti yake ya nje katika kisiwa cha Jersey, Uingereza Mbunge wa Bariadi Magharibi na Waziri wa Miundo Mbinu, Andrew Chenge amejiuzulu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Mwananchi usiku jana, Waziri Chenge aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais Jakaya Kikwete muda mfupi baada ya Rais kuwasili nchini.

Kujiuzulu kwa Waziri Chenge kulithibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu ambaye alisema kuwa rais amekwishaipokea barua ya kujiuzulu kwa Chenge na amemkubalia na akasema huo ndiyo uamuzi wa busara na ndiyo aliokuwa akusubiria.

"Rais amepokea barua ya Waziri Chenge na ameshamjibu akisema uamuzi huo ndiyo alikuwa akiusubiri,"alisema Rweyemamu alipozungumza na Mwananchi.

Taarifa za kujiuzulu kwa Waziri Chenge zilianza kusikika tangua subuhi ya jana, lakini zikawa hazijathibitishwa hadi zilipopatikana jana jioni.

Uamuzi huo unakuja siku chache baada ya Waziri Chenge kukataa kujibu tuhuma zinazomkabili za kumiliki mabilioni ya fedha nje ya nchi na kuwakimbia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, huku taarifa zingine zikidai kuwa aliomba radhi kwa Watanzania akidai kutojua kiswahili.

Chenge ambaye anatuhumiwa kumiliki dola za Marekani 1 milioni (Sh1.2 bilioni) katika mazingira tata, alifikia hatua hiyo baada ya kukataa kujibu maswali ya waandishi wa muda mfupi baada ya kufunga Mkutano wa Kimatiafa nchi 19 duniani kuhusu Udhibiti wa Vitendo vya Uharamia na Uvamizi dhidi ya Meli zinazopita katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, uliofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, jijini Dar es Salaam, Aprili 14-18, mwaka huu.

Mara baada ya kufunga mkutano huo, alitoka nje ya ukumbi wa mkutano na mwandishi wa gazeti hili alimfuata na kumwomba kufanya naye mahojiano lakini alimkatalia.

Tuhuma dhidi ya Chenge za kujilimbikizia fedha hizo, ziliibuliwa na gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza katika toleo lake la Jumamosi wiki iliyopita ambalo lilieleza kuanza kwa uchunguzi dhidi yake, kutokana na akaunti yake kukutwa na zaidi ya dola za Marekani 1 milioni.

1 comment:

Christian Bwaya said...

Huyu wa nne. Tusubiri atakayefuatia ni nani.

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...