Wednesday, January 01, 2025

NMB yadhamini kombe la Mapinduzi 2025, yafadhili Siku ya Mazoezi Kitaifa Z'bar

 






BENKI ya NMB, imetangaza udhamini wa Sh. Milioni 50 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar (Mapinduzi Cup 2025), inayotarajia kuanza Januari 03, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani visiwani Pemba, ambayo itashirikisha timu za Taifa, badala ya klabu za Tanzania Bara na Zanzibar kama ilivyozoeleka


Sambamba na udhamini huo, NMB pia imekabidhi 'tracksuit' 100 zenye thamani ya Sh. Mil. 9 za kuvaa viongozi wa Serikali ya Zanzibar katika Siku ya Kitaifa ya Mazoezi (Januari 1, 2025), ambayo ni sehemu ya Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo inafanyika chini ya kaulimbiu: 'Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo Yetu - Mapinduzi Daima.'

Hafla ya makabidhiano ya hundi ya udhamini na 'tracksuit' hizo, imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, ambako Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Jumaa Nassor, alimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Fatma Hamad Rajabu, mbele ya Meneja Uhusiano wa NMB Zanzibar, Jaha Khamisi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo baada ya kupokea hundi, Bi. Fatma aliishukuru NMB kwa mchango wao, ushirikiano na umoja wanaoonesha kwa Serikali ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, na kuitaka kudumisha mashirikiano hayo kwa ustawi wa Zanzibar na maendeleo ya Wazanzibar kwa ujumla.

Alibainisha kuwa mchango na ushiriki wa NMB sio tu katika Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, bali iko mstari wa mbele daima kuchagiza maendeleo ya visiwa hivyo na wakazi wake na katika nyanja nyingi, ikiwemo michezo, ambako imejitoa vya kutosha kudhamini Kombe la Mapinduzi kwa miaka kadhaa na kuchangia ongezeko la ajira kupitia michezo.

"Wazanzibar wengi wanahudumiwa na NMB na uwingi wao unalenga kuiwezesha benki kukuza pato lao ili nao wanufaike na mchango wa maendeleo ya Zanzibar na watu wake. Tunawapongeza kwa kufadhili Siku ya Mazoezi Kitaifa, lakini pia kwa udhamini wenu mnono katika Kombe la Mapinduzi 2025.

"Tofauti na miaka yote ambako klabu hushiriki Kombe la Mapinduzi, mwaka huu zitacheza timu za Taifa, ikiwemo Zanzibar Heroes. Wito wetu kama Serikali, tunawataka Wazanzibar wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Gombani Pemba, kuisapoti timu yao iweze kubakisha nyumbani taji la mashindano hayo," alisema Bi. Fatma.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Jumaa Nassor, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa sehemu ya Shamrashamra za Mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka 12 sasa na kwamba inatambua na inathamini mchango wa Serikali ya Zanzibar katika kuweka mazingira wezeshi ya wao kuhudumia Wazanzibar na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya wananchi.

"NMB imekuwa mshirika mkubwa wa Serikali zote (Zanzibar na Tanzania), hivyo ni heshima kuendelea kuwa sehemu ya Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

"Tuko hapa kufanya mambo mawili, yote yakihusiana na sherehe hizo zinazoanza Januari Mosi na kufikia ukomo wake Januari 13, siku moja baada ya kilele cha Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Leo tunakukabidhi 'tracksuit' 100 za kuvaa washiriki wa Siku ya Mazoezi Kitaifa Zanzibar Januari Mosi, tukiamini kuwa mchango huu utatumika kama chachu katika muendelezo wa hamasa ya mazoezi miongoni mwa Wazanzibar, pia tunakabidhi kwako hundi ya udhamini wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, wenye thamani ya Sh. Milioni 50," alisema Ahmed na kuongeza:

"Udhamini huu pamoja na vifaa hivi, ni kilelezo na uthibitisho wa dhati kuwa NMB inathamini michezo, kwani afya zetu zinaimarika zaidi kupitia michezo na uimara wa afya ndio chachu ya kukua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

"Ni fahari kubwa kwetu kuendelea kushirikiana na Serikali kwa miaka 12 ya NMB kuwa sehemu ya ukamilifu wa matukio hayo kwa kipindi chote hicho," alisisitiza Ahmed katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa pia na maafisa wa wizara hiyo ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo pamoja na Wajumbe wa kamati ya kombe la mapinduzi 2025.

WHO Yaitaka China Kueleza Chanzo Cha Uvico 19

 

Mkurugenzi Mkuu wao Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus
Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO bado linasubiri ushirikiano kamili kutoka kwa serikali ya China ili kufafanua chanzo cha janga la UVIKO-19 pia katika salamu zake za mwaka mpya akisisitiza amani duniani.

Hii ni miaka mitano baada ya visa vya kwanza vya ugonjwa mpya wa mapafu (Uvico 19) kuripotiwa katika mji wa China wa Wuhan. WHO imesema jijini Geneva kuwa hilo ni sharti la kimaadili na kisanyasi.

Shirika hilo la Afya Ulimwenguni linaloongozwa na Mkurugenzi Mkuu wao Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus (pichani)  limeitaka China kutoa data zote ili wanasayansi waelewe chimbuko la janga hilo lililotikisa dunia na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Taarifa ya WHO imesema kuwa bila uwazi na ushirikiano miongoni mwa nchi tofauti, dunia haiwezi kuzuia na kujiandaa vya kutosha kwa magonjwa ya milipuko na majanga ya siku za usoni.

Wakati huo huo Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa wito kwa viongozi “kuleta amani inayohitajika sana duniani, afya na usalama kwa wote,” akisisitiza kwamba “amani ni, na daima itakuwa, dawa bora kwa afya na ustawi wa watu wote, kila mahali.”

Kupitia ujumbe wake wa video wa mwishoni wa mwaka, Tedros amekumbusha kwamba wakati wa wiki ya Krismasi, alikuwa Yemen katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa kujadiliana na mamlaka ya nchi hiyo ili kuachiliwa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wasaidizi wengine wa kibinadamu.

Mkurugenzi Mkuu wao Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus

Uhamiaji Yatakiwa Kuimarisha Udhibiti Wa Wahamiaji Haramu

  Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Dkt. Tulia Akson

Idara ya Uhamiaji nchini imetakiwa kuimarisha udhibiti wa Wahamiaji haramu na baadhi ya wageni wanaoingia na kufanya biashara haramu huku wakiwa na lengo lililojificha la kuvunja amani yetu kukamatwa na kuwachukulia hatua kali za kisheria pindi wanapobainika

Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Dkt. Tulia Akson katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi la Jengo la Afisi za Uhamiaji Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja Desemba 29, 2024

Dkt.Tulia amesema usafirishaji haramu wa binadamu umekuwa ukipigwa vita duniani na hapa nchini hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kupambana nalo ili kuweza kulitokomeza kabisa.

“Kwa kusema hayo ndugu zangu hatua tumepiga ni kweli lakini tunataka hatua ipigwe zaidi hasa katika hili eneo la Uhamiaji kwanini kwasababu wako wale watu huwa wanaitwa wahamiaji haramu tunatamani waendelee kudhibitiwa, kwakweli mnafanya kazi kubwa sana lakini muendelee kuifanya vizuri zaidi ili nchi yetu iendelee kuwa salama”.Alisema Dkt. Tulia

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo akimuwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Idara ya Uhamiaji imeboresha njia za kielektroniki katika huduma zote za kiuhamiaji.

“Idara ya Uhamiaji Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo ambapo imefanikiwa kuweka mifumo ya kielektronikia katika utoaji wa huduma zote za kiuhamiaji kwa nchi nzima kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar”. Amesema Sillo

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania CGI Dkt. Anna Makakala amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha na kuiamini Idara ya Uhamiaji kwa kuboresha miundo mbinu na maslahi ya Watumishi, Maafisa na Askari wa Uhamiaji.

Mradi huo wa ujenzi wa jengo la Afisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 1.8 ambapo umefikia asilimia 85% za utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Aprili 2025 ukiwa unatarajiwa kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za Uhamiaji kwa raia, wawekezaji na Wageni.


Nafasi Za Kazi 24 Taasisi Mbalimbali Za Umma, Mwisho wa kutuma Januari 2, 2025


Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kituo cha Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Kituo cha Tiba cha Bugando (BMC), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), The Public Service Recruitment Sekretarieti (PSRS), inawaalika Watanzania mahiri na wenye sifa stahiki kujaza ishirini na nafasi nne (24) zilizoachwa wazi zilizotajwa hapa chini.

Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 02 Januari, 2025;

FUNGUA HAPA >>> NAFASI ZA KAZI 24 TAASISI MBALIMBALI ZA UMMA

MAHAKAMA YAMUACHIA HURU ALEX MSAMA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni Kinondoni imemuachia huru Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka ya kughushi nyaraka za kiwanja dhidi yake.


Katika kesi hiyo ya jinai namba 275 ya mwaka 2022 imetolewa hukumu leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isihaka Kupwa ambapo Msama alikuwa anakabaliwa na mashtaka matano.

Hakimu Kupwa alisema mahakama hiyo ilipokea na kupitia vielelezo na ushahidi wa pande zote mbili pasina kuacha.

Hakimu Kupwa amesema baada ya mahakama hiyo kupitia ushahidi wa pande zote mbili, imeona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake hivyo inamuachia huru na kumpa ushindi.

Miongoni kwa sababu alizozitaja Hakimu Kupwa ni kwamba Jamhuri ilishindwa hata kuwasilisha cheti cha kifo cha marehemu aliyetajwa katika kesi hiyo, pia kukosekana kwa mtaalamu wa kuthibitisha maandishi yaliyoghushiwa.

“Mahakama hii inamuachia huru Alex Msama Mwita, haki ya kukata rufaa ipo wazi,”.

Miongoni mwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Msama ni Kughushi, ambapo anadaiwa siku isiyojulika ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa nia ya kufanya udanganyifu alighushi nyaraka za mauziano yenye Tarehe ya Julai 6, 1970, akikusudia kuonyesha kuwa ni nyaraka halisi za mauziano kati ya Khalid Swalee Chengu na Ndelikyama Mweleli huku akijua fika kuwa ni za uongo.

Pia shtaka jinginr inadaiwa Aprili 24, 2016 ndani ya Jiji la Dar es Salaam Kwa nia ya kufanya udanganyifu, anadaiwa kughushi sahihi ya Ndelikyama Mabolio Mweleli katika Mkataba wa mauzo wa Aprili 24, 2016 Kwa kusudi la kuonyesha kuwa ni nyaraka halisi za mauziano kati yake na Ndelikyama Mabolio Mweleli, huku akijua wazi kuwa ni uongo.

Pia inadaiwa siku ya Aprili 24, 2016 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, Kwa nia ya kufanya udanganyifu, alighushi barua ya ofa yenye kumbukumbu namba D/KN/A/13504/TMM yenye Tarehe ya Septemba 28, 1979 na jina la Ndelikyama M. Mweleli, Kwa kusudi la kuonyesha kuwa Kiwanja namba 160 kilichopo Mbezi Beach Dar es Salaam, kilikuwa ni Cha Ndelikyama Mabolio Mweleli huku akijua wazi kuwa ni za uongo.

DKT. SAMIA AMEIHESHIMISHA TANZANIA MATUMIZI YA NISHATI SAFI-MAJALIWA

 









-Asema Watanzania tunapaswa kumuunga mkono

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiheshimisha Tanzania katika hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na umuhimu wake kwenye afya ya binadamu na utunzaji wa mazingira.

Amesema kuwa kutokana na jitihada hizo, mashirika ya kimataifa yameonesha nia ya kumuunga mkono ikiwemo kufanya mkutano mkubwa wa nishati safi Afrika hapa nchini. “Watanzania tumuunge mkono Rais Dkt. Samia katika kampeni hii na kuhakikisha tunaongoza kwenye matumizi ya nishati safi barani Afrika”

Amesema hayo leo (Jumanne, Desemba 31, 2024) wakati wa Tamasha la Azimio la Kizimkazi ambalo lilienda sambamba na ugawaji wa majiko 1000 ya gesi kupitia kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tukio hilo limefanyika katika eneo la Kilimahewa Majumbakumi, Ruangwa mkoani Lindi.

“Tunapaswa kumuunga mkono kwasababu agenda imeanzishwa na Rais wetu, dunia lazima iitambue Tanzania kama ambavyo imetambua na kuleta mkutano mkubwa wa nishati safi hapa nchini, sisi tusiwe nyuma, tuwe mstari wa mbele”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuhamasisha umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo ikiwemo umeme, gesi na mkaa rafiki.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amesema kuwa azimio la kizimkazi linakwenda kuwa mkombozi kwa mwanamke kupata nishati safi ya kupikia.

Mmoja ya wanufaika wa mpango huo wa ugawaji wa mitungi ya Gesi Hawa Mpinga mkazi wa Kata ya Nachingwea amesema awali walipata changamoto za kiafya kutokana na matumizi na nishati chafu “Moshi wa kuni umetuharibu sana macho”

Katika tukio hilo Mheshimiwa Majaliwa amewaga mitungi ya gesi 1000, ambayo 800 imetolewa na Shirika la Utangaji Tanzania kupitia Bongo Fm na mitungi 200 imetolewa na Taifa gesi.

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, KWA WATANZANIA

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akilihutubia Taifa wakati akitoa Salaam za kuaga Mwaka 2024 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2025 Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar tarehe 31 Desemba, 2024.

 Ndugu Wananchi;

Leo, tarehe 31 Disemba, tunauhitimisha mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa neema ya uhai na afya njema. Wapo wenzetu wenye changamoto za kiafya, ambao tunaendelea kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajaalie afya njema ili warudi kwenye shughuli zao za kujenga Taifa.

Kuna ndugu na jamaa zetu ambao tungetamani kuwa nao leo hii, lakini kwa mapenzi yake Mola, haikuwezekana. Tuendelee kuwaombea mapumziko mema peponi. Amen

Ndugu Wananchi;

Mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa kihistoria, wenye mafanikio na unaotupa matumaini zaidi tunapoitazama kesho ya Taifa letu. Katika jitihada za kutekeleza majukumu yangu, nilipata fursa ya kufanya ziara katika baadhi ya Mikoa, na kote nilikopita nimejionea ari na hamasa kubwa ya wananchi kujiletea maendeleo. Kuanzia Morogoro hadi Rukwa, Mwanza hadi Ruvuma na Zanzibar, kote niliona kazi inaendelea. Serikali inatekeleza majukumu yake, wananchi wanajituma na mabadiliko yanaonekana.

Leo nitagusia baadhi ya masuala makubwa yaliyojiri mwaka tunaoumaliza, changamoto tulizokabiliana nazo na tunayoyatarajia mwakani 2025.

Ndugu zangu;

Kama nilivyotangulia kusema kuwa mwaka 2024 ulikuwa ni wa kihistoria. Tuliadhimisha miaka 60 ya kuasisiwa kwa Muungano wetu. Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere “Tanzania ni nchi ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake kutoka katika Ukoloni.” Hivyo basi, tuendelee kujivunia na kuudumisha Utaifa wetu, uliojengwa katika misingi imara ya Muungano wa Jamii mbili zenye udugu wa asili.

Pamoja na kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, tuliadhimisha pia miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, miaka 60 ya Jeshi la Polisi, na miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Ni fahari kwamba tulifanya maadhimisho hayo yote huku nchi yetu ikiwa salama yenye Amani na Utulivu. Kwa hakika, ninavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda nchi yetu. Nawashukuru pia wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa; umoja ambao unaifanya Tanzania kuwa na sifa ya kipekee.

Ndugu Wananchi;

Mwaka huu pia tulikuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika kwa amani na utulivu. Katika uchaguzi ule, kwa mara ya kwanza, wagombea ambao hawakuwa na washindani ilibidi wapate ridhaa ya wananchi, kwa kupigiwa kura ya ndiyo au hapana. Hii imeondosha rasmi utaratibu wa kupita bila kupingwa, ambayo ni hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia nchini.

Ndugu Wananchi;

Mwaka 2024 ulikuwa wenye neema na mafanikio, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa yote. Uchumi wa nchi yetu uliendelea kuimarika na kuwanufaisha wananchi. Kati ya Januari hadi Juni 2024 uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023. Deni la Taifa nalo liliendelea kuwa himilivu. Mfumuko wa bei umebaki ndani ya lengo la asilimia 3, hali iliyochangiwa na sera madhubuti za kifedha.

Tulishuhudia ongezeko la uwekezaji kutoka ndani na nje ya Nchi. Kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania kati ya Januari hadi Novemba 2024, tumesajili miradi ya uwekezaji 865 yenye thamani ya Dola za kimarekani bilioni 7.7 inayotarajia kuzalisha ajira 205,000.

Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), imetoa vibali vya kuwekezwa nchini viwanda vipya vikubwa 15 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235, vinavyotarajia kuzalisha ajira karibu 6,000 na kuuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 94 kwa mwaka.

Kwa upande wa mapato, Mamlaka ya ukusanyaji Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya Shilingi trilioni 21.276 kati ya mwezi Januari na Oktoba, 2024 sawa na asilimia 99.3 ya lengo. Hili ni ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa na makusanyo katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Mwaka huu pia tumeendelea na jitihada za kujenga uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya TEHAMA. Katika kufanikisha hilo, tumeunda Wizara mahsusi ya TEHAMA na tayari tumezindua Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali. Miongoni mwa mipango yetu ya baadaye katika kutekeleza mkakati huo ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anatambulika kwa kutumia Jamii Namba, itakayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Ndugu Wananchi,

Kwa upande wa Diplomasia, mwaka huu nchi yetu ilizidi kuimarika na kutuletea manufaa makubwa katika nyanja za kimataifa. Tumepata heshima ya kushiriki Mkutano wa G20, ambao pamoja na maamuzi mengine yaliyofanyika, mkutano huo pia uliazimia kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa nishati safi, na vile vile, uliazimia kuimarisha uwekezaji kwenye kilimo ili kuondosha njaa na umaskini duniani; jitihada zinazoendana na malengo yetu Tanzania.

Kwa mara nyingine tena, Tanzania iling'ara kwenye medani za kimataifa baada ya mgombea wetu Mheshimiwa Daktari Faustine Ndugulile kuwania na kushinda nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika. Hata hivyo, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Ndugulile alituacha kabla hata ya kuingia ofisini. Tunazidi kumuombea pumziko la Amani.

Ndugu Wananchi,

Ziara tulizozifanya katika nchi 16 duniani, zilituwezesha kujenga mahusiano ya kidiplomasia, na kiuchumi. Ziara yangu nchini Jamhuri ya Korea, ilifanikisha kupatikana fedha zenye masharti nafuu kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta za maendeleo. Kupitia fedha hizo, pamoja na mambo mengine, tutajenga kituo cha kisasa cha mafunzo ya reli, chuo cha mafunzo ya anga na urubani, ujenzi wa kituo cha kusambaza umeme Nyakanazi, na kituo cha uchenjuaji wa madini na maabara za kisasa za vito.

Miradi mingine itakayoangaliwa ni mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ujenzi wa Kongani ya Viwanda Bagamoyo, na Ununuzi wa Mabehewa ya Abiria na Mizigo kwa ajili ya Kipande cha Reli kutoka Mwanza hadi Isaka, Ujenzi wa Bandari ya Wete na Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo. Fedha hizo pia zitatumika kwenye Ujenzi wa Barabara Zanzibar, ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano Zanzibar, na Ujenzi wa Studio ya Filamu ya Kisasa na Kituo cha burudani mbalimbali kwa ajili ya ajira za vijana.

Ziara hiyo pia ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba wa masharti nafuu wenye kiasi cha Dola za Marekani milioni 163.6 kwa ajili ya kugharamia mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Binguni na Kituo cha Mafunzo ya Afya huko Zanzibar.

Ziara ya nchini China, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, ilifungua milango ya soko la bidhaa mbalimbali ikiwemo mihogo mikavu, soya, mabondo ya samaki, mazao ya baharini, asali, mashudu ya alizeti na pilipili. Ni matarajio yangu kuwa wakulima na sekta binafsi watachangamkia fursa hizi ili tuweze kunufaika na soko hilo. Wakati wa ziara hiyo, Tanzania, China na Zambia zilikubaliana kuifufua reli ya TAZARA ili kuboresha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.

Kwa upande wa ukanda wa SADC tulipata heshima ya kupokea Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, yenye jukumu la kusimamia masuala ya Ulinzi na Usalama katika Kanda hiyo, ambapo mbali na masuala mengine tumeweza kusimamia uangalizi wa chaguzi kwenye Nchi za Botswana, Mauritius, Msumbiji na Namibia.

Ndugu Wananchi,

Kuimarika kwa uchumi kumetuwezesha kuendelea kufanya mabadiliko chanya katika mifumo yetu wa Elimu Msingi na Sekondari hadi vyuo vya ufundi. Tumeendelea kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi, kutandaza zaidi miundombinu ya umeme, na kusambaza umeme vijijini. Aidha, tumetekeleza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, kwa kusimamia utekelezaji wa miradi 1,300 ya maji nchi nzima. Kukamilika kwa miradi hio kutatufikisha kutimiza lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.

Katika sekta ya kilimo tulifanikiwa kuhamasisha kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kuboresha mifumo ya masoko ya mazao mbalimbali, na kupata bei nzuri ya mazao kwa wakulima. Kwa mfano, kwa mwaka 2024 ufuta uliuzwa kwa Shilingi 4,850 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi 3,600 mwaka uliopita 2023; Kahawa aina ya Arabika iliuzwa kwa Shilingi 8,500 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi 6,500 mwaka uliopita na kwa kahawa aina ya Robusta iliuzwa kwa Shilingi 5,000 kwa kilo badala ya shilingi 3,500 mwaka 2023. Mbaazi iliuzwa kwa Shilingi 2,236 kwa kilo mwaka 2024 badala ya Shilingi 2,000 mwaka 2023, kakao imeuzwa kwa Shilingi 35,000 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya Shilingi 29,500 mwaka uliopita 2023; na korosho iliuzwa kwa Shilingi 4,195 mwaka 2024 ikilinganishwa na Shilingi 2,190 mwaka 2023, huku uzalishaji wa korosho unatarajiwa kufikia tani 425,205 kwa msimu wa 2024/2025 unaoendelea ikilinganishwa na tani 310,787 zilizozalishwa msimu uliopita wa 2023/2024.

Mwelekeo wa Serikali ni kuboresha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kupitia soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kwa mazao ya kilimo.

Ndugu Wananchi,

Tukiangazia miradi ya kimkakati, baadhi yake tayari imefikia hatua ya kuanza kutoa huduma. Bwawa la Mwalimu Nyerere limeanza kuzalisha umeme, na kufanya hali ya huduma za umeme nchini kuimarika. Uzalishaji kwa sasa umefikia jumla ya Megawatt 3,169 ikilinganishwa na mahitaji ya Megawatt 1,888.

Aidha, Mradi wa Reli ya Kisasa - SGR, unatoa huduma kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma. Shirika la Reli lilikuwa linasafirisha wastani wa abiria laki 3 hadi 4 kwa mwaka. Inafurahisha kwamba ndani ya miezi mitano ya huduma za SGR, zaidi ya abiria 1,200,000 wameshasafiri na reli hiyo.

Tumeendelea na maboresho kwenye sekta ya anga na uwekezaji kwenye shirika la ndege Tanzania. Mwaka huu, Shirika letu limefikisha ndege 16, na limeongeza safari za ndani ya nchi na kimataifa kufikia 25, ikiwemo kuanza tena safari za abiria kwenda Afrika Kusini na kukamilisha taratibu za kuanza safari za mizigo kwenda China. Mwaka huu Shirika limefanikiwa kusafirisha abiria zaidi ya milioni 1 na laki 1 na zaidi ya tani 10,000 za mizigo.

Serikali pia imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya anga na kuboresha mifumo kwenye viwanja vya ndege. Mwaka huu tuliendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Arusha, Kahama, Mpanda, na Songwe. Mwakani tunatarajia kukamilisha viwanja vya ndege vya Iringa, Mtwara, Songea, Kigoma, Msalato, Musoma, Shinyanga na Sumbawanga.

Hapa nataka nisisitize kuwa, miradi hii ni yetu sote, na imejengwa kwa kutumia rasilimali zetu. Hivyo, tunawajibika kuitunza ili itunufaishe sisi na vizazi vijavyo kesho. Vitendo vya kuhujumu miradi hii ni kulihujumu Taifa.



Ndugu Wananchi,

Katika hatua nyingine, tuliendeleza mageuzi ndani ya Serikali ili kuimarisha utendaji na ufanisi. Tuliendelea na zoezi la kubaini taasisi na mashirika yanayopaswa kufutwa, kuunganishwa au kurekebishwa kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi zaidi.

Mwaka huu pia tuliendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya ushirika ili kuchochea maendeleo vijijini. Dhamira ya Serikali ni kurejesha hadhi ya ushirika nchini. Ili kupata maendeleo endelevu kwa ushirika na wana-ushirika, Serikali imechagiza mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika, ambayo iko katika hatua za mwisho, ikiwemo kufikia lengo la ukwasi wa shilingi bilioni 50.

Mwaka huu tuliendelea kushirikisha sekta binafsi na kuhamasisha uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na huduma. Katika kufanikisha hilo mpaka sasa kuna jumla ya miradi 74 ya Ubia ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji. Hadi kufikia mwezi Desemba 2024, miradi 4 imefikia hatua ya utekelezaji, ambapo miradi miwili 2 ni ya uendeshaji wa bandari inayosimamiwa na TPA. Miradi mingine ni Ujenzi wa Jengo la Biashara (Business Complex) kubwa kuliko zote Kariakoo na ule wa Ubungo - East African Logistic.

Miradi mingine inayotazamiwa kuanza utekelezaji mwakani 2025 ni ujenzi wa barabara ya Haraka (Express way) kutoka Kibaha- Chalinze - km 78.9, mradi wa Ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto chini ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) chini ya DART na mradi wa Ujenzi wa Jengo la Biashara na Hoteli ya Nyota Nne katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Ndugu Wananchi,

Katika kukabiliana na athari za mazingira kutokana na matumizi ya kuni, mwaka huu tulizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia. Niwatake wahusika wasimamie ipasavyo utekelezaji wa Mkakati wa kuchochea matumizi ya nishati safi ili kufikia lengo la asilimia 80 ifikapo mwaka 2034. Aidha, nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa zitokanazo na kukua kwa matumizi ya nishati safi.

Ndugu Wananchi;

Pamoja na kuwa ni mwaka wa kihistoria na mafanikio, mwaka 2024 pia ulikuwa na changamoto zake. Nitagusia zile kubwa na namna tulivyokabiliana nazo.

Changamoto moja kubwa tuliyokabiliana nayo ilikuwa ni athari za mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya, iliyosababisha mafuriko, maporomoko na upotevu wa maisha, uharibifu wa makazi, mashamba na baadhi ya miundombinu ikiwemo barabara na madaraja sehemu mbali mbali nchini. Tulisimama pamoja kama Taifa, misaada ya kibinadamu kwa waathirika kama vile vifaa vya ujenzi, chakula, nguo na malazi ilitolewa. Aidha, Serikali ilijenga nyumba 109 kwa ajili ya walioathirika na maporomoko kule Manyara.

Kupitia TANROADS na TARURA, Serikali ilitumia shilingi bilioni 136 kutengeneza miundombinu iliyoathiriwa. Pia tulitenga shilingi bilioni 868 kutekeleza miradi 70 ya kujenga miundombinu katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa. Ni wazi kuwa, nguvu kubwa iliyotumika kushughulikia changamoto hiyo ya dharura iliathiri utekelezaji wa baadhi ya miradi ya barabara iliyokuwa inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Changamoto nyingine kubwa tuliyokabiliana nayo mwaka huu ilikuwa ni uhaba wa fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani. Hali hii iliathiri shughuli nyingi za biashara na uzalishaji. Katika kukabiliana na athari hizo, tuliunda kikosi kazi cha wataalam kilichotafiti hali hio na kushauri hatua za kuchukuliwa. Ushauri ulituongoza kutengeneza Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Upatikanaji wa Fedha za Kigeni. Nafarijika kwamba, kufuatia utekelezaji wa Mkakati huo, upatikanaji wa fedha za kigeni umeimarika. Aidha, katika kuchukua hatua za kuuhami uchumi wetu, Serikali imefanya uamuzi wa kuweka akiba ya taifa ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania, ili kuongeza uhimilivu wa uchumi wetu.

Katika mwaka 2024, nchi yetu ilikumbwa na jinamizi la ajali za barabarani. Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonesha kuwa kati ya Januari hadi Disemba mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Na ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715. Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7% ya ajali zote. Niwatake Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi Tanzania kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.

Ndugu zangu,

Katika kutatua changamoto hizo nilizoziainisha, tumedhihirisha uwezo wetu Kitaifa wa kukabili changamoto zinazojitokeza. Ninawashukuru sana wananchi wote kwa ustahimilivu, ushirikiano na uelewa wenu tunapopatwa na changamoto za aina hio. Hakika, tunauaga mwaka huu, tukiwa na faraja zaidi kwamba hakuna changamoto tuliyoshindwa kuikabili tunaposimama pamoja kama Taifa.

Ndugu Wananchi;

Kama mlivyosikia, pamoja na changamoto tulizokabiliana nazo, mwaka tunaoumaliza, umekuwa wa mafanikio mengi yanayoimarisha ustawi wa wananchi. Katika mwaka tunaouanza muda mchache ujao, Serikali yetu itaendelea kuimarisha na kusambaza huduma za kijamii (Afya, Elimu, Maji na Umeme), tutachochea maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu, kuwaongezea fursa vijana na wanawake katika Biashara ndogo na za kati, na kuimarisha ustahimilivu wa Taifa.

Tutaendelea kukamilisha miradi ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo/Busisi ambalo limefikia asilimia 94, linalotazamiwa kulikamilisha mwezi Februari, 2025. Tutatoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kupunguza msongamano katika miji mikubwa kama vile Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma na kurahisisha usafiri na usafirishaji katika miji inayokua kwa kasi.

Miongoni mwa miradi hii ni mradi wa Barabara za Mzunguko katika Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 80, upanuzi wa Barabara ya Uyole-Ifisi-Songwe Airport jijini Mbeya ambao umefikia asilimia 20, na Awamu ya Tatu na Nne ya miundombinu ya barabara za mwendo kasi jijini Dar es Salaam, huku tukianza huduma kwenye Awamu ya Pili kwa njia ya Mbagala iliyokwishakamilika.

Mapema mwakani, tunatazamia Reli ya SGR, ianze kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma kiasi cha tani milioni 1 kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi kote inapopita. Vile vile, tutakamilisha kipande cha Mwanza hadi Isaka na kukifanya kianze kutoa huduma. Ujenzi wa vipande vyengine hadi Kigoma vitaendelea kujengwa kama ilivyopangwa.

Ndugu Wananchi,

Katika juhudi za kuvutia Michezo na Mikutano ya Kimataifa, Serikali itajenga viwanja na maeneo yenye sifa za Kimataifa kwa ajili hiyo. Mbali na ukarabati mkubwa unaofanywa katika viwanja vya mpira wa miguu vilivyopo, nchi yetu inaendelea kujenga viwanja vyengine kule Arusha na Dodoma. Kama mnavyofahamu mwezi Februari 2025, nchi yetu inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN na mwaka 2027 kutachezwa mashindano ya AFCON. Sambamba na miundombinu ya michezo tumeanza jitihada za kujenga na kurekebisha kumbi za mikutano katika viwango vya kimataifa ili tuweze kuvuta mikutano mingi zaidi. Kwa kuwa nchi yetu imebeba ajenda ya upatikanaji wa nishati safi Afrika, tumepata heshima ya kuwa wenyeji wa Mkutano kuhusu masuala ya nishati kwa Bara la Afrika (Africa Energy Summit) unaoandaliwa kwa ushirikiano wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika utakaofanyika mwezi Januari 2025.

Ndugu Wananchi,

Nchi yetu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Falsafa ya R4, inayohimiza Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga nchi yetu. Vile vile, tunaendeleza uhuru wa habari unaoashiriwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, na uhuru kutoa maoni kupitia vyombo mbalimbali; na hata uhuru wa kukusanyika na kujumuika.

Tutaendeleza mchakato wa kupata maoni ya Wananchi ili tukamilishe uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 mapema mwakani ili tuanze utekelezaji wake. Niwapongeze wananchi wote waliochangia katika mchakato huu, na niwasihi tuendelee kutoa maoni yetu hadi mchakato utakapokamilika.

Katika hatua nyingine, mwakani tutapokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ambayo itatusaidia kuboresha wigo na mifumo ya kodi, pamoja na kustawisha mazingira ya kibiashara nchini.

Katika utekelezaji wa mapendezo ya Tume ya Haki Jinai, mwakani 2025 tutakamilisha Sera na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki jinai. Tutaendelea pia kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji. Hadi sasa, jumla ya wananchi 495,552 wameshanufaika na Msaada wa Kisheria wa Kampeni ya Mama Samia Legal Aid chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Ndugu zangu;

Mwaka 2025 ni mwaka maalum kwa maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia nchini. Tutafanya Uchaguzi Mkuu kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani, na kwa upande wa Zanzibar, tutachagua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Miongoni mwa maandalizi ya awali ya uchaguzi huo, ilikuwa ni kufanya mashauriano na wadau wote wa kisiasa yaliyopelekea kurekebishwa kwa sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na Sheria ya Vyama vya Siasa. Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo. Nitoe rai kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya Nchi yetu ya kuwa na demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki.

Ndugu Wananchi;

Nilianza kwa kusema kuwa mwaka tunaoumaliza ulikuwa mwaka wa kihistoria, wenye mafanikio na unaotupa matumaini zaidi kuhusu kesho ya Taifa letu; na maelezo yangu yameonesha kwa nini nilisema hivyo. Nikihitimisha, niseme tu kwamba, mwenendo mzuri wa uchumi, uwezo wa kukabiliana na changamoto na kusimamia mipango yetu, na ari kubwa ya wananchi kujiletea maendeleo, vinatupa sote matumaini makubwa sana tunapoingia mwaka 2025. Nimalizie kwa kuwashukuru sana kwa imani na ushirikiano mkubwa mliotoa kwa Serikali na kutuwezesha kutekeleza vyema majukumu yetu. Nitoe shime kwa Watanzania kujenga ari na ujasiri wa kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, bidii na maarifa zaidi, katika kuchangia maendeleo yetu.

Katika mwaka ujao 2025 na mengine mingi ijayo, namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie afya njema na furaha mioyoni mwetu. Tujaaliwe uwepo wa Amani na Utulivu nchini, kheri na fanaka katika maisha yetu.

Mungu ibariki Afrika,

Mungu ibariki Tanzania,

Ahsanteni kwa kunisikiliza!



Nawatakia mwaka mpya wenye kheri.

Asante.

MTUHUMIWA WA “KUFUTA MADENI” YA MIKOPO AKIRI KOSA, AHUKUMIWA KIGOMA

KIGOMA, Septemba 4, 2026 — Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu Nicholaus Komba Mahitana maarufu kama Abdallah Mahimbo baad...