Tanzania na Uingereza zimeendelea kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, safari hii zikiweka mkazo katika uwekezaji, uongezaji thamani wa madini na namna sekta hiyo inavyoweza kuleta manufaa mapana zaidi kwa wananchi na uchumi wa Taifa.
Hatua hiyo imejidhihirisha leo jijini Dodoma, wakati Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, kwa mazungumzo yaliyolenga kuchambua fursa zilizopo katika sekta ya madini na maeneo mapya ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kuweka msisitizo katika kuhakikisha rasilimali zake za madini haziondoki nchini zikiwa malighafi pekee, bali zinaongezewa thamani ili kuchochea uwekezaji wa viwanda, kuongeza ajira, kukuza biashara na kupanua mchango wa sekta hiyo katika uchumi.
Kwa mantiki hiyo, kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini hakulengi tu kuongeza mitaji, bali pia kujenga minyororo ya thamani inayoweza kutoa nafasi kwa Watanzania kushiriki katika hatua mbalimbali—kuanzia uchimbaji na uchakataji hadi biashara na huduma zinazohusiana na sekta hiyo.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili pia zimeweka mkazo katika umuhimu wa ukuaji wa sekta ya madini unaoshirikisha wote, ili manufaa yatokanayo na rasilimali hizo yaweze kugusa maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo endelevu.
Mkutano wa Mhe. Mavunde na Balozi Young unaendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uingereza, huku diplomasia ya kiuchumi ikizidi kuwa daraja muhimu la kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo.
Tanzania na Uingereza zimeahidi kuendelea kufanya kazi pamoja katika maeneo yenye maslahi ya pande zote, kwa lengo la kuimarisha ustawi wa mataifa hayo mawili na kuhakikisha ushirikiano wao unazalisha matokeo yanayoonekana katika uchumi na maisha ya wananchi.









No comments:
Post a Comment