LUSAKA, Zambia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema, jijini Lusaka, ikiwa ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kihistoria, kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.
Rais Hichilema ameapishwa kuongoza Zambia kwa muhula wa pili, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 13, 2026.
Ushiriki wa Rais Samia katika sherehe hizo unaakisi undugu wa muda mrefu baina ya mataifa hayo mawili, uliojengwa tangu enzi za waasisi wa mataifa hayo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Dkt. Kenneth Kaunda.
Uhusiano huo umeendelea kupanuka kutoka katika undugu wa kihistoria na kisiasa na sasa kujikita zaidi katika biashara, uwekezaji, nishati, miundombinu na usafirishaji, maeneo ambayo yana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa nchi hizo mbili.
Miongoni mwa miradi ya kimkakati inayozidi kuunganisha Tanzania na Zambia ni ufufuaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ujenzi wa bomba jipya la mafuta la TAZAMA, pamoja na juhudi za kuimarisha muunganisho wa gridi za umeme kati ya Zambia, Tanzania na Kenya.
BIASHARA YAPAA, UWEKEZAJI WAONGEZEKA
Uhusiano huo pia umeendelea kutoa matokeo yanayoonekana katika biashara. Katika muhula wa kwanza wa Rais Hichilema, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Zambia iliongezeka kutoka Sh bilioni 320.978 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 820.359 mwaka 2024, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi hicho.
Zambia pia ni mtumiaji wa pili kwa ukubwa wa Bandari ya Dar es Salaam, jambo linaloifanya Tanzania kuwa lango muhimu la kibiashara kwa Zambia na nchi nyingine zisizo na bahari katika ukanda wa Kusini na Kati mwa Afrika.
Kwa upande wa uwekezaji, Zambia imewekeza katika miradi 29 nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 86.34, ambayo imezalisha ajira 1,204. Wakati huohuo, Watanzania wanamiliki hisa katika kampuni kubwa na za kati takribani 965 nchini Zambia.
Mahudhurio ya Rais Samia katika sherehe hizo, hivyo, hayabebi tu ujumbe wa kidiplomasia, bali yanaendelea kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kutumia uhusiano wake wa kihistoria na Zambia kufungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji, ajira na maendeleo ya wananchi wa mataifa yote mawili.
Kwa Tanzania na Zambia, urafiki uliojengwa na waasisi wa mataifa hayo unaendelea kuingia katika sura mpya—kutoka undugu wa kihistoria kuelekea ushirikiano wa kimkakati wa kiuchumi na maendeleo ya pamoja.







No comments:
Post a Comment