Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewahakikishia Watanzania kuwa atatekeleza majukumu yake kwa uadilifu, umakini na kujituma, huku akiahidi kutumia nafasi yake kumsaidia Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia wananchi na kusukuma mbele maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo, Septemba 1, 2026, alipowasalimu wananchi wa Mbuyuni, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, waliojitokeza kwa wingi kumlaki akiwa katika ziara binafsi mkoani humo.
Akizungumza na wananchi hao, Mhe. Ndejembi aliwashukuru kwa mapokezi yao na kuwaomba waendelee kumuombea Rais Samia pamoja na yeye, akisisitiza kuwa maombi na imani ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha viongozi kutekeleza dhamana waliyopewa kwa hekima na ufanisi.
Amesema anatambua ukubwa wa jukumu alilopewa na kwamba ataendelea kumsaidia Rais Samia kwa hekima, utii na uaminifu, huku akishirikiana kwa karibu na viongozi wa Serikali pamoja na wananchi katika kutekeleza majukumu yake.
“Endeleeni kumuombea Mheshimiwa Rais na kuniombea mimi pia, ili niweze kumsaidia kwa hekima na utii katika jukumu kubwa la kuwatumikia Watanzania,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Katika ujumbe uliopokelewa kwa shangwe na wananchi, Mhe. Ndejembi alirejea kauli aliyowahi kuitoa kwa wananchi wa Chamwino mkoani Dodoma mara baada ya kuapishwa, akisema: “Sitawazingua wana wala sitamzingua Mama.”
Kauli hiyo imebeba ujumbe wa dhamira yake ya kuwa mshirika mwaminifu katika uongozi, anayelenga kuimarisha mshikamano, ushirikiano na utendaji wenye tija kwa maslahi ya Taifa.
Awali, Makamu wa Rais aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambako alipokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Ziara hiyo ni miongoni mwa safari za mwanzo za Mhe. Ndejembi mkoani Kilimanjaro tangu kuapishwa kwake kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.





No comments:
Post a Comment