Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeahirisha ziara yake katika miradi ya Samia Housing na 711 Kawe inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Mwenyekiti wa PIC, Masanja Kadogosa amewatangazia wajumbe wa kamati hiyo kuwa uamuzi huo umefikiwa kufuatia kifo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi, kilichotokea leo Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kabla ya kuahirishwa kwa ziara hiyo, Kamati hiyo ilikuwa imetembelea mradi wa Samia Housing Scheme uliopo Kawe na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na NHC katika eneo hilo. Akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, Mwenyekiti Kadogosa alipata fursa ya kusikiliza maelezo ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah.
Katika maelezo yake, Mkurugenzi Mkuu alibainisha kuwa mradi huo wa majengo ya ghorofa kumi, unaojumuisha jumla ya nyumba 560, ulitekelezwa kikamilifu na wahandisi wa Shirika la Nyumba la Taifa, hatua inayodhihirisha uwezo wa ndani wa taasisi hiyo katika kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Akitoa ufafanuzi wa kina kuhusu mradi huo, Msimamizi wa Utekelezaji, Mhandisi Grace Musita, alisema kuwa majengo hayo yanajumuisha nyumba za vyumba vitatu zenye ukubwa wa mita za mraba 89, ambazo zimeuzwa kwa shilingi milioni 192.7.
Aidha, kuna nyumba 160 za vyumba viwili zenye ukubwa wa mita za mraba 68, zilizouzwa kwa shilingi milioni 147, pamoja na nyumba ndogo zenye ukubwa wa mita za mraba 21.2 zilizouzwa kwa shilingi milioni 38.8.
Aliongeza kuwa mradi huo ulianza Novemba 2022 na kukamilika Juni 2025, ambapo kwa sasa wakazi tayari wameanza kuishi, huku Shirika likiendelea kushughulikia dosari ndogo ndogo zinazojitokeza ili kuboresha zaidi huduma kwa wateja.
Mhandisi Musita alibainisha kuwa mradi huo umeleta manufaa makubwa kijamii na kiuchumi, ikiwemo kuzalisha ajira 11,800 kwa mafundi na wataalamu mbalimbali. Pia wanafunzi 630 kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) walipata mafunzo ya vitendo, ambapo kati yao wanafunzi 47 walipata ajira za kudumu na muda mfupi. Vilevile, vibarua 100 wasio na elimu rasmi lakini wenye nidhamu walipata ajira kupitia mradi huo.
Alisisitiza kuwa NHC ilitekeleza mradi huo kwa viwango vya juu kwa kuwa mkandarasi na mbunifu, huku malighafi zote zilizotumika zikifanyiwa vipimo na taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), pamoja na kukaguliwa na mamlaka husika za Kinondoni na wataalamu wa ndani wa NHC.
Aidha, alieleza kuwa matumizi ya mitambo ya kisasa inayomilikiwa na Shirika, ikiwemo mtambo mkubwa wa kuzalisha zege, magari ya kusafirisha zege na pampu, yalichangia kukamilika kwa mradi huo kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
Mradi wa Samia Housing Scheme Kawe umegharimu jumla ya shilingi bilioni 49, ambapo hadi sasa takribani shilingi bilioni 45 tayari zimetumika.
Hata hivyo, ziara ya Kamati hiyo haikuweza kuendelea katika mradi wa Kawe 711 kufuatia tukio hilo la msiba. Akisoma kanuni za kudumu za Bunge, Afisa Sheria wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Elizabeth Malogo, alinukuu kanuni namba 176 inayotaka shughuli za Bunge kuahirishwa endapo Mbunge atafariki dunia wakati wa shughuli za Bunge, ili kutoa nafasi kwa maombolezo.
No comments:
Post a Comment