Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Serikali imesema uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya usafiri na usafirishaji Kanda ya Ziwa utachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani za Ukanda wa Maziwa Makuu, huku ikiwahimiza wawekezaji wa sekta binafsi kutumia fursa zinazojitokeza katika eneo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa leo, jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali ya serikali.
Msigwa alisema ujenzi wa meli kubwa ya kisasa ya New MV Mwanza ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya usafiri katika Ziwa Victoria, hatua itakayofungua fursa mpya za kiuchumi hususan katika sekta ya utalii na biashara.
Alisisitiza kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji, hivyo wadau wa utalii wanapaswa kujitokeza kuwekeza ili kunufaika na ongezeko la shughuli za kiuchumi katika Kanda ya Ziwa.
Msemaji Mkuu huyo wa Serikali alisema, meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo itakuza biashara na uchumi, itaimarisha usafiri wa majini kati ya Mwanza na miji ya Jinja na Port Bell nchini Uganda pamoja na Kisumu nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Msigwa, hatua hiyo itaongeza mzunguko wa biashara na kukuza uchumi wa bidhaa mbalimbali zikiwemo pamba, madini, samaki, nyama na maziwa, huku akionya kuwa serikali haitaridhika kuona uwekezaji huo mkubwa unakosa tija.
Akizungumzia mradi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR), Msigwa alisema ni uwekezaji mkubwa wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 12 unaolenga kuimarisha uchumi wa taifa na nchi jirani.
Alieleza kuwa ujenzi unaendelea katika vipande mbalimbali, huku lengo likiwa ni kufikisha reli hiyo Mwanza ifikapo mwaka 2028 ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kuongeza ufanisi wa biashara za kikanda.
Aidha, alisema serikali inaendelea na mipango ya kujenga reli ya kisasa inayotumia umeme yenye uwezo wa kusafirisha tani 10,000 za mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam pamoja na meli nyingine ya mizigo katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Alibainisha kuwa uwekezaji huo wa kimkakati utaongeza matumizi ya reli, kukuza biashara na kuchochea mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi, huku Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikilenga kufikia pato la mtu mmoja mmoja la dola 7,000 kwa mchango mkubwa wa sekta binafsi.

No comments:
Post a Comment