Tuesday, March 31, 2026

VIONGOZI WAUNGANA KUAGA MWILI WA MAREHEMU MHE. WILLIAM LUKUVI IRINGA

 










Iringa, Machi 31, 2026 — Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewasili nyumbani kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, Marehemu Mhe. William Lukuvi, kilichopo Kijiji cha Idodi mkoani Iringa, kuongoza mamia ya waombolezaji katika shughuli za maziko zilizofanyika leo.

Ujio wa kiongozi huyo umeambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika utumishi wa umma.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba alieleza kuwa taifa limepoteza kiongozi mwenye uzoefu, aliyekuwa mstari wa mbele kusimamia sera, uratibu wa shughuli za Serikali na utetezi wa masuala ya watu wenye ulemavu. Alisisitiza kuwa mchango wa Marehemu Lukuvi utaendelea kukumbukwa na kuthaminiwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Marehemu Mhe. William Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu. Enzi za uhai wake, alitumikia nafasi mbalimbali za uongozi serikalini kwa weledi na uzalendo mkubwa, akijijengea heshima ndani na nje ya Bunge.

Maziko hayo yamefanyika katika kijiji chake cha nyumbani cha Idodi, huku yakihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi waliokusanyika kumlaki na kumuaga kiongozi wao kwa heshima na majonzi makubwa.

Taifa linaendelea kuungana na familia, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Isimani katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi.

No comments:

VIONGOZI WAUNGANA KUAGA MWILI WA MAREHEMU MHE. WILLIAM LUKUVI IRINGA

  Iringa, Machi 31, 2026 — Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewasili nyumbani kwa aliyekuwa Wazir...