Mwenyekiti wa HoneyGuide Foundation Olekiri Mbai akikabidhi gari aina ya Suzuki Jimmy kwa Mkuu wa Wilaya wa Monduli Iddi Hassan ikiwa ni msaada wa shirika hilo katika kusaidia hifadhi ya wanyamapori ya Randilen.
Na Woinde Shizza,Arusha.
Hifadhi ya Wanyamapori ya Randlen Community Wildlife Management, iliyoko Arusha wilayani Monduli imekabidhiwa gari aina ya Suzuki Jimmy kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya ujangili na uharibifu wa mazingira katika hifadhi hiyo ya jamii.
Akipokea gari hilo kutoka Shirika la Honey Guide, Mkuu wa Wilaya ya Monduli Iddi Hassan alisema, gari hilo litasaidia juhudi za kupambana na ujangili katika wilayani humo na kukuza utalii endelevu kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kupokea gari hilo, Hassan amesema msaada huo utasaidia kuimarisha shughuli za uhifadhi Wilayani humo, kwa kuwa kuwa hifadhi hiyo ni hifadhi pekee inayofanya vizuri katika wilaya hiyo na kunufaisha vijiji tisa vinavyozunguka hifadhi.
Alisema,msaada huo wa gari utaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ujangili hasa hasa katika kipindi hiki ambacho wanajipanga katika kuzuia uvunaji holela wa maliasili katika hifadhi hiyo pamoja na kuzuia ujangili
kwa upande wake, mwenyekiti wa Honey Guide Foundation Olekiri Mbai alisema, wameamua kutoa msaada huo unaogharimu kiasi cha shilingi milioni 25 ili kusaidia shughuli za uendeshaji wa hifadhi hiyo ya jamii (WMA) katika kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kuwa uhifadhi unafanyika kwa namna ambayo unanufaisha wanajamii wa Monduli.
“Kumekua na changamoto ya Hifadhi nyingi kutokuwa na Meneja lakini hifadhi ya Randilen ni hifadhi pekee yenye meneja ambaye anasimamia shughuli zote za utawala hivyo msaada huu wa gari utamsaidia kutekeleza majukumu yake ya kila siku” Alisema Olekiri
Mwenyekiti wa Hifadhi hiyo Daniel Alais ameshukuru shirika la Honey Guide kwa kutoa msaada huo ambao utasaidia kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ujangili na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kurahisisha utendaji kazi wa kila siku.
No comments:
Post a Comment