Saturday, January 04, 2025

Waziri Ndejembi Ajitosa Mgogoro wa Fidia Kurasini Uliochukua Miaka 17







Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka wa mgogoro wa fidia uliodumu kwa miaka 17 katika eneo la Kurasini, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam. Mgogoro huo unahusisha wananchi 41 ambao hawajapokea fidia baada ya eneo lao kutwaliwa mwaka 2008 na kumilikishwa kwa Kampuni ya Tanzania Road Haulage.

Mhe. Waziri alikutana na wawakilishi wa wananchi hao Januari 4, 2025, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Katika kikao hicho, Mhe. Ndejembi alisisitiza dhamira ya Serikali ya kutatua changamoto za wananchi kwa haki na kwa wakati. Ameahidi kufanya ziara ya haraka katika eneo la mgogoro ili kushughulikia suala hilo kwa kina na kupata suluhu ya kudumu.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, pamoja na mwakilishi wa Kampuni ya Tanzania Road Haulage. Katika mazungumzo, wananchi walieleza masikitiko yao ya kukosa fidia kwa muda mrefu, huku wakisubiri hatua za Serikali kuwapatia haki yao.

Mhe. Mapunda alieleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanazokabiliana nazo wananchi hao na itaendelea kushirikiana na wadau husika kuhakikisha haki inapatikana bila kuchelewa.

Hatua ya Waziri Ndejembi kuingilia mgogoro huo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi, ambao wamekuwa wakilalamikia kupuuzwa kwa muda mrefu. Ziara ya Waziri katika eneo hilo inatarajiwa kutoa mwanga mpya wa suluhisho la changamoto hiyo ambayo imeathiri maisha ya familia nyingi.

Mgogoro wa fidia katika eneo la Kurasini ni moja ya changamoto zinazowakumba wananchi katika maeneo ya ardhi nchini, na hatua ya Serikali kushughulikia masuala haya inaonyesha dhamira ya dhati ya kulinda haki za wananchi na kuhakikisha maendeleo ya haki kwa wote.


Rais Samia Aipa Kipaumbele Sekta ya Afya, Aimarisha Huduma Nchini










Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amepongeza juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya nchini, akisema dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uhakika bila kulazimika kuzifuata nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Afya Kizimkazi, Wilaya ya Kusini Unguja, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Balozi Kombo alisema, "Vission yake ni kwamba wasitoke wagonjwa kutoka Zanzibar kwenda kutibiwa nje ya nchi. Watatibiwa hapa hapa, huo ndiyo muono wake."

Alifafanua kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kizimkazi ni sehemu ya mpango mkubwa wa Samia Foundation unaolenga kuboresha huduma za afya nchini. "Hiki Kituo cha Kizimkazi ni asilimia ndogo sana ya mpango mzima wa Mama Samia Foundation, lakini muundo na vission yake ni kubwa zaidi," alisema.

Balozi Kombo alieleza kuwa yeye pamoja na Dkt. Jakaya Kikwete walipewa jukumu maalum la kwenda kujifunza mifumo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute ili kuimarisha utekelezaji wa mpango huu. Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhandisi aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Samia Foundation, akisema uteuzi huo utasaidia kutafsiri ndoto pana ya Rais Dkt. Samia kwa manufaa ya Watanzania wote.

Akizungumzia hatua za maendeleo katika sekta nyingine, Waziri Kombo aliipongeza serikali ya Rais Samia kwa kuwekeza katika upatikanaji wa nishati ya uhakika, hatua ambayo imeungwa mkono na viongozi wa ndani na nje ya Afrika.

Kituo cha Afya Kizimkazi kinatarajiwa kuwa mfano wa miradi mingine itakayotekelezwa chini ya Samia Foundation ili kuimarisha ustawi wa wananchi na kupunguza mzigo wa kutafuta matibabu nje ya nchi.


Friday, January 03, 2025

WAZIRI NDEJEMBI AKUTANA NA WAMILIKI WA SHAMBA LA KWASHEMSHI LA KOROGWE

 










WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amekutana na kufanya kikao cha pamoja na Wamiliki wa Shamba la Sisal Estate “Kwashemshi” lililopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa muda mrefu baina ya wananchi wa eneo hilo na wamiliki hao.

Kikao hicho kimefanyika Januari 03, 2025  Ofisi za Makao Makuu ya Wizara zilozopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Netho Ndilito, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mzava, Mkurugenzi wa Halmashauri ua Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango, Viongozi wa Sisal Estate wakiongozwa na Wakili Ndurumah Magembe na Mathew Kashindye pamoja na wajumbe wa Mejimenti na wataalamu wa wizara.

WAZIRI CHUMI APONGEZA JUHUDI ZA UPANDAJI MITI NA UHIFADHI MISITU ZINAZOFANYWA NA TFS







Mbunge wa Jimbo la Mafinga na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi (Mb) ametembelea TFS-Shamba la Miti Sao Hill ili kuona namna shughuli za upandaji miti na uhifadhi wa misitu zinazofanywa na Shamba leo Januari 03, 2025.

Waziri Chumi ameipongeza TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill kwani imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi kwa wakazi wanaolizunguka shamba kwani limekuwa likichangia uendelezaji wa miradi mingi ya maendeleo hususani katika Wilaya ya Mufindi na Taifa kwa ujumla.

Aidha amesema kuwa Shamba la Miti Sao Hill limekuwa msingi mkubwa wa uzalishaji wa malighafi za viwanda hali iliyochangia kukua na kuongezeka kwa uwekezaji wa viwanda vya mazao ya misitu katika Wilaya ya Mufindi.

Pamoja na hayo amewataka wahifadhi kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaolizunguka shamba ili kuendeleza uhusiano mzuri iliopo baina ya Shamba na wananchi pamoja  na kuongeza jitihada za ulinzi wa rasilimali misitu dhidi ya majanga ya moto yanayoweza kujitokeza na ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kuharibu rasilimali hiyo.

Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa viongozi wa ngazi zote Wilayani Mufindi kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinafanyika kwa ufasaha na kuhakikisha elimu ya uhifadhi inawafikia wananchi wote.

Wednesday, January 01, 2025

JKCI imefungua tawi jipya katika jengo la Oyster Plaza

 

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefungua tawi jipya kuwapa wananchi nafasi kuwa karibu na huduma ili pale wanapopata changamoto za kiafya wasichukue muda mrefu kufuata huduma zilipo.

Tawi hilo lililopo katika jengo la Oyster Plaza Haile Salassie barabara ya Ali Bin Said limeanza kutoa huduma bobezi za moyo leo lengo likiwa kuwapa fursa wananchi kupata huduma katika maeneo tofauti na ilipo taasisi hiyo na kupunguza msongamano uliopo katika makao makuu ya taasisi

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imekuwa ikiwafikia wananchi walipo kwa kuwafuata mikoani na kuwapa huduma bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Tumekuwa tukiwafuata wananchi mikoani kuwapa huduma sasa tumeamua kuanzisha matawi ya Taasisi, hii pia ni sehemu ya kuwafuata wananchi mahali walipo kwani hapa tulipo leo tunawapa nafasi wananchi wa eneo hili kupata huduma kwa karibu lakini pia hata wale wanaotoka mbali tunawapa nafasi ya kupunguza msongamano uliopo makao makuu”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema JKCI pia inaendelea kuyafikia makundi ya watu mbalimbali kuwapa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo ili makundi yote yanayofikiwa yaweze kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na kuwa na tabia za kuchunguza afya zao mara kwa mara.

“Tumekuwa tukiwafikia watu tofauti kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kipindi hiki cha kufunga mwaka tunatoa huduma kwa wasanii, na wanamichezo kila jumamosi na jumapili katika kliniki yetu ya Kawe, wanahabari tulishawapa huduma hii huko nyuma ila tutakuja kuwarudia tena”

Aidha Dkt. Kisenge ametoa wito kwa wasanii na wanamichezo kuendelea kujitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwani kinga ni bora kuliko tiba na kama watagundulika mapema watakuwa kwenye nafasi ya kutibiwa magonjwa hayo mapema na kupona.

Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kliniki ya JKCI iliyopo Oyster Plaza Haile Salassie ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuwa na maono ya kusogeza huduma karibu na jamii na kuipa jamii ari ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Mwananchi huyo ambaye hakutaka jina lake lifahamike alisema huduma za afya zikiwa karibu na jamii zinatoa motisha kwa jamii kufika hospitali na kufanya uchunguzi wa afya hivyo kupunguza matumizi ya dawa yasiyo sahihi.

“Mara nyingi tumekuwa tukipata hali za maumivu ama kuumwa kichwa, mafua, kikohozi, kifua tunaenda duka la dawa kununua dawa tu bila ya kufanya uchunguzi lakini kama tutakuwa karibu na Hospitali itatusaidia kwenda kupima kwanza na kupata ushauri wa daktari kabla ya kununua dawa”, alisema.

Naye msimamizi wa kliniki hiyo Nyanjura Nyaruga alisema kliniki hiyo imeanza kwa kuwa na mwitikio mkubwa wa watu waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.

Nyanjura ambaye pia ni Afisa Muuguzi mbobezi wa magonjwa ya moyo alisema katika kliniki hiyo wanatoa huduma za kliniki ya moyo, kliniki ya mishipa ya damu, kliniki ya magonjwa ya moyo kwa watoto, huduma za maabara, huduma za mazoezi kwa wagonjwa wa moyo na huduma za dharura.

“Wananchi wasisite kufika katika kliniki yetu hii kwani tumejipanga kufikisha huduma bora kwenu na tutakuwa tukitoa huduma zetu kwa muda wa masaa ishirini na nne”, alisema Nyanjura

WAZIRI KOMBO AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA YA MAGHARIBI B








Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amesema kuimarika kwa miundombinu ya Mahakama ni hatua muhimu itakayowawezesha wananchi kupata huduma katika mazingira mazuri, salama na rafiki.

Ameyasema hayo leo Januari 1, 2025 wakati akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B huko Kisakasaka, Zanzibar.

Balozi Kombo amesema, kwa miaka mingi mahakama zimekuwa na changamoto ya miundombinu ya majengo na Serikali inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kumaliza changamoto hizo kwa kujenga majengo mapya na ya kisasa.

"Kwa mfano jengo lililokuwa likitumiwa na Mahakama ya Magharibi B pale Mwanakwerekwe lilikuwa finyu mno kiasi cha kusababisha msongamano mkubwa na kuwapa usumbufu waliofuata huduma mahali pale," alisema Mhe. Kombo.

Waziri huyo ameongeza kuwa, pamoja na ufinyu huo, pia halikuwa rafiki kutokana na kukosekana nafasi kwa ajili ya maofisa wa Mahakama.

Vilevile, kukosekana kwa huduma za watu wenye mahitaji maalumu na maegesho kulisababisha muda mwingi wananchi walikuwa wanazagaa kwa kukosa sehemu tulivu ya kusubiri huduma.

Amesema, hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kuchukua hatua za makusudi kuja na mradi wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya mikoa na wilaya Unguja na Pemba.

Pia, amesema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Kwa upande wa Unguja, Balozi Kombo amesema, mradi huo wa Loti Nambari 2 unajumuisha majengo manne ambayo ni: Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini, Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Mahakama ya Mkoa wa Kusini na Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B.

Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya majengo ya ofisi, hivyo ni wajibu wa watumiaji wa miundombinu hii na wananchi kwa ujumla kuitunza ili iweze kudumu kwa miaka mingi ijayo.

DC MALINYI:ZOEZI LA KULIPA FIDIA WANANCHI NGOMBO LINAKWENDA VIZURI

 





Na Beatus Maganja, Malinyi

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amesema zoezi la kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo kilichopo ndani ya Pori la Akiba Kilombero Mkoani Morogoro linaendelea vizuri ambapo asilimia 93 ya wananchi wote tayari wamekwishalipwa fidia zao kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi katika Hifadhi hiyo na asilimia 7 ya wananchi waliosalia wanaendelea kushughulikiwa ili kukamilisha malipo yao.

Akizungumzia zoezi hilo jana Desemba 31, 2024 wilayani humo Mhe. Sebastian amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi billioni 6.9 kulipa wananchi 1,056 ili waweze kuhama kwa hiari kutoka maeneo ya Hifadhi huku akitoa maelekezo kwa watendaji wa vijiji 32 wilayani Malinyi kuwapokea ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.

“Kwanza si kweli kwamba wananchi wa Ngombo hatujawaambia mahali pakwenda. Katika barua yangu ya tarehe 4 Disemba, 2024 niliyowaandikia watendaji wa vijiji 32 vilivyo ndani ya wilaya ya Malinyi, nilitoa maelekezo ya kuwapokea wananchi wa Kijiji cha Ngombo wanaopisha shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Kilombero, na ndivyo inavyofanyika na pia nilielekeza watendaji hao wawataarifu wananchi wote kupitia mikutano ya hadhara” amesema

“Na tangu wananchi wangu wa Ngombo walipoanza kuhama kwenda katika maeneo yao waliyokwenda, sijapata lalamiko lolote kwa simu au kwa mdomo kwamba wamezuiliwa kukaa mahali fulani na kwa taarifa nilizonazo baadhi yao wamehamia sehemu mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Pwani na Halmashauri ya Mlimba. Kwahiyo mimi ninaamini mambo yanakwenda vizuri na ndivyo ilivyo” amesisitiza Sebastian.

Kuhusu wanafunzi waliokuwa wanasoma shule katika Kijiji cha Ngombo, Mkuu huyo wa wilaya amesema amekwishatoa maelekezo kwa Afisa elimu kuwapokea na kuwasajili katika shule zilizopo kwenye vijiji vilivyo ndani ya wilaya hiyo bila masharti yoyote ili waweze kusoma kwa uhuru.

Aidha,Sebastian amesema wananchi wa Kijiji cha Ngombo waliandaliwa mapema kwa kupewa elimu juu ya malipo ya fidia ili weweze kuhama kutoka katika eneo la Hifadhi ya Kilombero tangu mwezi Agosti, 2024. Hivyo, walikuwa na uelewa kuhusu zoezi hilo na amewataka kuepuka watu wenye nia ovu ya kupotosha dhamira njema ya zoezi hilo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Biro Elizabeth Mnenuka amekiri kupokea zaidi ya wananchi 50 katika Kijiji cha Biro na wengine zaidi ya 30 katika Kijiji cha Mbalinyi na kuongeza kuwa baadhi yao tayari wameshapatiwa maeneo kwa ajili ya kuendeleza kwa kilimo na makazi.

Nao wananchi waliohamia Kijiji cha Biro kutoka Kijiji cha Ngombo wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwalipa fidia zao Kwa wakati ambazo zimewasaidia kuhama na kuanza maisha mapya katika vijiji jirani.

“Toka nitoke Kijiji cha Ngombo ambapo tuliondolewa kisheria kwakweli sina changamoto yoyote kimaisha, niko vizuri naishi vizuri na familia. Naishukuru Serikali, fidia nimepata kwahiyo mpaka hapa sina neno na Serikali” amesema Daudi Deodatus Lyambu aliyekuwa mkazi wa Ngombo ambaye sasa amehamia Kijiji cha Biro.

Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 17 Februari, 2023 Pori la Akiba Kilombero lenye sehemu A na B lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 64 kufuatia kupandishwa hadhi kwa sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero kuwa Pori la Akiba.

Aidha, kufuatia kuanzishwa kwa Pori la Akiba Kilombero, masharti na sheria zinazosimamia eneo hilo zilibadilika ambapo shughuli zote za kibinadamu zimesitishwa isipokuwa zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria. Lengo la Serikali likiwa ni kuimarisha usimamizi wa eneo hilo kwa kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori ili kuongeza tija ikiwemo upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Mwl. Nyerere.

MTUHUMIWA WA “KUFUTA MADENI” YA MIKOPO AKIRI KOSA, AHUKUMIWA KIGOMA

KIGOMA, Septemba 4, 2026 — Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu Nicholaus Komba Mahitana maarufu kama Abdallah Mahimbo baad...