Saturday, March 31, 2018

WATALII WENGI WAZIDI KUTEMBELEA TANZANIA - WAZIRI KIGWANGALLA



Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akipokelwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudensi Milanzi mjini Dodoma jana ambapo alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 25 wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi kufikia 1,327,143 mwaka 2017 hali iliyopelekea kuongezeka kwa mapato ya Serikali.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika mjini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema Wizara yake itaendelea kuvutia watalii wengi zaidi ili kukuza utalii na kuongeza pato la Taifa. 

“Mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Kimarekani Bilioni 2.2 mwaka 2017” alisema Dk. Kigwangalla.Akifafanua Dkt. Kigwangala amesema lengo la Serikali ni kuona mafanikio haya yanazidi kuimarika, hivyo kila mtumishi katika Wizara hiyo lazima atimize wajibu wake ipasavyo katika kutimiza lengo la Wizara hiyo ambalo ni kuhifadhi na kusimamia maliasili, malikale na kuendeleza utalii.

Aliongeza kuwa ili kufanikisha majukumu ya Wizara hiyo ipasavyo ni muhimu kuwa na bajeti ambayo itawezesha kushughulikia changamoto za migogoro ya mipaka katika maeneo ya hifadhi, kufanya mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali, upungufu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi, kutoa elimu ya maadili na kusimamia watumishi. 

Alisema Wizara yake itaendelea na mapambano dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara, magogo na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo.Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudensi Milanzi amesema kuwa Wizara hiyo itazingatia ushauri utakaotolewa na Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ili kuongeza tija katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Wizara itaendelea kupambana dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara na magogo na kuwachukulia hatua kali watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo “ Alisisitiza Meja Jenerali Milanzi.Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliendelea na utaratibu wa kuendeleza watumishi katika mafunzo ya aina mbalimbali kama ifuatavyo:-Jumla ya watumishi wanne (4) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu nje na ndani. Aidha, mtumishi mmoja(1) yupo nje ya nchi.

Watumishi wengine kumi na moja (11) walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Mafunzo haya yalihusu watumishi wa kada mbalimbali.Jumla ya watumishi saba (7) wamehudhuria mafunzo ya ujasiliamali unaohusiana na maandalizi ya kustaafu. Aidha, Wizara bado inaendelea na utaratibu wa kuwaandaa watumishi wote wanaokaribia kustaafu kuhakikisha wanapata mafunzo hayo. 

Akifunga mkutano huo wa siku moja Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Japhet Hasunga aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufikia lengo lililokusudiwa la uhifadhi wa maliasili, malikale na kuendeleza Utalii.
Waziri wa Mali Asili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akihutubia Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika mjini Dodoma jana.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudensi Milanzi akizungumza na Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wa baraza wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. HamisI KigwangalLa (katikati) akiimba wimbo wa mshikamano pamoja na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudensi Milanzi pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la Wafanyakazi.
Baadhi ya ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Wakiimba wimbo wa mshikamano wa wafanyakazi wakati wa mkutano huo uliofanyika mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akisalimiana na Katibu Mteule wa Tughe Tawi la Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita muda alipowasili kufunga mkutano huo wa baraza. Katikati anayemtambulisha kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.
Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara wizara hiyo, Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi muda mfupi kabla ya kufunga mkutano huo wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na watumishi wa wizara hiyo wakatika akifunga mkutano huo wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara hiyo walioshiriki baraza hilo.
Baadhi ya watumishi wa Wizara na wajumbe wa baraza hilo.

No comments: