Wananchi pamoja na wanachama wa CUF wa Kijiji cha Ughandi wakimsubiri kwa hamu Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Prof.Ibrahimu Lipumba kumsikiliza sera za chama na kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho, Delphina Mngazija.
Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof.Ibrahimu Lipumba (wa kwanza kutoka kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa wanawake wa chama hicho, Salama Masudi kwenye viwanja vya mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Ughandi, wilaya ya Singida Vijijini kabla ya kuongea na wananchi hao.(Picha zote Na Jumbe Ismailly).
Na,Jumbe Ismailly, SINGIDA
MKURUGENZI wa wanawake wa Chama Cha Wananchi (CUF) Taifa, Salama Masudi amesema kuwa sera ya viwanda nchini haiwezi kufanikiwa iwapo hatutaendana na mabadiliko makubwa ya soko la wakulima na ikiwezekana katika mpango mzima wa mapinduzi ya kilimo wenye lengo la kuwawezesha wakulima wa chini kuelekea soko kuu la dunia kuweza kuinua kipato kutoka kwa wananchi maskini kabisa.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wakati wa kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida Kaskazini uliofanyika katika Kijiji cha Ughandi, wilaya ya Singida vijijini.
Alifafanua Salama kwamba baada ya wakulima kuwa wamewezeshwa hususani katika maeneo hayo wanayotoka ambapo kilimo ndicho uti wa mgongo,basi kuwezeshwa kwa viwanda hivyo kunawezekana kabisa kutoka maeneo muhimu kulingana na mazao yanayotokana na uwezeshwaji wa viwanda hivyo.
Hata hivyo Salama alisisitiza pia kwamba katika miaka yote wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakipelekewa wagombea wanaume ambao wameshindwa kukidhi haja zao kwa kuwa wanaguswa na matatizo yanayowashika wanawake wenyewe,lakini mwaka huu CUF imewaletea mwanamama huyo mahiri na ambaye wanaamini ndiye suluhisho pekee la matatizo ya wananwake.
“Tunaomba kwa namna ya pekee na utulivu mkubwa tunaomba kura kwa akina mama mtusaidie kuweza kumsaidia mama Delphina Mngazija kwa kuwa ninyi ndio wengi kabisa katika upigaji wa kura na mnatumiwa kuwa chambo cha kuwakandamiza wananchi”alisisitiza Salama.
“Tumewaletea mama huyo anaguswa na changamoto zinazotukbili sisi wanawake,wengi wetu hapa tunaumizwa na sera mbovu,tumekuja na kampeni pekee kupitia mgombea wa chama chetu ‘Mwanamke tua ndoo maana yake akiwa sauti ya Bunge kupitia Singida kaskazini anaweza kuongea na serikali kupitia mifuko ya jimbo ili aweze kuleta visima vitakavyosaidia akina mama kupunguza adha ya maji katika maeneo mnayoishi”alifafanua
Hata hivyo Mkurugenzi huyo wa wanawake Taifa alionyesha pia kukerwa na baadhi ya watu au vyama vinavyosusia chaguzi,na kwamba vitendo vya aina hiyo ni kinyume na demokrasia pamoja na upatikanaji wa maendeleo ya nchi.
Hivyo Salama alitumia wasaa huo kutoa tahadhari kwa wananchi wa jimbo la Singida kaskazini kutosusia chaguzi kwani kwa kufanya hivyo wanapoteza haki zao za msingi za kikatiba.
“Niwaombe wananchi wa kata hii,hususani katika kata hii ya Ughandi hususani wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mtupigie kura chama cha wananchi CUF,siyo dhambi kabisa iwapo wananchi wenyewe kwa mapenzi mliyonayo mmemchagua mtu ambaye ni chaguo lenu na anayewahurumia,lakini badala yake ameletwa mtu kupitia kwenye njia zisizoeleweka”alibainisha Mkurugenzi.
Hata hivyo mkurugenzi huyo alitumia mkutano huo kuwashawishi wananchi wa kata ya Ughandi kutokichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kile alichokiita ni nyimbo zilizokosa utekelezaji wake.
Akizungumzia CUF kiongozi huyo wa chama alibainisha kuwa katika kipindi cha takribani miaka ishirini tangu kuanzishwa kwake kimekuwa kikitetea maslahi ya watanzania wote na kutoa mfano kwamba chama hicho kinachoongozwa na Prof.Ibrahimu Lipumba amekuwa akiandaa mijadala mbali mbali iliyochangia kuleta maendeleo.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Singida kaskazini kupitia Chama Cha Wananchi (CUF),Delphine Mngazija akiomba kura kwa wananchi wa Kijiji cha Ughandi aliahidi kwamba endapo watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao ataenda Bungeni kutetea akina mama waondokane na adha ya kutembea na mabeseni,ndoo pamoja na mipira ya kujifungulia.
Alifafanua mgombea huyo kwamba maana mama mjamzito akishakuwa na ujauzito hupatwa na mawazo ya kuondoka kwenda kujifungua kwa kuanza kufikiria ni namna gani atakavyonunua ndoo,beseni na mipira.
“Ninawaomba ridhaa yenu akina mama mambo ya kwenda hospitali na kwenda kubeba mabeseni niende kuwatetea nipigane na hilo kwa akina mama kwa sababu taasisi ya afya ina mambo mengi kwani mama akijifungulia nyumbani akimchukua mtoto wake kumpeleka hospitali hatapokelewa”alisisitiza mgombea huyo.
No comments:
Post a Comment