Thursday, February 10, 2011

Mkapa: Kura ya maoni Sudan Kusini ilikuwa ya uhuru


Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya watu watatu iliyoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuangalia mchakato wa maandalizi na hatimaye upigaji kura ya maoni katika Sudan ya Kusini. Ameliambia Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa matokeo ya kura hiyo ni ya haki, huru na kuaminika.

Rais Mstaafu Mkapa, ameyasema hayo siku ya jumatatu wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa yake mbele ya Baraza hilo, ikiwa ni siku mbili zimepita tangu kutangazwa rasmi matokeo ya kura hiyo yaliyoonyesha, kuwa asilimia 98.83 ya wananchi waliopiga kura wameamua kujitenga na kuwa na taifa lao.

“ Timu yetu inapenda kuhitimisha kwamba matokeo ya kura hiyo ya maoni yameonyesha matakwa ya wananchi wa Sudan ya Kusini, mchakato mzima wa upigaji wa kura ulikuwa wa uhuru, haki na wa kuaminika”. Anasema Mkapa.

Akasema kukamilika kwa zoezi hilo ni moja ya hatua muhimu sana kuelekea upatikanaji wa amani ya kudumu.

Baada ya matokeo ya mwisho ya kura hiyo kutangazwa na baada ya pande zote mbili kuridhia na kuyakubali, huku Jumuia ya Kimataifa ikiyaridhia, Taifa huru la Sudan ya Kusini litakaribishwa rasmi katika Jumuia ya Kimataifa Julai 9 mwaka huu.

Mkapa ambaye timu yake ilitembelea Sudan ya Kusini mara tano katika kipindi cha kuelekea upigaji wa kura hiyo. Amelieleza Baraza hilo kwamba, katika kutathimini mchakato huo wote, timu yake ilizingatia misingi yote iliyoainishwa katika Sheria ya Kura ya Maoni ya Sudan ya Kusini. Na kwamba Timu imejiridhisha kuwa zoezi lilifanyika katika mazingira ya uwazi wa hali ya juu.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...