Tuesday, February 03, 2026

RAIS SAMIA AANZA ZIARA YA KIKAZI DUBAI, AONGEZA KASI YA DIPLOMASIA YA KIUCHUMI NA UWEKEZAJI


Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameanza rasmi ziara ya kikazi nchini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akilenga kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja nchini Tanzania.

Katika ratiba ya leo, Rais Samia anafanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Mheshimiwa Gaston Browne, Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi rafiki. 

Aidha, Rais Samia anakutana na Bi. Shaikha Al Nuwais, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), kwa mazungumzo ya pande mbili yanayolenga kuendeleza sekta ya utalii kama nguzo muhimu ya uchumi na kichocheo cha uwekezaji.

Jioni ya leo, Rais Samia anatarajiwa kushiriki uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa mahsusi la uwekezaji linalolenga kuoanisha miradi iliyo tayari kuwekezeka barani Afrika na wawekezaji wa kimataifa. Ushiriki wa Tanzania katika GAIS unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kugeuza fursa kuwa matokeo halisi ya kiuchumi.

GAIS ni mpango wa kimkakati unaoendeshwa sambamba na majadiliano ya sera ya World Governments Summit (WGS), ukiwa na lengo la kubadili mijadala ya sera kuwa uwekezaji wenye tija, unaochochea ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo endelevu barani Afrika.

Wananchi wanaendelea kushauriwa kufuatilia taarifa zaidi kupitia akaunti rasmi za Ikulu Mawasiliano, kwa maendeleo ya ziara hii muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa Taifa.

KATAMBI AKUTANA NA BALOZI WA UINGEREZA



Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi amekutana na Balozi wa Uingereza nchini,Marianne Young ambae aliambatana na Mkuu wa Usalama na Sheria,Alex Beck pamoja na Mkuu wa Ofisi ya Dodoma,Godfrida Magubo.

Katika kikao hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa chini ya mwamvuli wa kusimamia na kuhakikisha Amani,Utii wa Sheria,Usalama wa Raia na Mali.

Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya wizara,Mtumba jijini Dodoma.

DKT. KIJAJI: LENGO LA RAIS SAMIA NI WATANZANIA WANUFAIKE NA RASILIMALI ZAO.







Na Sixmund Begashe, Dodoma 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zao hivyo Wizara anayoiongoza itaendelea kushirikiana na wadau katika usimamizi wa urithi wa Maliasili na Utalii ili kufikia lengo hilo.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo jijini Dodoma kwenye kikao chake na wadau wa Uwindaji Wenyeji na Bucha za Nyamapori kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja wa sekta hizo muhimu kwa uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Amebainisha kuwa, Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo bega kwa bega na wadau wa sekta binafsi hivyo uongozi wa Wizara hiyo hautakuwa na muhali kwa mtumishi yeyote atakaye kwamisha juhudi hizo za kuendelea kuwaletea watanzania tabasamu kwa kuwainua kiuchumi kupitia sekta ya Maliasili na Utalii. 

Pamoja na kuwapongeza wadau hao kwa uzalendo wao, amewataka kuendelea kushikamana na Wizara hiyo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika  uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja ili kufungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira  hususani kwa vijana. 

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasi na Utalii anaeshughulika na Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amewahakikishia wadau hao kuwa, ofisi yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Dkt. Kijaji ambayo yametokana na maono mbalimbali waliyotoa.

Monday, February 02, 2026

RAIS SAMIA AONDOKA DAR AWASILI DUBAI KUSHIRIKI MKUTANO WA DUNIA WA SERIKALI NA JUHUDI ZA UWEKEZAJI AFRIKA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiondoka nchini kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) leo tarehe 02 Februari, 2026, ambapo atashiriki kwenye mkutano wa World Government Summit (WGS 2026) na uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS).

Ushiriki wa Tanzania katika WGS 2026 unaakisi utekelezaji wa DIRA 2050 na Sera Mpya ya Mambo ya Nje, zinazoweka diplomasia ya kiuchumi kama nguzo ya mahusiano ya kimataifa.

Lengo ni kuoanisha sera, ushirikiano na mitaji ya uwekezaji kwa maendeleo ya taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum (DWC) Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), tarehe 02 Februari, 2026. 

Rais Mhe. Dkt. Samia atashiriki kwenye Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Governments Summit – WGS) 2026pamoja na kushiriki Jukwaa la Kimataifa wa Uwekezaji Afrika (GAIS).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Waziri wa Sheria wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Abdullah bin Sultan bin Awad al Nuaimi mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum (DWC) Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), tarehe 2 Februari, 2026. 

Rais Mhe. Dkt. Samia atashiriki kwenye Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Governments Summit – WGS) 2026 pamoja na kushiriki Jukwaa la Kimataifa wa Uwekezaji Afrika (GAIS).

MAKAMU WA RAIS AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI








Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma.

 Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama, na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwa Kata zote nchini zisizo na  Mahakama za Mwanzo.

Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwamba, uhuru wa Mahakama usitumike kama sehemu ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki. Amesema uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.

Makamu wa Rais amesema Mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.

Ameongeza kwamba Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa Kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba, Kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki, Kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi, Kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na Kudumisha amani na mshikamano wa Kitaifa, ambao ni msingi wa maendeleo endelevu.

Pia amesema ni muhimu Mahakama, Kuzuia migogoro inayoweza kuwa chanzo cha migawanyiko ya kijamii au kisiasa, Kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na thabiti, Kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi za umma, Kuchangia katika mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na Kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi mbalimbali kuheshimu tume iliyoundwa na Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuacha kuongelea masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria. 

 Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo kufuatia maombi ya Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Mwabukusi ambaye aliomba Viongozi kuacha kuzungumzia suala hilo ambalo limekuwa likiwaumiza wananchi.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju amesema Mahakama inaendeleza na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Mahakama ili kuimarisha ufanisi. Amesema kwa sasa Mahakama inajenga mfumo unaotumia Akili Unde (AI) kwaajili ya kurekodi mwenendo wa kumbukumbu za mashauri na hukumu Mahakamani.

Amesema katika mfumo huo, Jaji, Hakimu, Wakili na Shahidi wanapozungumza mahakamani mfumo huo utatafsiri lugha iliyotumika na kuiandika kwa lugha iliyokuwa imechaguliwa kuandika kwa wakati huo huo.

 Ameongeza kwamba mfumo huo utakapoanza kutumika utaimarisha ufanisi wa utendaji wa Mahakama kwani kuchukua kumbukumbu za mwenendo wa mashauri Mahakamani kwa kuandika kwa mkono au kompyuta kunachelewesha na wakati mwingine kupotosha.

 


Sunday, February 01, 2026

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

 


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani katika jamii, huku akitahadharisha dhidi ya wanaoingilia masuala ya imani, hatua ambayo inaweza kuhatarisha mshikamano wa Taifa.

Akizungumza leo jumapili Februari 01, 2026 katika ibada ya Kanisa Kuu la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha Mjini, iliyokuwa ikiongozwa na Baba Askofu Dkt. Godson Abel Mollel, Waziri Mkuu alisema mmomonyoko wa maadili unaoanza na kejeli mitandaoni, dharau kwa wazee na viongozi pamoja na kukosa staha kwa mamlaka, unaweza kuathiri misingi ya Taifa endapo hautadhibitiwa mapema kupitia malezi thabiti.





Waziri Mkuu pia alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini, ikiwemo kurekebisha sheria ili taasisi za dini zisichukuliwe kama taasisi za kibiashara, kuweka mifumo ya misamaha ya kodi, na kutatua changamoto za akaunti zilizokuwa zimefungwa kutokana na masuala ya kikodi.

Katika Ibada hiyo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alisema kuwa Rais Samia ametoa kiasi cha shilingi milioni 50 ili kuunga mkono juhudi za Ujenzi wa Kanisa Kuu la KKKT Arusha ambalo ujenzi wake ulianza Januari 2021.

Kanisa hilo jipya litakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 1,000, parking ya magari 200, ofisi, madarasa, chumba cha kunyonyeshea watoto, Chumba cha Mawasiliano na Teknolojia, na madhabahu inayoning’inia.

Waziri Mkuu aliwataka Watanzania kuendelea kujenga Taifa lenye heshima, maadili na mshikamano, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila misingi imara ya malezi na utu.

Awali, Baba Askofu Dkt. Godson Abel Mollel alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti wa Taifa na aliwahimiza waumini, hususan vijana, kutulia, kuepuka vurugu, na kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake.

DKT. MSEMWA: UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 KUANZA JULAI 1, 2026

 





Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaanza rasmi Julai 1, 2026 ukiwa na lengo la kuhakikisha ustawi wa kila Mtanzania bila kujali hali yake.

Aidha amebainisha kuwa dira hiyo inalenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na ushiriki wa wananchi wote katika maendeleo ya Taifa huku ikisisitiza kutomuacha nyuma Mtanzania yeyote.

Dkt. Msemwa ameyabainisha hayo Februari 01, 2026 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050.

Amesema kuwa Dira 2050 ilizinduliwa Julai 17, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na baadaye Serikali kuielekeza NPC kuandaa mipango ya utekelezaji wake ikiwemo Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Miaka 25 (2026/2027–2050/2051), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031) pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027.

Aidha amebainisha kuwa mipango hiyo imepitia mashauriano ya kitaalamu na inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni Februari 2, 2026 kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Amesema kuwa NPC imezingatia uzoefu wa utekelezaji wa Dira ya 2025 na ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi ya Taifa (NPMIS) utakaotumika kufuatilia utekelezaji wa Dira 2050 kuanzia Julai 2026 huku wananchi na wadau wakihimizwa kufuatilia mchakato huo kwa karibu.

MKUTANO WA CATA UANGAZIE MIJADALA YA KUHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UKUSANYAJI MAPATO - MAKAMO WA RAIS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia ni chachu kati...