Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Katibu Mkuu wa Mabaraza ya Habari Duniani, Bw. Ernest Sungura akizungumza na Wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo ambao wameonesha namna urafiki ulioanzia shuleni unavyoweza kubadilishwa kuwa nguvu ya kiuchumi, baada ya kuanzisha kikundi cha TUJIJENGE AMSHA Investment Group, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahitimu wa Milambo (AMSHA), Dereck Murusuri.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahitimu wa Milambo (AMSHA), Dereck Murusuri akizungumza na Wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo ambao wameonesha namna urafiki ulioanzia shuleni unavyoweza.
Wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo ambao wameonesha namna urafiki ulioanzia shuleni unavyoweza.
Dodoma, Oktoba 25, 2026. Wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo wameonesha namna urafiki ulioanzia shuleni unavyoweza kubadilishwa kuwa nguvu ya kiuchumi, baada ya kuanzisha kikundi cha TUJIJENGE AMSHA Investment Group na kuweka mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kufikia thamani ya shilingi trilioni 6.6 kupitia uwekezaji.
Kikundi hicho, kilichoanzishwa na baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Wahitimu wa Milambo (AMSHA), kinalenga kuunganisha mitaji, maarifa na uzoefu wa wahitimu ili kujenga uchumi wa pamoja, kuboresha maisha ya wanachama na kusaidia maendeleo ya jamii, ikiwemo shule waliyosoma.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TUJIJENGE AMSHA Investment Group uliofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Bw. Dereck Murusuri, amesema wameamua kutumia mshikamano wa wahitimu kama msingi wa kuanzisha taasisi ya uwekezaji itakayozalisha faida na kujenga uwezo wa kiuchumi kwa muda mrefu.
Murusuri amesema wazo la kuanzisha kikundi hicho lilitokana na kutambua kuwa wahitimu wa Milambo wana rasilimali muhimu mbili, ambazo ni uwezo wa kuchangisha mitaji na maarifa ya kitaalamu yanayoweza kutumika kuanzisha na kusimamia uwekezaji wenye tija.
"Tuliona umuhimu wa kuanzisha mkono wa uwekezaji ndani ya jumuiya yetu ya wahitimu. Lengo ni kukusanya fedha, kuziwekeza na kutumia faida itakayopatikana kuboresha maisha yetu, kusaidia jamii na kuchangia maendeleo ya shule yetu ya Milambo," amesema Murusuri.
SUNGURA APONGEZA WAHITIMU WA MILAMBO KUGEUKIA UWEKEZAJI, WAJA NA MKAKATI WA SH TRILIONI 6.6
TUJIJENGE AMSHA Investment Group yakusanya karibu Sh milioni 60 bila wanachama kukutana ana kwa ana; Sungura asema ni mfano wa kuigwa na jumuiya nyingine za wahitimu nchini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Katibu Mkuu wa Mabaraza ya Habari Duniani, Bw. Ernest Sungura, amewapongeza wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo kwa kubadilisha mfumo wa kawaida wa jumuiya za wahitimu wa kuchanga na kugawana fedha na badala yake kuunganisha nguvu zao katika uwekezaji wenye manufaa ya muda mrefu.
Sungura ametoa pongezi hizo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TUJIJENGE AMSHA Investment Group uliofanyika jijini Dodoma, ambapo wahitimu hao wameweka mkakati wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2026 hadi 2031, wenye lengo la kufikia thamani ya shilingi trilioni 6.6 kupitia uwekezaji.
Amesema hatua hiyo inaonesha mabadiliko muhimu ya fikra miongoni mwa wahitimu, kutoka kutumia jumuiya zao kwa mikusanyiko ya kijamii pekee na kuwa vyombo vya kujenga uchumi, kuimarisha maisha ya wanachama na kusaidia maendeleo ya jamii.
Akisisitiza umuhimu wa kuwa na maono ya muda mrefu katika uwekezaji, Sungura ametumia mfano wa mbegu kueleza namna mtaji mdogo unavyoweza kuwa chanzo cha utajiri mkubwa endapo utasimamiwa kwa nidhamu na uvumilivu.
"Mtu wa kawaida huhesabu mbegu kwenye tunda, lakini mwenye fikra pevu huhesabu matunda ndani ya mbegu," amesema Sungura, akiwahimiza wanachama kutazama zaidi fursa za baadaye badala ya faida za muda mfupi.
Amesema uamuzi wa wahitimu hao kuwekeza fedha zao, ikiwemo kupitia UTT AMIS, ni hatua inayostahili kuigwa kwa kuwa unaweka msingi wa kukuza mitaji badala ya kutumia fedha zote zinazochangwa na wanachama.
"Fedha mnayojinyima leo ndiyo utajiri wenu wa kesho," amesema Sungura, akisisitiza umuhimu wa nidhamu ya fedha, uvumilivu na kuendelea kuwekeza kwa malengo ya muda mrefu.
WAKUSANYA KARIBU SH MILIONI 60 BILA KUKUTANA
Katika hatua inayoonesha nguvu ya mshikamano na matumizi ya teknolojia, Murusuri amesema kikundi hicho kimefanikiwa kukusanya na kuwekeza fedha zinazokaribia shilingi milioni 60 kupitia mawasiliano ya mitandao ya kijamii, bila wanachama wake kukutana ana kwa ana.
Amesema mafanikio hayo ni ushahidi kuwa kuaminiana, kuwa na malengo ya pamoja na kujitoa kunaweza kuwa msingi wa kujenga taasisi imara ya kiuchumi hata kwa watu wanaoishi katika maeneo tofauti.
"Uwekezaji wote tulioufanya mpaka sasa, unaokaribia shilingi milioni 60, umefanyika kupitia mitandao ya kijamii bila kukutana. Lakini baada ya kukutana ana kwa ana, hamasa imeongezeka sana. Baadhi ya wanachama wamechangia fedha zaidi kutokana na kufurahishwa na hatua tuliyofikia," amesema.
Ameeleza kuwa mkutano huo umekuwa wa kipekee kwa sababu umewakutanisha wahitimu ambao baadhi yao hawakuwa wameonana kwa zaidi ya miaka 30 tangu walipomaliza masomo.
Kwa mujibu wa Murusuri, mkusanyiko wa wanachama ulioanza kwa hafla ya kukutana tena (reunion) umeongeza ari ya kushiriki katika uwekezaji na kuimarisha mahusiano ya wanachama.
MKAKATI WA MIAKA MITANO WENYE MALENGO MAKUBWA
Akizungumzia mwelekeo wa kikundi hicho, Murusuri amesema wameandaa mpango mkakati wa uwekezaji wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2026 hadi 2031, unaolenga kujenga taasisi yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha mapato na faida.
Amesema mpango huo umeweka lengo la kufikia thamani ya shilingi trilioni 6.6, huku wanachama wakitarajiwa kutumia taaluma na uzoefu wao kutambua na kusimamia fursa mbalimbali za uwekezaji.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa kikundi hicho kinajumuisha wataalamu kutoka kada mbalimbali, wakiwemo wachumi, wanasheria, waandishi wa habari, waandishi wa vitabu na wanasayansi.
"Tuna wataalamu wa kada mbalimbali. Tunapokutana, kila mmoja analeta maarifa na uzoefu wake, kisha tunaunganisha nguvu hizo kutengeneza mikakati ya uwekezaji. Tunaamini kupitia umoja huu tunaweza kufikia malengo makubwa tuliyojiwekea," amesema Murusuri.
MKUTANO MKUU WA KWANZA WAWEKA MSINGI WA TAASISI
Murusuri amesema TUJIJENGE AMSHA Investment Group ilianzishwa Desemba 21, 2024, na kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2025, hivyo Mkutano Mkuu wa Kwanza ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha uendeshaji wa kikundi hicho.
Amesema mkutano huo umejikita katika mambo makuu matatu ambayo ni kupitia katiba ya kikundi ili iendane na malengo yake, kujadili mpango mkakati wa uwekezaji wa miaka mitano na kutathmini mwenendo wa kifedha tangu kuanzishwa kwake.
Ameongeza kuwa mkutano huo pia umetoa nafasi kwa wanachama kujenga uelewano, kuimarisha mshikamano na kujadili kwa pamoja mustakabali wa taasisi yao.
"Kwetu huu ni mkutano wa kihistoria. Ni hatua kubwa ya maendeleo ya kitaasisi kwa sababu tunajenga misingi ya kuendesha kikundi chetu kwa utaratibu, uwazi na malengo ya muda mrefu," amesema.
FAIDA ZA UWEKEZAJI KUSAIDIA WANACHAMA, SHULE NA JAMII
Katika hatua nyingine, Murusuri amesema dhamira ya kikundi hicho haijaishia katika kutengeneza faida kwa wanachama pekee, bali pia kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazoweza kutoa ajira na kusaidia maendeleo ya jamii.
Amesema wahitimu wa Milambo wamekuwa wakichangia maendeleo ya shule yao kupitia jumuiya ya AMSHA, na kuanzishwa kwa kikundi cha uwekezaji kutasaidia kuongeza uwezo wa kutoa mchango huo kwa njia endelevu.
Amefafanua kuwa wanatarajia kujenga taasisi itakayoweza kujitegemea kiuchumi na kuwa mfano kwa jumuiya nyingine za wahitimu nchini kuhusu umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwekeza.
URAFIKI WA SHULENI WAGEUKA MTAJI WA MAENDELEO
Mwenyekiti huyo amesema moja ya mambo yanayowapa nguvu ni historia ya pamoja ya wahitimu wa Milambo, ambao licha ya kutawanyika katika maeneo mbalimbali na kufanya kazi tofauti, wameendelea kudumisha mshikamano.
Katika kusisitiza utambulisho wa shule hiyo, Murusuri amebainisha kuwa wahitimu wake wanajitambulisha kama "Milambo Men", akieleza kuwa huo ndio utambulisho wao wa kihistoria.
Kwa wahitimu hao, mkutano wa Dodoma haukuwa wa kukumbushana maisha ya shule pekee, bali pia wa kuweka msingi wa kujenga uchumi wa pamoja unaoweza kuwanufaisha wao, familia zao na jamii kwa ujumla.
Kutoka kwenye madarasa ya Milambo hadi kwenye ulimwengu wa uwekezaji, TUJIJENGE AMSHA Investment Group imeanza safari ya kuonesha kuwa urafiki wa shule unaweza kuwa zaidi ya kumbukumbu, na badala yake kuwa mtaji wa kujenga uchumi wa sasa na vizazi vijavyo.












No comments:
Post a Comment