π Amshukuru Rais Samia kwa uwekezaji wa bilioni 3.2 Makuyuni
✍️ Na Beatus Maganja, Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kukamilisha kwa wakati miradi ya kimkakati yenye thamani ya Shilingi billioni 1.7 inayotekelezwa Makuyuni Wildlife Park kupitia Tozo za Maendeleo ya Utalii (TDL), ili kuboresha huduma na kutumia fursa za AFCON 2027.
Akikagua miradi hiyo Oktoba 25, 2026 mkoani Arusha, Dkt. Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa Sh bilioni 3.2 katika kipindi cha miaka mitatu kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo.
“Tunamshukuru sana Rais wetu kwa kuendelea kuimarisha sekta ya utalii . Katika kipindi cha miaka mitatu tangu tukabidhiwe eneo hili, tumepatiwa shillingi billioni 3.2 ambazo tunaendelea kuwekeza katika kuiboresha miundombinu ya Makuyuni Wildlife Park" amesema Dkt. Kijaji.
Sambamba na hilo, amesema ujenzi wa geti la kisasa na ufunguzi wa barabara umefikia asilimia 90, akielekeza maeneo yote ya hifadhi yaunganishwe kwa barabara ifikapo Aprili 2027. “Fedha zipo, hivyo hatuna sababu ya kuchelewa,” amesisitiza.
Aidha, amewakaribisha Watanzania kufurahia vivutio vya Makuyuni na eneo la kupiga kambi linaloandaliwa, akieleza kuwa hifadhi hiyo ni lango muhimu la kutembelea vivutio vingine vya ukanda wa kaskazini.
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, amesema Mamlaka itatekeleza maelekezo hayo kwa kukamilisha miradi kwa wakati na kuzingatia ubora huku akimshukuru Rais Samia kwa fedha za kuimarisha huduma za utalii.
Awali, Kamanda wa Hifadhi hiyo, Andrew Kishe amesema kutokana na uboreshaji wa miundombinu ambao umekuwa ukifanywa na Serikalli, hifadhi hiyo imekuwa ikirekodi ongezeko la idadi ya watalii kutoka 292 mwaka 2023/24 hadi 3,844 mwaka 2025/26, huku mapato yakipanda kutoka Sh milioni 14.5 hadi Sh milioni 157.9.
Amesema asilimia 72 ya wageni mwaka 2025/26 walikuwa Watanzania, huku Julai–Septemba 2026 hifadhi ikipokea wageni 1,077 na kukusanya Sh milioni 44. Maboresho hayo yanalenga kuongeza wageni, mapato na fursa za ajira na uwekezaji kwa wananchi.










No comments:
Post a Comment