Wednesday, April 01, 2026

WATENGENEZA MAUDHUI MTANDAONI WATAKIWA KUTENGENEZA MAUDHUI YANAYOLINDA TASWIRA YA NCHI

 

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana iliyopo mkoani Mwanza, Mhe. Amina Makilagi {pichani juu] amewataka Watengeneza Maudhui Mtandaoni kuzingatia maadili, uzalendo pamoja na kulinda taswira ya Tanzania kwenye maudhui wanayoyatengeneza.

Mhe. Amina ametoa rai hiyo Aprili 1, 2026 mkoani hapo wakati akizungumza kwenye Mafunzo kwa Watengenza Maudhui Mtandaoni (Content Creators) awamu ya kwanza yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. 

“Msisitizo kwenu watengeneza maudhui, mafunzo mliyoyapata hapa yasiishie hapa bali yatumieni katika kuboresha kazi zenu ili muweze kuongeza kipato cha familia na Taifa kwa ujumla” alisistiza Mhe. Amina.

Aidha, amewataka washiriki hao kuongeza ujuzi kupitia njia mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, CPA (T) Nyakaho Mahemba amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia wazalisha maudhui mtandaoni kupata elimu ya mkopo, uandishi wa mradi pamoja na namna ya kuzalisha kazi bora zaidi zitakazokidhi soko la ndani na nje pamoja na kuweza kuweka ushindani.

Naye Bw. Andrew Ngonyani (Brother K) aliyeshiriki mafunzo hayo aliishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo ambayo yamewasaidia vijana wengi kuweza kutumia maudhui yao kupata pesa, akiishauri Serikali kuendelea kuweka mazingira bora kwa wasanii kufanya sanaa na kunufaika nayo.

Mafunzo hayo yamekuwa na mada mbalimbali ikiwemo Elimu ya Mtaji, Kubiasharisha Maudhui Mtandaoni, Uaminifu uwajibikaji kwa wafuasi wako pamoja na hatua kwa hatua namna ya kutengeneza akaunti ya biashara na kuingiza kipato.










No comments:

WATENGENEZA MAUDHUI MTANDAONI WATAKIWA KUTENGENEZA MAUDHUI YANAYOLINDA TASWIRA YA NCHI

  Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana iliyopo mkoani Mwanza, Mhe. Amina Makilagi {pichani juu] amewataka Watengeneza Maudhui Mtandaoni kuzingatia ...