Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Tuzo ya Heshima ya “Malkia wa Nishati Safi” ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda afya za jamii pamoja na mazingira.
Tuzo hiyo imetolewa na Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), kupitia Mwenyekiti wake Bi. Havijawa Omary, katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Havijawa alisema kuwa Dkt. Samia amekuwa kinara wa mageuzi katika sekta ya nishati safi nchini, hususan katika kuhimiza matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kupikia, hatua inayolenga kupunguza athari za kiafya na kimazingira zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa.
Alieleza kuwa juhudi hizo zimechangia kuboresha ustawi wa familia nyingi, hasa wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakuu wa moshi unaotokana na nishati chafu.
Kwa upande wake, Rais Samia alipokea tuzo hiyo kwa shukrani, akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayoharakisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi kwa Watanzania wote.
Alibainisha kuwa ajenda ya nishati safi siyo tu ya mazingira, bali pia ni suala la afya ya umma na maendeleo endelevu ya taifa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya lishe, afya, mazingira na nishati, ambapo ilitumika pia kama jukwaa la kuhimiza ushirikiano wa taasisi na jamii katika kuendeleza matumizi ya nishati safi nchini.
Tuzo ya “Malkia wa Nishati Safi” inaendelea kuwa alama ya kutambua viongozi na wadau wanaochochea mabadiliko chanya katika matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu nchini.




.jpeg)


No comments:
Post a Comment