Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamisi Mussa Omar, Mhandisi Munde alisema kuwa sekta ya ununuzi na ugavi ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi bora ya rasilimali za umma. Alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya manunuzi ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na thamani halisi ya fedha kwa manufaa ya wananchi.
Naibu Waziri huyo alieleza kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kumekuwepo na mageuzi muhimu katika sekta ya ununuzi na ugavi, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali, uboreshaji wa sera na sheria za manunuzi, pamoja na ujenzi wa uwezo wa wataalam wa ununuzi na ugavi. Alibainisha kuwa hatua hizo zimechangia kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi na kupunguza mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Mhandisi Munde aliwahimiza wataalam wa ununuzi na ugavi kutumia kongamano hilo kama jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za kitaaluma, huku wakijikita katika kubuni suluhisho zitakazosaidia kuimarisha taaluma hiyo na kuifanya iwe chachu ya maendeleo ya Taifa.
Kongamano hilo limewakutanisha wataalam wa ununuzi na ugavi kutoka taasisi za umma na binafsi, wakandarasi, wasambazaji, wasimamizi wa miradi pamoja na wadau wa maendeleo, likiwa na lengo la kujadili mustakabali wa sekta ya ununuzi na ugavi katika mazingira yanayobadilika kwa kasi ya teknolojia na ushindani wa kiuchumi.
Kupitia vipindi vya majadiliano, warsha na mada mbalimbali za kitaaluma, washiriki wanatarajiwa kujadili masuala ya uwajibikaji, maadili ya kazi, matumizi ya teknolojia, pamoja na mchango wa wataalam wa ununuzi na ugavi katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Serikali na ajenda ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Kwa ujumla, Kongamano la 16 la Mwaka la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi limeelezwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uwezo wa wataalam, kuboresha mifumo ya manunuzi, na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa tija na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.









No comments:
Post a Comment