
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuweka mikakati madhubuti na ya kudumu ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika vyanzo vya maji, hususan Mto Ruvu, unaojitokeza mara kwa mara katika vipindi virefu vya ukosefu wa mvua.
Akizungumza kuhusu hali ya upatikanaji wa majisafi jijini Dar es Salaam, Mhe. Chalamila amesema changamoto ya upungufu wa maji katika Mto Ruvu si jambo jipya, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa watendaji na wataalamu wa sekta ya maji kukaa pamoja na kubuni suluhisho la muda mrefu litakalosaidia kuondokana na athari zinazowakumba wananchi kila inapotokea hali ya ukame.
Amesisitiza kuwa DAWASA inapaswa kubuni na kutekeleza miradi ya maji itakayowezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika hata katika vipindi vya upungufu wa maji, ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam linaloendelea kukua kwa kasi.
“Kwa kuwa changamoto hii inajirudia mara kwa mara, ni wajibu wa DAWASA kuhakikisha inabuni miradi ya kimkakati itakayowezesha upatikanaji wa majisafi kwa kipindi chote cha uhaba wa maji, hususan wakati wa kiangazi,” amesema Mhe. Chalamila.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameitaka DAWASA kuongeza jitihada katika kufufua visima vya maji vilivyopo ili viweze kutoa huduma ipasavyo, hatua itakayosaidia kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo, amesema mamlaka hiyo imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na tayari hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa haki na usawa.
Mhandisi Mwangingo ameongeza kuwa DAWASA inaendelea na jitihada za kutoa maji kwa mgao sawia katika maeneo yote ya jiji, sambamba na kufufua visima vilivyopo kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa majisafi na kupunguza athari za uhaba wa maji kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Bonde la Wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi, amesema changamoto ya upungufu wa maji katika Mto Ruvu imesababishwa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zimeendelea kuathiri vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Ameeleza kuwa hatua kadhaa tayari zimechukuliwa, ikiwemo kusitisha utoaji wa vibali kwa watumiaji wa skimu za umwagiliaji katika kipindi cha kiangazi, kwa lengo la kulinda na kuimarisha wingi wa maji katika vyanzo vya maji, hususan Mto Ruvu.
Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia kupunguza makali ya uhaba wa majisafi na kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kupatikana kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam, huku Serikali ikiendelea kusisitiza suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji.








No comments:
Post a Comment