Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Kombo (Mb.) amefanya kikao kazi na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian pamoja na Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam tarehe 6 Desemba 2025.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kampuni za China ikiwemo miradi ya ujenzi wa barabara, majengo pamoja na viwanja vya michezo na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano kwa siku za mbeleni.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kombo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa ushirikiano wake katika kuimarisha diplomasia ya uchumi na Tanzania kupitia miradi ya maendeleo katika sekta za ujenzi, ikiwemo ujenzi wa Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika mkoa wa Dar es Salaam na ujenzi wa majengo ya Serikali jijini Dodoma.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega ameishukuru China kwa mchango wake katika kutekeleza miradi ya ujenzi nchini, na kusisitiza umuhimu wa kampuni za ujenzi kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati ili kuruhusu utekelezaji wa miradi mipya ijayo, katika muda uliopangwa.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ameipongeza China kwa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa mataifa hayo mawili kupanua wigo wa ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wao na vizazi vijavyo.
Awali, Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian, amepongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuwezesha utoaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, jambo lililochangia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa










No comments:
Post a Comment