Wednesday, September 24, 2025

KAMISHNA KUJI ATOA WITO TANAPA KUWA NA SACCOS MOJA










Na Edmund Salaho - Tanga

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji ambaye pia ni mlezi wa HIFADHI SACCOS LTD ametoa wito kwa watumishi wote wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania kujiunga pamoja na kuanzisha SACCOS moja kwa watumishi wote wa TANAPA itakayoitwa TANAPA SACCOS LTD.

Kamishna Kuji ameyasema hayo leo Septemba 24, 2025 katika Mkutano Mkuu wa mwaka 2025 wa HIFADHI SACCOS unaofanyika Jijini Tanga.

"Ninafahamu kuwa kulikuwa na timu maalum ya uhamasishaji ambayo ilipita katika vituo vyote vya kazi kuhamasisha watumishi kufahamu faida za kuwa na SACCOS moja na kuwaomba watumishi wawe tayari kuunga mkono suala hilo muhimu. Mimi pia katika ziara zangu katika vituo vyote katika Shirika nimewasihi watumishi kukubali wazo la kuwa na SACCOS moja. Katika maeneo yote niliyopita, watumishi wamenihakikishia kuwa wazo hilo ni wazo jema na wapo tayari kuliunga mkono wakati ukifika".

Akitaja faida chache zitakazopatikana kwa kuwa na SACCOS moja, Kamishna Kuji alibainisha kuwa popote kwenye umoja pana nguvu ya mafanikio na hivyo mtaji wa Chama utaongezeka maradufu na kuifanya SACCOS hiyo iaminike na Serikali na taasisi nyingine za kifedha nchini.

Aidha, ameutaka Uongozi wa HIFADHI SACCOS kuendelea na uhamasishaji wa kupata wanachama zaidi ambao wataunda TANAPA SACCOS. Pia. Chama kuendelea kubuni mazao mapya na bora zaidi yatakayowanufaisha mwanachama pamoja na kuwekeza katika teknolojia ili kuwasaidia wanachama kufanya shughuli za kichama kidigitali.

Naye, Mwenyekiti wa Hifadhi SACCOS Philip Mwainyekule aliueleza Mkutano Mkuu wa 2025 kuwa Mchakato wa  kuunda SACCOS moja ya Shirika zima umeendelea vizuri kwa msaada wa Sekretarieti iliyoundwa ambapo uliweza kutembelea Hifadhi zote ili kutoa elimu ya Ushirika kwa watumishi pamoja na kuandikisha wanachama waanzilishi wa TANAPA SACCOS na hadi sasa jumla ya watumishi 665 wameshajiandikisha kuwa wanachama wa  TANAPA SACCOS.

Ushirika wa akiba na mikopo mahali pa kazi ni nyenzo muhimu katika kupata utatuzi wa mahitaji ya kifedha kwa gharama nafuu kwa watumishi ambapo wanaweza kupata rasilimali za kuendesha maisha yao.

Dkt. Samia Akiweka Shada la Maua Kaburini kwa Hayati Mkapa, Lupaso




Mtwara – Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, huko Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara. Tukio hilo limefanyika tarehe 24 Septemba, 2025.

Dkt. Samia aliongozana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, katika tukio lililobeba kumbukumbu ya heshima na kutambua mchango mkubwa wa Hayati Mkapa katika kuijenga Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mazingira ya tukio yaligubikwa na unyenyekevu, ukitoa taswira ya mshikamano wa kitaifa na dhamira ya kuenzi urithi wa viongozi waliolitumikia taifa kwa dhati.

Kwa kuweka shada hilo la maua, Dkt. Samia alionesha kuendeleza desturi ya heshima na kuthamini misingi iliyowekwa na marais waliotangulia katika kudumisha mshikamano wa Watanzania na mustakabali wa taifa.

Tuesday, September 23, 2025

CHEREKO ZATAWALA BANDA LA REA KATIKA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA



Furaha na shangwe (chereko) zimetawala katika Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati wananchi walipofurika kununua majiko ya gesi na majiko banifu yanayouzwa kwa bei ya ruzuku katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Wananchi wengi waliokuwa wakipata huduma hiyo hawakuficha furaha yao, wakieleza kuwa hatua hiyo imewasaidia kupata majiko ya kisasa kwa gharama nafuu, hatua inayochochea mapinduzi ya nishati safi ya kupikia hasa vijijini.

“Kawaida majiko haya ni ghali, lakini kupitia REA tumeyapata kwa bei ya ruzuku. Hii ni neema kwa familia zetu na pia ni msaada mkubwa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni,” alisema mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo.

Katika maonesho hayo, REA imejipambanua kwa kuonyesha mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kulinda mazingira, kupunguza ukataji miti ovyo, na kuboresha afya za wananchi hasa akina mama wanaotumia muda mwingi jikoni.

Maonesho ya mwaka huu yamefunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambaye alisisitiza dhamira ya Serikali kuendeleza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na kuongeza upatikanaji wa nishati safi na nafuu nchini.

REA, kupitia banda lake, limekuwa kivutio kikuu kwa wageni na wananchi waliohudhuria, huku wengi wakihamasika kununua majiko hayo na kujifunza mbinu mpya za matumizi yake.

Maonesho haya yanaendelea kutoa nafasi kwa wananchi na wadau mbalimbali kushuhudia teknolojia zinazobadilisha maisha ya Watanzania, huku REA ikionekana kuibua matumaini mapya ya kupikia kwa usalama, afya na gharama nafuu.

TFS yaendelea kuimarisha uwezo wa wahifadhi kukabiliana na majanga ya moto













Iringa, Septemba 22, 2025 — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuimarisha uwezo wa wahifadhi wake kwa kuendesha mafunzo maalumu ya kudhibiti na kuzuia majanga ya moto katika mashamba ya miti nchini.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika Shamba la Miti Sao Hill mkoani Iringa yamewakutanisha wahifadhi kutoka mashamba 24 ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na TFS. Yanalenga kuongeza ujuzi wa vitendo na nadharia kuhusu mbinu za kisasa za kudhibiti moto, ikiwemo utambuzi wa mapema, udhibiti wa kuenea kwa moto na matumizi ya vifaa maalumu.

Akifungua mafunzo hayo, Mhifadhi Mkuu wa Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, alisema moto wa misitu umeendelea kuwa tishio kubwa linalosababisha hasara, hivyo elimu na mafunzo ya kitaalamu ni nyenzo muhimu katika kulinda rasilimali za taifa.

“Tunahitaji kuimarisha mikakati ya kuzuia na kudhibiti matukio ya moto kabla hayajasababisha madhara makubwa. Mikakati ikitekelezwa ipasavyo, itatupa ufanisi mkubwa katika kulinda rasilimali za taifa letu,” alisema Yoramu.

Aidha, alihimiza wahifadhi kushirikiana na jamii zinazozunguka mashamba ya miti ili kuongeza uelewa wa pamoja, kuimarisha tahadhari na kuchukua hatua za haraka pindi moto unapotokea.

Kwa upande wake, Askari Mwandamizi wa Shamba la Miti Kiwila, Nassib Omary Tekelo, alisema mafunzo hayo yatasaidia wahifadhi kupata mbinu za kitaalamu na kutumia vifaa maalumu vya kudhibiti moto.

“Tunaamini elimu hii itatusaidia kulinda misitu yetu dhidi ya majanga ya moto na pia kuwaelimisha jamii zinazozunguka mashamba yetu,” alisema Tekelo.

Naye Askari Mhifadhi kutoka Shamba la Miti Buhigwe-Kasulu, Maria Lupembe, alibainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kubadilishana ujuzi na uzoefu kati ya wahifadhi kutoka maeneo mbalimbali ili kurahisisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na majanga ya moto.

Mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku tatu yanahusisha nadharia na vitendo, na yanalenga kuongeza mshikamano kati ya wahifadhi na jamii katika kuhakikisha usalama wa mashamba ya miti na uendelevu wa misitu nchini

TEKNOLOJIA INAYOCHENJUA DHAHABU 98%, MKOMBOZI WA UCHIMBAJI MDOGO







📍 Geita

Katika historia ya wachimbaji wadogo, changamoto kubwa imekuwa namna ya kupata dhahabu kwa ufanisi, gharama nafuu na bila kuharibu mazingira. Kwa muda mrefu, mbinu za kiasili zilitumika, lakini nyingi ziliishia kupoteza sehemu kubwa ya dhahabu iliyokuwamo kwenye udongo, huku gharama za uchenjuaji zikibaki kuwa mzigo mkubwa.

Miaka michache iliyopita, wachimbaji wadogo walipoteza matumaini – dhahabu ilibaki ardhini, kemikali ziliharibu mazingira, na kipato hakikuakisi jasho lao. Lakini leo, simulizi mpya ya kiteknolojia imeibuka: mtambo wa uchenjuaji dhahabu kwa teknolojia ya Carbon in Pulp (CIP) unaotengenezwa kwa gharama nafuu na kurahisisha maisha ya wachimbaji wadogo.

Mtambo huo, unaochakata dhahabu kwa ufanisi wa zaidi ya asilimia 98%, ni mkombozi wa kweli. Ukishika udongo wenye dhahabu, matokeo yake ni dhahabu safi huku mabaki yake yakiwa ni udongo usio na madhara makubwa kwa mazingira.

John Ngeda, Mbunifu wa mtambo huo, anasema safari yake ya maarifa ilianzia nchini Zimbabwe, alipojifunza mbinu mbalimbali za uchenjuaji. Aliporudi Tanzania, akaamua kuboresha teknolojia hiyo ili iwe suluhisho kwa wachimbaji wadogo wa nyumbani.

"Niliona jinsi wenzetu wanavyotumia teknolojia rafiki kwa gharama nafuu. Niliporudi, niliamua kuunda kitu chepesi kinachomsaidia mchimbaji mdogo apate matokeo makubwa," anasema Ngeda kwa fahari.

Matokeo ya ubunifu huo yamekuwa makubwa. Tayari zaidi ya mitambo 25 imejengwa katika Kanda ya Ziwa pekee, na teknolojia hiyo sasa imesambaa hadi Mbeya na Mpanda. Wachimbaji wadogo wanashuhudia tofauti – wanapata dhahabu nyingi zaidi, gharama zao zimepungua, na mazingira yanalindwa.

Katika Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini Geita (23 Septemba 2025), mtambo huo wa CIP ulikuwa kivutio kikuu. Wageni na wadau wa madini walishuhudia namna teknolojia hii ilivyobadilisha sura ya uchimbaji mdogo kutoka mfumo wa mazoea hadi mfumo wenye tija na uendelevu.

Hii siyo simulizi ya dhahabu pekee – bali ni simulizi ya ubunifu wa Mtanzania, ni simulizi ya ushindi wa teknolojia rafiki kwa mazingira na ushindi wa kijamii na kiuchumi.

Dhahabu si ndoto, wala si mali ya ushirikina. Ni urithi halisi unaoweza kuendeleza maisha ya maelfu ya Watanzania, pale inapochimbwa na kuchakatwa kwa njia sahihi.

Kwa hakika, dhahabu haipo tu ardhini – ipo pia katika akili za wabunifu wanaothubutu.

Maabara ya Tume ya Madini Kuimarisha Sekta ya Madini Tanzania 🔬

 







Dar es Salaam: Maabara ya Tume ya Madini imejipambanua kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha sekta ya madini nchini Tanzania. Iko katika TIRDO Complex, Msasani, Dar es Salaam, maabara hii inatoa huduma za uchambuzi wa madini na ushauri wa kitaalamu kwa wachimbaji, wawekezaji, na watoa huduma mbalimbali wa madini, kuhakikisha kila sampuli inathibitishwa na kuthibitisha thamani halisi ya madini.

Chini ya uongozi wa Mhandisi Mvunilwa Mwarabu, timu ya wataalamu wa geokemia, mineralogi, na metallurgi hufanya kazi kwa viwango vya ISO 17025, kuhakikisha matokeo sahihi, haraka, na yanayokubalika kimataifa. Maabara hii inatumia teknolojia za kisasa, ikiwa ni pamoja na X-Ray Fluorescence (XRF), fire assay, na mbinu nyingine za kisayansi, kuhakikisha madini yote yanapimwa kwa usahihi mkubwa.

Maabara ya Tume ya Madini hutoa huduma mbalimbali zikiwemo uchambuzi wa XRF kwa madini ya chuma, zinki, shaba, nickel, tin, na madini mengine, fire assay kwa dhahabu na fedha, uchambuzi wa metali za msingi kwa kutumia Acid Digestion + AAS, ukaguzi wa almasi na dhahabu za mapambo, uchambuzi wa graphite na utambuzi wa madini mengine, maandalizi na ukavu wa sampuli, pamoja na vipimo vya unyevu na kupoteza uzito kwa moto.

Matokeo sahihi ni msingi wa uamuzi wa kibiashara kwa wachimbaji na wawekezaji. Maabara ya Tume ya Madini inahakikisha madini yanauzwa na kununuliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, kuongeza uwazi na kuimarisha thamani ya madini nchini. Hii inasaidia pia kuongeza uwekezaji na kuendeleza sekta ya madini kwa ufanisi.

Kwa maneno mengine, Maabara ya Tume ya Madini siyo tu mahali pa uchambuzi, bali ni kiini cha maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania, ikihakikisha madini yanathibitishwa, kupimwa, na kuthaminiwa kwa uwazi na ufanisi.


MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA KAMATI YA KITUO CHA KUDHIBITI MAGONJWA AFRIKA (CDC)










New York, Marekani –
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha uthabiti wa Afrika katika kukabiliana na dharura za afya ya umma.

Akizungumza katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Dkt. Mpango alisema Tanzania imejipanga kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kutumia mbinu bunifu za ufadhili na kuunga mkono mipango ya kikanda inayolenga kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.

Makamu wa Rais alibainisha kuwa uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu na bidhaa nyingine muhimu za afya ni hatua ya lazima ili kuimarisha kujitegemea kwa Bara la Afrika. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye viwanda vya ndani, kuanzisha mamlaka za pamoja za udhibiti barani na kushirikiana katika uhawilishaji wa teknolojia kwa lengo la kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.

Aidha, Dkt. Mpango alikumbusha masomo yaliyopatikana kutokana na milipuko ya hivi karibuni ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Marburg, akisisitiza haja ya kuimarisha maandalizi na mifumo ya dharura ya kiafya. Alisema Tanzania inaendelea kuimarisha vitengo vya matibabu, kuandaa timu za dharura zinazoweza kupelekwa kwa haraka na kuwekeza katika miundombinu ya afya pamoja na rasilimali watu.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma ikiwemo ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, vifaa, udhibiti wa maambukizi na uratibu wa haraka katika kukabiliana na milipuko.

Makamu wa Rais pia alitoa wito wa mshikamano mkubwa kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda na Africa CDC kwa kuunda mbinu ya pamoja ya utafiti, sera na mipango ya kujenga uwezo, ili kuboresha uwezo wa pamoja wa kuzuia, kugundua na kushughulikia milipuko.

Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo: “Kuhakikisha Uhuru wa Afya Afrika: Uongozi wa Kisiasa kwa Ufadhili Endelevu wa Sekta ya Afya, Uzalishaji wa Ndani na Maandalizi Dhidi ya Milipuko ya Maradhi.”

Mazungumzo na Rais wa Ureno

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ureno, Mhe. Marcelo Rebelo de Sousa, pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Ureno katika sekta mbalimbali za maendeleo.

KAMISHNA KUJI ATOA WITO TANAPA KUWA NA SACCOS MOJA

Na Edmund Salaho - Tanga Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji ambaye pia ni mlezi wa HIFADHI SACCOS LTD ametoa wito kwa watumi...