Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Serikali
imeongeza ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni
pamoja na shughuli zote za mnyororo mzima wa thamani wa madini nchini
ambapo kwa Mkoa wa Geita pekee wachimbaji wadogo wamezalisha kilo
22,014.61 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.443 na Serikali kukusanya
mapato ya shilingi bilioni 2.5 katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi
2024/2025.
Mchango wa
wachimbaji wadogo wa madini umeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2020
hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2024 katika mapato yote ya sekta ya
madini na mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka
kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2024.
Akizungumza
Septemba 28, 2025 katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan
Bombambili mkoani Geita wakati akifunga Maonesho ya Nane ya Teknolojia
na Uwekezaji katika Sekta ya Madini, yenye kauli mbiu “Ukuaji wa Sekta
ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi
Bora/Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025”. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza wachimbaji wadogo na Wizara
ya Madini kwa hatua hiyo.
“
Napenda kutoa pongezi maalum kwa Wizara ya Madini kwa usimamizi mzuri
wa sekta hii pamoja na wachimbaji wadogo wa Tanzania. Ninyi ni sababu ya
kusheherekea mafanikio haya mmekuwa shamba darasa na baada ya Serikali
kuwapatia nafasi mmeonesha kwa vitu mlivyofanya mkipewa fursa mnaweza,”
Amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea
“Mmepambana sana kuleta teknolojia ndani ya nchi na mmeonesha
Watanzania wanaweza kufanya mambo makubwa na wakafanikiwa,”
Aidha,
amesema kuwa tangu kuanza kwa maonesho hayo mwaka 2018 kumekuwepo na
mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yanayochangia kuongezeka kwa kasi ya
uzalishaji madini hasa kwa wachimbaji madini wadogo. Ambapo katika
uchenjuaji madini, zimekuwepo teknolojia mbalimbali za kisasa zikiwemo
Carbon – In – Leach (CIL), Carbon – In – Pulp (CIP) na Froth Floatation
(FF) ambazo zimekuwa na tija zaidi kuliko matumizi ya zebaki ambayo
imekuwa na athari nyingi za kiafya na mazingira sambamba na kiwango
kidogo cha uzalishaji.
Dkt.
Biteko amesema kufuatia usimamizi thabiti na mabadiliko makubwa ya
teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uwepo wa maonesho
hayo ya teknolojia, Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa
kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 3.8 kwa kipindi cha miaka minne
kuanzia mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025.
Akizungumzia
hatua mbalimballi za Serikali katika kuhamasisha uongezaji thamani
madini, Dkt. Biteko amesema kumekuwepo na uanzishwaji wa viwanda vya
uyeyushaji na usafishaji wa madini ya dhahabu, nikeli na shaba katika
maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa sasa kuna jumla ya viwanda nane vya
uchenjuaji wa shaba na nickel katika Mkoa wa Dodoma, Kiwanda kimoja cha
Uyeyushaji wa Shaba (Chunya) na Viwanda Sita vya Usafishaji wa Dhahabu
katika Mikoa ya Geita, Mwanza na Shinyanga-Kahama.
“
Nitoe wito kwa wachimbaji na Wizara kuendelea kubuni na kuongeza
uwezeshwaji wa Watanzania kuongeza thamani ya madini wanayozalisha.
Mazingira haya yataongeza upatikanaji wa fedha za kigeni pamoja na
kuwapatia watanzania ajira kwenye viwanda vya uongezaji thamani, STAMICO
mmefanya kazi kubwa sana kubadilisha na kushiriki kwenye local
content.” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Amewahakikishia
kuwa Serikali sikivu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuweka mazingira
wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya madini ikiwemo kufikisha
huduma ya umeme katika maeneo yote muhimu.
Fauka
ya hayo, Dkt. Biteko amewaasa washiriki wa maonesho hayo kushiriki
kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuwa hatua hiyo ni
muhimu katika nchi ya kidemokrasia.
Naye,
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amemshukuru Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ambapo mwaka jana aliagiza
uwanja huo wa maonesho ujengewe miundombinu ya kudumu.
Amesema agizo hilo limetekelezwa na sasa uwanja huo una mabanda tisa ya kudumu ikiwa ni awamu ya kwanza ya ujenzi.
Amesema
maonesho hayo kwa mwaka huu yamehudhuriwa na washiriki 930 wakiwemo
washiriki kutoka nje ya nchi ikilinganishwa na washiriki 600 mwaka 2024.
Amesema
“Rais Samia amewezesha kutoa leseni 9,000 kwa wachimbaji wadogo
wakiwemo wa Pori la Kigosi na sasa tumeweza kuzalisha zaidi ya tani
22,000 za madini kwa wachimbaji wadogo,”
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Mhandisi Zena Said amewashauri wadau wa sekta ya madini kwa ujumla
kutumia fursa za taasisi za fedha ili kupata elimu kuhusu masuala ya
fedha na uwekezaji.
Akimwakilisha
Waziri wa Madini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo
amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuwa chachu
hususan kwa wachimbaji wadogo na kuwaongezea elimu kuhusu uchimbaji
hatarishi na matumizi ya zebaki.
Vilevile
amesema Wizara ya Madini itahakikisha inasimamia sheria na taratibu
zote ili kufanya sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi
wa nchi.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo amesema kuwa hivi sasa sekta ya
madini nchini imefikia kiwango cha kushawishi viwanda vya kuzalisha
vipuri kuja kuwekeza Tanzania ili vipuri hivyo vipatikane nchini na
kufikia lengo la kuwa na Tanzania ya viwanda.
Amebainisha kuwa Tume ya Madini itaendelea kuwezesha sekta ya madini ili kuhakikisha madini yanawanufaisha Watanzania wote.
Mwenyekiti
wa Wachimbaji Wadogo, Lenard Bugomola amesema kuwa Mkoa wa Geita
umekuwa ukiongoza kwa uzalishaji wa dhahabu, aidha ameomba STAMICO
iwapatie mitambo miwili ya uchimbaji madini.
Awali
Dkt. Biteko alitembelea mabanda ya mbalimbali yakiwemo Taasisi ya
Jiolojia na Utafiti wa Madini, Anglo Gold Ashanti, Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO), Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA),
Mwamba Mining ambapo alielezwa kuhusu teknolojia ya kisasa ya uchimbaji
madini