NMB watoa msaada wa vifaa tiba hospitali ya Jeshi Arusha

 Na PamelaMollel,Arusha


Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa tiba kwa hospitali ya Jeshi la wananchi Kanda ya Arusha iliyoko Monduli Mkoani Arusha vyenye thamani ya Sh 3.1 milioni.

Vifaa hivyo ni pamoja na stendi za dripu, vitanda pamoja na magodoro kwa ajili ya kusaidia wananchi mbalimbali wanaofika katika hospitali hiyo kupata huduma bora kwa urahisi zaidi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa taasisi hiyo imetenga zaidi ya Sh 5.4 milioni kwa mwaka 2024 kwa ajili ya kuchangia huduma mbalimbali nchini katika sekta ya Elimu, Afya, mazingira na majanga.

“Leo tumekuja kutoa vifaa hivi ajili ya kurahisisha huduma kufanyika katika hospitali hii tukitambua umuhimu wa afya bora kama moja ya kipaumbele chetu kwa maendeleo ya Taifa lolote duniani” amesema Baraka.

Amesema Serikali imekuwa ikifanya kwa nafasi kubwa katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wakati na kwa ukaribu hivyo wao kama wadau wa maendeleo wana jukumu la kusaidia kuhakikisha mazingira na miundo mbinu yote ya afya yanapatikana.

“Leo tunagawa vifaa hivi kama sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi wanaotuunga mkono kwa kufanya kazi na kufungua akauti zao kupitia benki yetu ambapo tumetenga asimilia moja ya faida kuhakikisha inawarudia wananchi katika huduma mbalimbali”

Amesema katika kuzidi kusogeza huduma kwa wateja, wamefanikiwa kufungua matawi zaidi ya 234 na kusambaza mashine zaidi ya 700 lakini pia wana mawakala zaidi ya 44,000 nchi nzima ili kutekeleza kauli ya ‘NMB Karibu yako’”Amesema.

“Pia tumeendelea kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha ikiwemo mikopo ya makundi mbalimbali lakini pia kubuni na kuzindua huduma mbalimbali za kidigitali kusaidia kurahisisha huduma kwa wateja, hivyo tunawakaribisha pia wateja kutoka hapa jeshini kuja kufungua akaunti zenu na kuwa sehemu ya mafanikio haya ya huduma kwa jamii” alisema Baraka.

Akipokea vifaa hivyo, Kamanda wa kikosi, hospitali ya Jeshi Kanda ya Arusha, Luteni Kanali Jichola Jilya Masanja ameshukuru kwa msaada huo kutoka NMB na kusema hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya jeshi na taasisi hiyo ya kifedha.

“Kutupatia vitanda, magodoro, na stendi za dripu zitasaidia watanzania wote wanaohudumiwa hapa kupanua wigo wa huduma na sisi kama wadau tunaahidi kutunza vifaa hivi kwa manufaa ya wengi zaidi na tuaomba mashirikiano yaendelee sio Arusha tu na maeneo mengine wafaidike” amesema Mkuu huyo.





Comments