Wednesday, July 19, 2017

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AZINDUA RIPOTI YA NCHI YA APRM

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya nchi kuhusu Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa afrika kujipima kwa Vigezo vya Utawala (APRM). (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akionyesha kitabu chenye ripoti  ya nchi kuhusu Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa afrika kujipima kwa Vigezo vya Utawala (APRM) mara baada ya kuzindua taarifa hiyo kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amezindua Taarifa ya Nchi kuhusu Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa Afrika kujipima kwa Vigezo vya Utawala (APRM).Uzinduzi huo  ulihudhuriwa na  kiongozi wa Jopo la Mchakato huo kwa Tanzania ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo  la Watu Mashuhuri Bi. Brigitte Sylvia Mabandla, Viongozi wengine wa APRM Tanzania ni Balozi Ombeni Sefue, Profesa Hasa Mlawa na Balozi Aziz Mlima aliyemuwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na baadhi ya Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

APRM ni mpango wa hiari wa kujipima kwa vigezo vya utawala bora uliobuniwa mwaka 2003 na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. Lengo la mpango huu ni kuziwezesha nchi  wanachama kujitathmini kwa vigezo vya utawala bora katika maeneo manne ambayo ni; Demokrasia na Utawala wa Kisiasa; Usimamizi wa Uchumi; Utendaji wa Mashirika ya Biashara; na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.

Akihutubia katika uzinduzi huo, Makamu Rais amewapongeza Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki katika mchakato wa APRM kwa ujasiri wao wa kushirikishana taarifa za kuaminika kuhusu masuala ya utawala bora katika nchi zao. “Taarifa hizi zinaonesha wazi juu ya hali ya utawala bora katika Bara letu na kutupa nafasi ya kujirekebisha pale ambapo kuna dosari na kujipongeza pale tunapofanya vizuri na kuwapa wengine nafasi ya kujifunza zaidi’’ alisema Makamu wa Rais.

Aidha alisisitiza kuwa kupitia utaratibu huu tumeweza kuuonesha ulimwengu nguvu zetu za pamoja kama Bara la Afrika katika kuboresha demokrasia, amani na utulivu, utawala wa sheria na utawala bora kwa ujumla.

Kwa upande wa Tanzania, Makamu wa Rais alisema mchakato huu unatuonesha na kutukumbusha falsafa na maono ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere (Tujisahihishe, 1962) na Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971.  Alisema nchi yetu imefanya mambo mengi katika kutekeleza mpango huo ikiwemo kuimarisha taasisi zinazoshughulikia masuala ya utawala bora ikiwemo Tume ya Haki za binadamu na Utawala Bora, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa na sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma.

Kuhusu changamoto zilizobainishwa kwenye taarifa husika, Makamu wa Rais alisema kwa kiasi kikubwa zimepatiwa ufumbuzi katika Mkakati wetu wa Maendeleo 2025 unaolenga kukuza na kupanua wigo wetu wa uchumi ili kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.  Kuhusu suala la Muungano alisema muundo wa Muungano wetu ni wa serikali mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Rais alisema miongoni mwa maeneo ya vipaumbele katika mchakato wa kuelekea kuwa nchi ya viwanda  ni kuimarisha sekta ya nishati na umeme. “Kwa ujumla tumefanya jitihada kubwa katika huduma ya nishati kutokana  na ugunduzi mkubwa wa gesi asilia hapa nchini” alisisitiza Makamu wa Rais. Kwa sasa umeme unasambazwa kwa kasi katika vijiji vyetu kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuzipatia ufumbuzi changamo za kijamii kama vile elimu, afya na maji ambazo zilitajwa kama vikwazo katika taarifa husika. Aidha, Serikali imeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za msingi na sekondari, imeboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, imejenga madarasa na maabara, imeboresha maslahi ya walimu na kuhakikisha inajenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya.

Pia Makamu wa Rais alisema Tanzania inatambua kuwa mchakato huu wa APRM ni endelevu hivyo serikali itaendelea na jitihada zake kuhakikisha kwamba changamoto zote zilizobainishwa ndani ya taarifa zinapatiwa majawabu kupitia serikali na taasisi zake, asasi binafsi na wananchi kwa ujumla.

Mwisho, alishukuru na kutambua mchango wa washirika wa maendeleo katika kufadhili kazi za APRM na kuwaalika kuendelea kuchangia shughuli za APRMTanzania ikiwemo mpango kazi wa Taifa.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...