Friday, October 08, 2010
Redet: Kikwete aongoza kura za maoni
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amewaacha mbali wapinzani wake kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kupata asilimia 71.2 ya kura za maoni katika utafiti uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (Redet).
Matokeo hayo yamekuja katika kipindi ambacho kuna mzozo mkubwa baina ya taasisi nyingine inayofanya utafiti wa masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ya Synovate na Chadema ambayo inadai kuwa mgombea wake wa urais, Dk Willibrod Slaa aliongoza kwenye kura ya maoni iliyofanywa na taasisi hiyo.
Synovate imekana kufanya utafiti wa aina hiyo na kwamba hadi sasa imefanya utafiti kuhusu mwenendo wa vyombo vya habari katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu, lakini Chadema imesema inao ushahidi kuwa taasisi hiyo iliendesha utafiti ulioonyesha kuwa Dk Slaa alipata asilimia 45 dhidi ya 40 za Kikwete.
Jana, Redet ilitangaza matokeo ya utafiti wake ambayo yanaonyesha kuwa Kikwete bado anaongoza, licha ya umaarufu wake kushuka kwa asilimia chache.
"Tukianzia uchaguzi wa rais wa Serikali ya Muungano, asilimia 71.2 ya wahojiwa wote walisema watamchagua mgombea urais wa CCM. Ilifuatiwa na Chadema ambayo asilima 12.3 walisema watamchagua mgombea wa Chadema na asilimia 10.1walisema watamchagua mgombea wa Cuf," alisema Dk Benson Bana ambaye ni mwenyekiti mwenza wa mpango huo.
Hata hivyo Kikwete anaonekana kupata kura nyingi zaidi kuliko asilimia za kura za wabunge ambazo ni 66.7 zikipungua kwa asilimia 4.5 kwa kulinganishwa na za kura za urais, huku madiwani wakipata asilimia 66.
Kwa mujibu wa Redet, matokeo yangekuwa hivyo iwapo uchaguzi mkuu ungefanyika kati ya Septemba 20 hadi 28 mwaka huu.
Akitoa matokeo ya utafiti huo wa 17 uliofanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Visiwani katika kipindi hicho cha Septemba, Dk Bana alisema jana kuwa waliohojiwa walitakiwa kutoa maoni kuhusu uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Alisema katika utafiti huo wahojiwa waliulizwa: "Mwezi Oktoba mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu.
Kama uchaguzi huo ungefanyika leo, je wewe ungemchagua mgombea wa chama gani?"
Alifafanua kuwa kutokana na swali hilo vyama vitatu vya CCM, CUF, Chadema vilipata alama nyingi kwa wagombea wake wa urais, wabunge na madiwani.
Hata hivyo, Dk Bana alisema kiwango cha asilimia za kura kimepungua kwa mgombea wa CCM kulinganisha na utafiti uliofanywa na Redet mwezi Machi wakati matokeo yalipoonyesha kuwa asilimia 77.2 wangemchagua mgombea urais wa CCM na tofauti na asilimia 71.2 alizopata safari hii.
"Itakumbukwa kwamba matokeo ya utafiti wa Redet wa hapo Machi mwaka 2010 yalionyesha wengi wangemchagua mgombea urais wa CCM asilimia 77.2. Katika utafiti CCM bado inaongoza, hata hivyo kiwango cha asilimia kimepungua," alisema Dk Bana.
Dk Bana alisema utafiti huo wa Redet ulifanywa kwa kuwahoji watu 2,600 katika wilaya 52 na kwamba watu 1,849 ndio waliosema watamchagua mgombea wa CCM, 263 wa CUF na 319 mgombea wa Chadema.
Ikilinganisha na utafiti wake wa mwezi Machi mwaka huu, Redet ilisema kuwa katika kipindi cha miezi sita kilichopita, idadi ya watu ambao wangemchagua mgombea wa Chadema imeongezeka kwa asilimia nane (8) kutoka 4.2 za mwezi Machi hadi 12.3.
Redet ilitaja pia kuongezeka kwa asilimia 0.9 kwa kura za urais wa CUF, asilimia 02 kwa TLP na 0.1 kwa NCCR-Mageuzi huku ikitaja sababu kuwa ni kampeni za uchaguzi zinazoendelea.
Lakini, taasisi hiyo ilisema mgombea urais wa CCM anaongoza kwa kutajwa jina lake kama mtu ambaye wangependa awe rais wa Tanzania na asilimia 68.5 ya wahojiwa wote akifuatiwa na Dk Slaa wa Chadema aliye na asilimia 11.9 huku Profesa Lipumba wa CUF akiwa wa tatu kwa asilimia 9.3 ya wahojiwa.
Dk Slaa
Taasisi hiyo ya utafiti wa kitaalam ilisema kuwa katika kura za urais, CCM itapata kura kidogo zaidi katika Jimbo la Kigoma Vijijini ambako atapata asilimia 28 huku Jimbo la Nkasi akipata asilimia zote 100.
Kwa mujibu wa utafiti huo kwa upande wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano, pia asilimia ya watakaochagua mgombea wa CCM imepungua kwa asilimia 1.3, huku ikiongezeka kwa vyama vya upinzani, vikiongozwa na Chadema ambayo imeongezeka kwa asilimia 2.9, CUF 1.5, TLP na NCCR-Mageuzi asilimia 0.8 kila kimoja.
Kwa mujibu ya Dk Bana asilimia 66.7 ya waliohojiwa walisema watamchagua mgombea wa CCM huku asilimia 11.7 wakitaja mgombea wa CUF na asilimia 11.5 wa Chadema huku vyama vingine vikitajwa na idadi ndogo ya wahojiwa katika nafasi hiyo na ile ya urais.
Utafiti huo unaonyesha kuwa TLP katika urais itapata asilimia 0.4 na ubunge asilimia moja wakati NCCR-Mageuzi ikipata 0.3 urais na 1.1 ubunge na UDP iliambulia sifuri.
Kwa mujibu wa Redet matokeo ya utafiti huo kwa nafasi za udiwani katika vyama hivyo yanakaribia kufanana na nafasi za ubunge na uraisi. habari imeandikwa na Exuper Kachenje na Zulfa Msuya: Source :MWANANCHI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
Adam Malima James Wanyancha Hamis Kagasheki RAIS Jakaya Kikwete ameteua Baraza la Mawaziri, huku likiwa na sura na damu mchanganyiko. Bar...
No comments:
Post a Comment