Tuesday, August 24, 2010

Tendwa aongeza siku 10 fomu za Gharama za Uchaguzi



MSAJILI wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amevitaka vyama vya siasa ambavyo vimeshindwa kupata nakala za fomu ya Gharama za Uchaguzi kuchukua fomu hizo na kuzijaza ndani ya siku kumi, kabla ya kuzikagua na kuweka pingamizi kwa wagombea ambao wameshindwa kuzijaza.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya vyama kikiwemo Chadema, kudai kukosa nakala hiyo ambayo inaweza kuwasababishia wagombea wao kuwekewa pingamizi kwenye Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Tendwa alisema kuwa malalamiko hayo yapo kwenye vyama vingi, jambo ambalo limemfanya aongeze siku kumi kwa ajili ya kuzijaza na kuwasilisha ofisini kwake au ofisi ya mkurugenzi wa Wilaya (DED).

“Nimeongeza siku kumi, kuanzia leo hadi Septemba 6 mwaka huu kwa vyama vya siasa kuchukua fomu hizo na kuzijaza, kwa sababu malalamiko haya hayapo kwa Chadema peke yake bali ni vyama vingi, jambo ambalo limenifanya niongeze siku ya kuzichukua na kuzijaza, hivyo basi wagombea au vyama wanapaswa kuzingatia suala hilo,”alisema Tendwa.

Aliongeza kutokana na hali hiyo vyama vya siasa vinapaswa kuwathibitisha wagombea wake kwenye fomu hizo ili kusiwe na sababu ya kuwekewa pingamizi kwa wagombea walioshindwa kufanya hivyo, jambo ambalo linaweza kuongeza malalamiko mengine kwenye uchaguzi.

Alisema kuwa wagombea ambao wamepita bila ya kupingwa kwenye majimbo yao pia wanapaswa kujaza fomu hizo kwa sababu ya kuthibitisha uhalali wake kwenye vyama na kuzikabidhi kwenye ofisi za DED, ikiwa watashindwa kufanya hivyo wataweza kuwekewa pingamizi na ofisi yake au wagombea wenzake.


Kwa mujibu wa Tendwa, wagombea ambao watashindwa kufanya hivyo wataweza kuwekewa pingamizi la kutokushiriki kwenye uchaguzi mkuu na ofisi yake ikiwa ni pamoja na kufuata utaratibu uliowekwa ndani ya sheria ya gharama ya uchaguzi hivyo basi vyama vya siasa vinapaswa kufuata utaratibu huo.

Alisema, awali fomu hizo alizigawa kwenye mkutano wa mwisho wa kujadili sheria ya gharama za uchaguzi, ambapo baadhi ya vyama vilishindwa kuhudhuria mkutano huo, badala yake wanaamua kulalamikia suala hilo.


“Baadhi ya vyama vya siasa vimezoea malalamiko, ukiwaita kwenye mikutano wanashindwa kuhudhuria badala yake wanaamua kulalamika kana kwamba wameonewa, sasa basi muda niliotoa umetosha, wasipojaza sheria itachukua mkondo wake,”alibainisha.

WAKATI huohuo Mussa Mkama na Lilian Mazula wanaripoti kuwa chama cha NCCR Mageuzi kimesema sheria ya gharama za uchaguzi inapingana na sheria mama ya uchaguzi ya mwaka 1985, kifungu cha (1) sehemu ya 40(ii).
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ofisi ya chama hicho jana jijini Dar es salaam, mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia alisema kitendo hicho ni hatari kwani kinaweza kusababisha machafuko nchini.
“Uzembe wa ofisi moja ya serikali kutunga sheria kwa nia mbaya isiwe chanzo cha Watanzania kuingia katika vurugu, zisizo na sababu ya msingi” alisema Mbatia na kuongeza kuwa
“Sheria mpya ya gharama ya uchaguzi iliyotungwa mwaka jana, kupitishwa mwaka huu na kusainiwa kwa mbwembwe na rais Jakaya Kikwete katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam kusudio siyo kwa maslahi ya Taifa, bali kwa maslahi binafsi”.
Alisema zoezi hilo la kutunga sheria hiyo kwa makusudi ni batili hivyo msajili wa vyama vya siasa John Tendwa awaache TAKUKURU wafanye kazi yake kwa sababu yeye ameshindwa kuandaa mazingira mazuri ya uchaguzi.
“Kutokana na sheria hiyo bado Tendwa anabolonga kazi yake anaonekana ajiamini na kitu anachokifanya, sheria hiyo mama inasema mgombea anatakiwa aweke pingamizi ndani ya masaa 24, lakini yeye anatoa siku saba huko ni kuvunja sheria” alisema Mbatia.
Hata hivyo Mbatia alisema kitendo cha msajili huyo kuvifanya vyama vya siasa kama wakala wa ofisi yake kwa kutaka vyama vyote vitoe kopi ya fomu hizo na kuzisambaza hadi ngazi ya vitongoji, huku ni kazi ya ofisi yake si utaratibu mzuri.
“Msajili kama alitaka vyama viwe wakala wa ofisi yake aseme tuzungumze, lakini siyo atupe fomu original alafu tuzitoe kopi mitaani, huo ni upungufu anatakiwa aombe radhi” alisema Mbatia kwa msisitizo.
Aidha alisema kutokana na mapungufu hayo tayari uchaguzi umeshaharibika asikae na kusema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni huru na wahaki, kwa kuwa na mapungufu mengi katika sheria hiyo ambayo hivi sasa inakwenda hovyo hovyo.
“Serikali iliyoko madarakani pamoja na ofisi yake ya msajili imeshindwa kuandaa mazingira bora ya uchaguzi utakaokuwa huru na haki,ambao kwa mara ya kwanza Watanzani wangejivunia kilicho bora” alisema Mbatia.
Hata hivyo Mbatia aliwataka wagombea wa vyama vyote waliowekewa pingamizi na ofisi ya msajili wasiwe na wasiwasi kwa sababu sheria mbili zinapokinzana, mahakama huwa inaangalia sheria mama, amabayo katika uchaguzi ni ya mwaka 1985.
“Pingamizi la msajili wa vyama halina maana yoyote kwa sheria mama, hivyo wagombea endeleeni kufanya kazi zenu kama kawaida” alisema Mbatia. Taarifa hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta: SOURCE: MWANANCHI

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...