Friday, May 12, 2006

Nani kakudanganya, maskini hana mtetezi!

SIJUI mambo haya yataisha lini? Tunasikia na kupata taarifa kwamba tumesamehewa madeni, tumepata mikopo nafuu, tunasifiwa kwa uchumi mzuri na ‘siasa safi’ , lakini maskini hatuoni ndani.

Wafadhili nao wanatukanganya kwa mbinu zao nyingi, eti wanatusamehe madeni, huku wanatupa mikopo kwa masharti magumu. Potelea mbali hata wakitukanganya, lakini iwapi nafuu?

Hivi nani alisema kuwa tajiri anaweza kumhurumia maskini, akamtengenezea programu za kumsamehe madeni na kutoa unafuu bila ya kuona uwezekano wa kujipatia faida, tena kubwa!

Wafadhili wanatusamehe madeni huku wanatumwagia mikopo,tena inayotoka kwa walipa kodi wao tunadhani wanatupenda sana! Halafu wanajifanya kusisitiza sana maendeleo ya maskini. Maskini wenyewe hawafaidiki. Mikopo huishia, ama katika mgawo au kujenga matumbo na nyumba za wajanja kule Mbezi Beach, Masaki, Capri Point, Uzunguni, Area C na kwingineko huku maskini wakiendelea kutaabika.

Miaka miwili iliyopita Benki ya Dunia, naambiwa ilifikia uamuzi kuifutia Tanzania deni lake ambalo inadaiwa na wanachama wa klabu ya Paris, tukaambiwa maisha yatanyooka, tujiulize, sasa tunashuhudia nini?

Rais wetu mstaafu, Benjamin Mkapa alikuwa hodari sana wa kutaja takwimu za mikopo tuliyochukua na hata misamaha, lakini faida zake bado maskini halisi wa Kitanzania hawajaziona ukiacha wachache wanaopata ‘bahati’ ya kuonwa na watawala.

Wakuu wetu wa kaya yetu hii, tunayoipenda sana, sijui kwa moyo wote kwa sababu tu hatuna pa kukimbilia, sasa wanatueleza maelezo yote hayo na sifa hizo hayana maana kwamba serikali itatuwekea fedha mfukoni! Mbona wengine tunawaona wanajiwekea mifukoni mwao tena kwa fujo.

Wanapora maskini mashamba, wanawapora pia mali zao, wanawadanganya kwa pesa ya nyanya na matokeo yake kunakuwa hakuna maendeleo.

Wanafaidika kwa jasho letu, wanajineemesha kwa ujanja ujanja , wa kututega kwa kauli nzuri na mipango hewa isiyokamilika kila uchao.

Wakishapata wanaanza kututukana kwamba sisi wananchi hatuna akili, hatujishughulishi, hatuna mbinu, tumebweteka. Ebo! Hivi ni nani aliyetufikisha hapa tulipo!

Kila kukicha kundi la vijana wasio na kazi linazidi kuongezeka, linaingia mitaani huku malalamiko ya wananchi kushindwa kuweza kufikia huduma za umma sababu ya kusambaa kwa rushwa yanazidi, ukosefu wa usalama wa umma na wa raia mmoja mmoja unaongezeka, tabia ya ukandamizaji ya dola, hususan polisi na mahakama inazidi, wakati hivyo ndivyo vyombo vya kukimbilia.

Maelfu ya wananchi wanazidi kumiminika katika miji mikubwa hasa Dar es Salaam kila siku kutoka katika kila kona ya nchi, ili kujinusuru na umaskini wakiamini hapo ndipo kuna unafuu wa fursa za ajira. Ni kweli, lakini, wengi wao wanaishia katika kazi za kijungu jiko zinazouwezesha mkono uende kinywani.

Wengine wanazidi kuwa maskini kutokana na ukosefu wa hatimiliki za nyumba zao, ardhi, maghala na mambo mengine kama hayo. Maskini hawezi kuuza raslimali yake au kukopa kwa kuitumia kama dhamana.

Umaskini unawafanya kutoweza kujimudu kupata malazi wanayoyataka, hivyo wengine wenye uwezo kidogo, wanaishia kujitwalia ardhi kwa njia mbalimbali na kuanza kujiendelezea kiholela, kwa kujenga makazi, kuweka biashara na kufanya lolote linalowezekana.

Kitu ambacho serikali inashindwa kukielewa japo ilijitahidi kumwelewa mtaalam wa uchumi, raia wa Peru, Hernando De Soto na au pengine kufanya makusudi ni kutotilia maanani kwamba hawa maskini pia wanachangia katika uchumi na ni jukumu la serikali kuwapatia mahitaji ya msingi.

Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba kwanini maskini wanakosa uwezo wa kufanya mapinduzi hata kama wapo wengi, wakati katika miaka ya karibuni kumekuwapo kuongezeka kwa demokrasia?

Matokeo ya milolongo hii ndiyo yote inayowafanya maskini kuona kwamba serikali haiyatilii maanani masuala na vilio vyao. Ingawa sera nyingi zimejiegemeza katika kunyanyua maisha ya maskini, mengi yaliyomo katika sera hizo hakika hayatekelezeki na matokeo yake maskini wanakuwa maskini wa kutupwa huku matajiri wakizidi kuukata.

6 comments:

Mija Shija Sayi said...

Hivi mimi tangu mtoto nimekuwa nikisikia wimbo huu wa madeni kwa Tanzania, hivi ni lini huwa tunakopa na kwa nini? mbona sioni lolote linaloimprove kutokana na mikopo hiyo? Au hiyo mikopo ndiyo inayosaidia kujenga majengo ya vioo pale Darisalama?

Halafu kuna hili suala la maendeleo ya nchi kuelekezwa katika mkoa mmoja hivi ni kwa nini? hawa watu wanaokuja kuwekeza kwa nini hawapelekwi Singida Lindi Mtwara au Sumbawanga? maana kama vitega uchumi vingewekezwa huko basi hili wimbi la vijana kuhamia Dar lingepungua na sanasana watu wa Dar wangependa kuhamia mikoani jambo ambalo lingeifanya nchi kuwa na uwiano mzuri wa makazi.

Charahani ninakutuma kwa mheshimiwa rais juu ya hili iwapo itatokea siku ukakumbana naye naomba unifikishie ujumbe.

mwandani said...

Ili kutafuta maendeleo inabidi uwe umeendelea.

Ili kupigania uhuru inabidi uwe huru.

Nitafafanua baadaye.

Vempin Media Tanzania said...

Da Mija hili ulilozungumzia la uwiano wa maendeleo ndiyo haswaa barabara linatakiwa kufanyiwa kazi kwa kina mbona hawa wanyonyaji wanaojiita wafadhili au wahisani na majina kibao kama ndugu yangu Ndesanjo anavyowaita kwao wamefanikiwa kuweka uwiano na isingekuwa hivi.
Nimekubali maagizo yako nikipata mwanya tu nitamwuliza JK hili, lakini nadhani analijua unafikiri hajui hili Mija?
Mwandani nasubiri ufafanuzi wa kauli yako ishaallah.

Sultan Tamba said...

Mr Charahani, kinachoisumbua nchi yetu ni sheria. Hizo ndizo zinafanya mambo mengi yasiende na wananchi wengi kubaki mafukara daima, angalia sheria ya uzembe na uzururaji, yaani mtu kutembea kwenye nchi yako mwenyewe unaitwa mzembe na mzururaji, mtu atahangaika vipi! Hayo madeni mi naona 'fiksi' tu, mbona tukisamehewa hatuoni maana yoyote! Madaraka matamu, unaiba kiulaini kabisa! Lakini mwisho utafika, sijui kama Kikwete ataweza kupunguza hii hali!

boniphace said...

Charahani, hili suala nashukuru kuwa unaendeleza mjadala wangu kuhusu nani anasema kweli kuhusu Afrika? Hivi viongozi wetu wanatoa fursa ipi kwa wananchi kabla ya kuchukua mikopo hiyo? Nini nafasi ya wananchi ktika kuangalia nini kikopwe na nini kisikopwe? Je wananchi wanaweza kukubali kukopa ili wabunge wapate pesa za kununua magari ya kifahari? Nini hasa maana ya mikopo na misaada kama si mirija ya kuongeza unyonyaji na ukandamizaji wa nchi za magharuibi? Je nchi zetu haziwezi kweli kujiendesha kama hazitakubali kukopa na misaaad isiyo na faida? NAOMBA TUJADILIANE.

Jeff Msangi said...

Mikopo ni utumwa.Tunachotakiwa kufanya ni kujifunza upya ujengaji wa nchi wenye kututegemea sisi wenyewe.Naona uvivu kabisa kujadili masuala ya mikopo,misamaha ya madeni nk

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...