Sunday, February 01, 2026

VIONGOZI WA SERIKALI WASHIRIKI IBADA YA MAZISHI YA MZEE NGAJILO

 

Viongozi mbalimbali wa taifa na mkoa wakiwasili katika uwanja wa Samora katika ibada ya marehemu  Mzee Fabian Ngajilo aliyefariki dunia tarehe 29 Januari mjini Njombe.
Mzee Fabian Ngajilo ni baba mzazi wa Mbunge wa Iringa mjini na mfanyabiashara maarufu nchini Fred Ngajilo Fred Vunjabei. 
Viongozi mbalimbali wa kitaifa wa chama na serikali waliofika hadi muda huu ni Mhandisi  Hamad Masauni,  Mwenyekiti wa Wazazi Taifa wa CCM Fadhili Maganya  wakuu wa mikoa ,wakuu wa wilaya na wabunge mbalimbali.





WAZIRI MCHENGERWA AONGOZA MAZOEZI KM 4.6 DHIDI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

 


Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo Februari Mosi ameongoza mazoezi ya kutembea umbali wa kilomita 4.6 kuanzia Uwanja wa Benjamin Mkapa hadi Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi ya mwili kwa lengo la kuimarisha afya.

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa mazoezi ya mwili ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na figo, ambayo yamekuwa yakiongezeka nchini na kusababisha gharama kubwa za matibabu kwa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhimiza Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kula lishe bora na kuepuka tabia hatarishi ili kujenga jamii yenye afya na tija katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, mazoezi ya mwili huchangia kuboresha afya ya moyo na mishipa ya damu, kuimarisha misuli na mifupa, pamoja na kupunguza hatari ya udhaifu wa mwili unaosababishwa na kutofanya shughuli za kimwili.

Aidha, amesema mazoezi husaidia kuboresha afya ya akili kwa kupunguza msongo wa mawazo na sonona, kuongeza umakini na ufanisi kazini, pamoja na kudhibiti uzito wa mwili na unene uliopitiliza.

Waziri Mchengerwa amewataka wananchi, taasisi na waajiri nchini kuanzisha na kuendeleza programu za mazoezi ya mwili katika maeneo ya kazi na makazi ili kukuza mtindo bora wa maisha na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.

Mazoezi hayo yamehudhuriwa na watendaji mbalimbali wa Wizara ya Afya, wadau wa sekta ya afya pamoja na wananchi wa jijini Dar es Salaam, walioungana na Waziri katika kuonyesha kwa vitendo umuhimu wa kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha ya kila siku

TANAPA YASHINDA TUZO YA MCHANGO BORA WA UTANGAZAJI UTALII TANZANIA BARA NA VISIWANI KATIKA TUZO ZA UBUNIFU SEKTA YA UMMA 2026









Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeibuka mshindi wa Tuzo ya Mchango Bora wa Ushirikiano katika kuendeleza utalii na kuitangaza Tanzania kama kivutio kimoja cha utalii kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, katika Tuzo za Ubunifu wa Sekta ya Umma 2026, hafla iliyofanyika jana Januari 31, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.

Tuzo hiyo ilitolewa na Bodi ya Tuzo za Ubunifu katika Sekta ya Umma kwa kutambua jitihada za TANAPA katika kushirikiana na Serikali ya Zanzibar pamoja na wadau mbalimbali kutangaza vivutio vya utalii, hasa vilivyopo katika ukanda wa pwani, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Saadani, Mikumi na Nyerere.

Aidha, tuzo hiyo ilipokelewa na Afisa Uhifadhi Mshitu Mshitu, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Ofisi Kiunganishi ya TANAPA visiwani Zanzibar, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi CPA Musa Nassoro Kuji. Mshitu aliwashukuru waandaji wa tuzo hizo kwa kutambua mchango wa TANAPA kwa hasa katika nyanja ya kuitangaza nchi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Taasisi nyingine zilizotambuliwa katika hafla hiyo ni pamoja na Wizara ya Afya Zanzibar, ZHC, ZFDA, ZURA, ZAWEMA, ZAA, ZECO, ZPPRA, ZCT, ZIC, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG Zanzibar), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar (TAKWIMU Zanzibar), ZMA, ZIPA, ZVETA, IPA, ZAHRI, ZARI na ZBS, pamoja na taasisi nyingine nyingi za umma ambazo zimeonesha ubunifu, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tuzo za Ubunifu wa Huduma za Umma (Public Sector Innovation Awards) Ndugu Steven Mkomwa, aliipongeza TANAPA kwa kuendelea kuwa miongoni mwa taasisi za umma zenye ubunifu baada ya TANAPA kuwa miongoni mwa taasisi zaidi ya 40 zilizopokea tuzo za ubunifu zilizopita zilizotolewa Desemba 16, 2025 Jijini Dar Es Salaam.

TANAPA imeendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), taasisi zote zilizopo chini ya Wizara, pamoja na wadau wote wa uhifadhi na utalii nchini, kuhakikisha kuwa Hifadhi za Taifa zinaendelea kutunzwa na kutangazwa ili kufikia malengo ya Serikali ya kuvutia watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.

ULEGA AAGIZA MKATABA WA MKANDARASI MCHINA UVUNJWE


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kuanza utaratibu wa kuvunja mkataba wa kampuni ya ujenzi kutoka China ambayo imekuwa ikisuasua katika ujenzi wa barabara ya Omurushaka – Kyerwa mkoani Kagera yenye urefu wa kilomita 50.

Pamoja na agizo hilo, Waziri Ulega pia amezitaka mamlaka zinazohusika na utoaji wa kazi za ujenzi wa barabara kuiweka kampuni hiyo, Shandong Luquiao Group, katika orodha ya kampuni zisizotakiwa kupewa kazi za ujenzi wa barabara hapa nchini kwa sababu rekodi yake kwa kazi ilizopewa hairidhishi. 

"Natoa maelekezo kwa TANROADS na Mkurugenzi wa Barabara kutoka wizarani mpitie taratibu za kuvunja mkataba kwa mkandarasi huyu ndani ya mwezi mmoja ili tuweze kumchukulia hatua za kisheria, hatuwezi kuona fedha za wananchi zinachezewa kwa namna hii", amesema Ulega

Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo katika mkutano na wananchi wa Kyerwa mara baada ya kumaliza ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.

Katika mkutano huo, Waziri Ulega alitoa maagizo kwa wataalamu wa sheria kuwa wanatakiwa kufuata vigezo vyote vya kisheria ili baadaye serikali isiingie katika kesi ambazo zitaigharimu fedha nyingi kwa sababu ya kushauriwa vibaya na wataalamu. 

Awali katika taarifa zao kwa waziri , Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Kyerwa, Khalid Nsekela, walieleza kutofurahishwa kwao na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na ukweli kwamba pamoja na rekodi ya kusuasua kwake, mkandarasi huyo ameendelea kupewa kazi za ujenzi mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya TANROADS, mkandarasi huyo tayari amelipwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tisa na ingawa alitakiwa kuwa amefikia walau asilimia 50 ya lengo, hadi sasa yuko katika asilimia tano tu ya utekelezaji wa mradi.

Katika hotuba yake hiyo, Ulega aliitaka TANROADS kutafuta suluhisho la haraka kwa kumtafuta mkandarasi wa ndani mwenye uwezo atakayeikarabati barabara hiyo ndani ya mwezi mmoja ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.

Ametoa rai kwa wasimamizi wa miradi kutoka TANROADS kuhakikisha wanasimamia vyema miradi kwa mujibu wa mkataba ambapo amesema pia wasimamizi wa mradi huo wachunguzwe endapo kama wamehusika kwenye uzembe wa ucheleweshaji wa mradi huo ili hatua zichukuliwe pia dhidi yao.

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwasa amesema mkandarasi huyo amekuwa akisuasua pia katika utekelezaji wa miradi mingine ikiwemo ya TARURA katika mkoa huo na kushauri serikali kusitisha mikataba hiyo na kutompa zabuni tena mkandarasi huyo.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Ulega, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Kagera, Eng. Joel Mwambungu, amesema kuwa mradi huo kwa sasa umefika asilimia 5.43 na unafadhiliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 94.

Ameongeza kuwa mradi huo upo nyuma kwa asilimia 46.26 ambapo ni tofauti kati ya maendeleo yaliyotarajiwa ya asilimia 51.69 huku maendeleo halisi yaliyofikiwa yakiwa asilimia 5.43 pekee.









WAZIRI WA FEDHA AIMWAGIA SIFA TADB

 

Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.) kulia, akipokea  taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, ya kipindi cha miaka 10 tangu ianzishwe mwaka 2015-2025, kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Frank Nyabundege,  katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma. (Picha na KItengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-Dodoma)




BIBI CLOTILDA AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUOKOA MAISHA YAKE





Na OWM - TAMISEMI, Dodoma

Bibi Clotilda Isidory Kokupima, mkazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, amemtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, na kumuomba awasilishe shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada alioutoa wa Shilingi Milioni 20 kugharamia matibabu ya ugonjwa wa kansa ya utumbo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

Akizungumza na Prof. Shemdoe ofisini kwake, Bibi Clotilda amesema alifika ofisini hapo mahsusi kuomba shukrani zake ziwasilishwe kwa Mheshimiwa Rais, ambaye msaada wake ulimwezesha kupata matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, hatua iliyookoa maisha yake.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuokoa maisha yangu. Nilikuwa nikisumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya utumbo kwa kipindi cha miaka sita, na matibabu yalisimama baada ya familia yangu kushindwa kumudu gharama. Hata hivyo, baada ya kupata msaada wa Shilingi Milioni 20 kutoka kwa Mheshimiwa Rais, niliweza kuendelea na matibabu,” amesema Bibi Clotilda.

Ameongeza kuwa aliwasilisha barua za maombi ya msaada wa fedha za matibabu kwa wadau wasiopungua kumi, akiwemo Mhe. Rais na ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kuwasilisha ombi lake, alipatiwa msaada huo uliomuwezesha kuendelea na matibabu.

Bibi Clotilda amesema fedha hizo zilimwezesha kukamilisha matibabu katika Hospitali ya Ocean Road na baada ya kumaliza dozi ya mwisho, vipimo vilionesha kuwa hana tena ugonjwa wa kansa uliokuwa ukimsumbua. 

Ameeleza kuwa ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kila siku, huku akitakiwa kufanyiwa uchunguzi wa afya kila baada ya miezi mitatu.

Aidha, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kukubali kuwasilisha shukrani zake kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa huruma na upendo wake umeokoa uhai wake, na kumuomba aendelee kuwa msaada kwa wananchi wengine wenye uhitaji.






Na Philipo Hassan - Arusha

Kamishna wa TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji, jana Januari 31, 2026 alipokea tuzo ya “Best Development Partner Supporting Tourism Development” kwa niaba ya Shirika la Korea International Cooperation Agency (KOICA), katika hafla ya utoaji wa tuzo za The Serengeti Awards zilizofanyika katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Tuzo hiyo alikabidhiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abasi, ikiwa na dhima ya kutambua mchango wa Kituo cha “Serengeti Media Centre” kilichojengwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ufadhili na ushirikiano wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA).

Lengo la mradi huo ni kuboresha uzoefu wa watalii pindi watembeleapo hifadhi, hususan kituo cha “Serengeti Media Centre”, kwa kuwawezesha kupata picha mjongeo na mnato zinazoonyesha vivutio vya utalii na ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, hivyo kusaidia katika kuimarisha juhudi za uhifadhi kupitia teknolojia.

Pia, Kamishna Kuji alipata fursa ya kutoa tuzo kwa mshindi wa kipengele cha “Best Conservation Influencer”, ambapo mshindi alikuwa ni Nakaaya Sumari.

Tuzo za Serengeti Awards ni jukwaa adhimu ambalo limeendelea kutambua mchango wa wadau wa utalii na uhifadhi katika maendeleo ya sekta husika, huku zikichochea ubora wa huduma na ubunifu. Kupitia tuzo hizo, Tanzania inaendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa kama kinara wa utalii wa safari na wanyamapori katika bara la Afrika na duniani kote.

MKUTANO WA CATA UANGAZIE MIJADALA YA KUHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UKUSANYAJI MAPATO - MAKAMO WA RAIS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia ni chachu kati...