Friday, November 27, 2026

WAZIRI MKUU: LINDENI MAADILI YA KITANZANIA.





▪️Asema kupungua kwa fedha za wahisani si sababu ya kusitisha huduma kwa jamii

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini  yazingatie maadili ya Kitanzania na uzalendo katika utekelezaji wa shughuli zao.

Pia, Dkt. Mwigulu ameyataka Mashirika hayo  yaepuke kupokea fedha zenye masharti yanayoweza kuhatarisha utu na maadili ya Watanzania.

Ametoa wito huo leo, Novemba 27, 2026,  Wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, lililofanyika katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Amesema kuwa mashirika hayo yanapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato ndani ya nchi, kuimarisha ubia na kutumia ubunifu ili kuhakikisha huduma muhimu wanazozitoa kwa jamii haziathiriki.

Akisisitiza umuhimu wa kulinda maadili na utu wa Watanzania, Waziri Mkuu amesema: “Tusipokee fedha za kutuangamiza. Tunatafuta fedha ili tulinde utu na tuboreshe ustawi wa Mtanzania, si kupata fedha zenye masharti yanayohatarisha maadili yetu, kizazi cha sasa na kijacho. Lazima tulinde utu wetu na mustakabali wa Taifa letu kwa gharama yoyote ile.”

Waziri Mkuu ameyapongeza mashirika hayo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma muhimu, ikiwemo elimu, afya, maji na ustawi wa jamii, akibainisha kuwa mchango wake ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, ameyataka mashirika hayo yaoanishe mipango yao na shughuli zao na Dira 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, akieleza kuwa utekelezaji wa Dira hiyo unahitaji ushiriki wa wadau wote, hususan sekta binafsi inayotarajiwa kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wa mwaka 2022/23–2026/27. 

Amesema sekta hiyo imepiga hatua katika utoaji wa huduma, uzalishaji wa ajira na kuwafikia wananchi, huku akihimiza ubunifu, ubia na matumizi ya vyanzo vya ndani vya fedha.

Awali, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Bw. Jasper Makala, amesema jukwaa hilo ni fursa ya mashirika kujipanga upya kwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya mapato na kupunguza utegemezi wa ufadhili wa nje. 

Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa huduma kwa wananchi na kuimarisha mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa.

No comments:

RUAHA KUWA MWENYEJI WA PROGRAMU YA “SAFARI FIELD CHALLENGE” MSIMU UJAO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amewakaribisha waandaaji wa kipindi  cha “Safari Field Challenge” kuhamishia ...