Sunday, November 08, 2026

PIC: WAKATI WA MAGEUZI YA KWELI KATIKA MASHIRIKA YA UMMA UMEFIKA!






Yaihakikishia OTR ushirikiano wa dhati; Msajili wa Hazina asema sasa ni wakati wa kubadili uelewa wa majukumu kuwa matokeo yanayopimika.

Na Mwandishi wa OTR

DAR ES SALAAM. Mageuzi ya mashirika ya umma nchini yanaingia katika hatua muhimu inayolenga kuondoa utendaji wa mazoea na kujenga taasisi zenye ufanisi, uwajibikaji na matokeo yanayopimika, huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikiahidi kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kufanikisha mabadiliko hayo.

Akizungumza Jumamosi, Novemba 7, 2026, wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa PIC, Mhe. Ojambi Masaburi, alisema kamati yake iko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika kuhakikisha mageuzi yanayoendelea katika mashirika ya umma yanafanikiwa.

Mhe. Masaburi alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha utendaji wa taasisi za umma inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Bunge na taasisi zinazosimamia uwekezaji wa mitaji ya umma.

“Uwezo wa kuwasaidia tunao na nia hiyo tunayo,” alisema Mhe. Masaburi, akisisitiza utayari wa PIC kushirikiana na kuitetea OTR pale inapohitaji msaada wa kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

Alieleza kuwa mafanikio ya mageuzi hayo yanategemea mshikamano, uwajibikaji na utayari wa kila upande kutekeleza wajibu wake, huku akihimiza taasisi hizo kufanya kazi kwa umoja ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema mageuzi ya mashirika ya umma yamepiga hatua kubwa, lakini akasisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha viongozi wa taasisi hizo wanageuza uelewa wa majukumu yao kuwa utekelezaji wenye matokeo halisi.

Bw. Mchechu alibainisha kuwa kati ya asilimia 70 na 90 ya wakuu wa taasisi tayari wanafahamu majukumu yao na matarajio yaliyopo katika kusimamia taasisi wanazoziongoza.

“Asilimia 70 hadi 90 ya wakuu wa taasisi wanajua nini wanapaswa kufanya. Hii ni hatua kubwa katika safari ya mageuzi ya mashirika ya umma,” alisema.

Hata hivyo, alieleza kuwa kufahamu majukumu pekee hakutoshi, kwani mafanikio ya mageuzi yatapimwa kwa uwezo wa viongozi kuchukua hatua, kufanya maamuzi sahihi na kuhakikisha taasisi zao zinatimiza malengo yaliyowekwa.

Kauli hiyo inaashiria hatua mpya katika mageuzi ya mashirika ya umma, ambapo msisitizo unahamia kutoka kwenye uelewa wa wajibu kwenda kwenye utekelezaji, uwajibikaji na matokeo yanayopimika.

Katika hatua hiyo, OTR inalenga kuimarisha uwezo wa viongozi wa taasisi za umma kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku ikisisitiza umuhimu wa maamuzi yenye tija na usimamizi unaozingatia matokeo.

Bw. Mchechu aliishukuru PIC kwa ushirikiano wake na kueleza kuwa uhusiano wa karibu kati ya taasisi hizo ni muhimu katika kusukuma mbele mageuzi yanayolenga kuimarisha mchango wa mashirika ya umma katika uchumi wa Taifa.

Ziara hiyo, iliyowakutanisha wajumbe wa PIC na Menejimenti pamoja na viongozi waandamizi wa OTR, imeweka msingi wa kuendeleza ushirikiano katika kusimamia mageuzi hayo.


No comments:

SERIKALI YANUNUA ASILIMIA 27.73 YA HISA TMRC KWA ZAIDI YA BIL.17/-

SERIKALI imekuwa mwanahisa mkubwa zaidi wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC) baada ya kukamilisha umiliki wa asilimia 27.73 ya his...