Tuesday, May 30, 2006

Gari chapa ng'ombe mwalikumbuka hili

(Picha na Yahya Charahani)
Kwa wale waliokulia maeneo haya, hili ni jambo la kawaida ukitoka mjini, shambani sijui hadi wapi kote ni haya haya, na kwa mbaaali nadhani mwaweza kuona nyumba ya tembe zinazojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa nyasi na udongo. Mungu tusaidie haya ndo maisha tuliyo nayo sasa katika karne hii ya sayansi na teknolojia licha ya kwamba wenzetu wapo wanaojigamba kwa kuwa na ma-bangalow kote nchini. Hapa ni kijiji kimoja kinaitwa Mwanjoro, wilaya ya Meatu, Shinyanga nilikuwa katika ziara ya kikazi.

Saturday, May 27, 2006

Huyu naye vipi kaingia kijijini hivi hivi tu

Kumekucha tena wanakijiji wenzangu sasa kuna kitu kipya chenye mambo kibao, ambayo bila shaka yana faida kuwa kwetu sote, blogu hii imeingia kistaili yake na bila shaka mtakubaliana nami kwamba sasa tunasonga mbele katika haya masuala ya teknolojia. Ukitaka mambo mapya hebu bonya hapa . Kwa huyu kwa taratibu zetu za hapa kijijini unaweza kugonga kuomba chumvi, kibiriti na hata mshumaa kama umechacha.

Thursday, May 25, 2006

CHAKULA KWA WATOTO MASHULENI


Wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili katika Shule ya Msingi Twende Pamoja, iliyopo katika kijiji cha Mwamalili, Wilaya ya Shinyanga mjini, Tanzania wakigawiwa chakula cha mchana na wenzao, ikiwa ni katika mpango wa kupunguza utoro na kuongeza ubora wa elimu unaosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Misaada la Oxfam, tangu kuanza kwa mpango huo mahudhurio ya watoto yameongezeka. (Picha na Yahya Charahani)Toa maoni yako.

Tuesday, May 16, 2006

Huruma zetu Wabongo tumezificha wapi

Bibi Kikongwe Asha Msawila wa Kijiji cha Mkamba, Morogoro akitoka nje ya kasri lake, hebu fikiria haya ndo maisha. Picha hii imepigwa na Kaanaeli Kaale.

KWETU Tanzania, kidesturi unapoamka hakuna siku utaamka ukamsalimu jirani au ndugu yako wa karibu akakujibu kuwa mambo ni safi sana, ikitokea hivyo huwa ni nadra mno.

Unapotoa salamu, moja kwa moja tegemea majibu kama: Habari mbaya, Tunaumwa umwa, Alhamdulillahi, Tunaendelea hivyo hivyo na mengine mengi. Ndugu zangu kina Makene, Ndesanjo, Mwaipopo,Jeff, na Tungaraza nadhani bado wanaikumbuka hii hali.

Inawezekana tukajibu hivyo kwa vile huwa tunakabiliwa na matatizo. Wala sina maana kwamba tunapokuwa na matatizo, basi tusiseme hivyo, lakini sijui ni asili yetu kujisikia wanyonge au ni hali ya maisha ndiyoinayotupeleka hivyo, au ni walalamishi!

Wenzetu wa ughaibuni hapa niseme kabisa weupe ni wawazi wanapokuwa na unafuu wa maisha husema kabisa mambo ni safi, mambo ni barabara , murua na kila kitu cha namna hiyo, ni safi sana. Pengine ni kwa sababu walishatunyonya katika mfumo usio wa haki.

Lakini, hili la unyonge si la kulipuuzia hata kidogo, hebu tujiulize unyonge wetu huu unatokana na nini je ni uvivu wetu tu, na au ni uzembe?

Kama wanaojituma wanafanya kazi kwa bidii, damu au hata jasho, kwa machozi na mabavu wanafanya hivyo, lakini kila kukicha wanabakia pale pale hawasongi mbele, tujiulize, hivi tatizo ni nini hasa.

Zipo taarifa kwamba wananchi wengi sasa wamefuta baadhi ya milo ya siku, utakuta au wanakula chakula cha mchana pekee, halafu ndiyo basi tena.

Au wanakula chakula cha usiku pekee halafu ndiyo siku inakwisha au chakula kinasogezwa mpaka jioni halafu siku imekwenda hivyo.

Watafanyaje wakati bei ya mchele imepanda mara dufu hivi sasa inakimbilia Sh1,300 au zaidi wakati muda mfupi uliopita ilikuwa Sh600, mkaa ambao ndiyo kimbilio la wengi umefikia Sh22,000 kwa gunia wakati ulikuwa chini ya 10,000, maharage ya soya nayo hayashikiki wakati kipato kimebakia pale pale au kushuka.

Kwa mahesabu ya kawaida tu uchukulie mwananchi anayeishi mjini na kisha anafanya pengine kazi na mara nyingi ni kibarua analipwa Sh 60,000, kwa maisha ya sasa atafanya nini ili aweze kujimudu wakati kila kitu kimepaa.

Nauli ya daladala inazidi kupaa ilikuwa sh. 150 sasa inakimbilia 250 hadi 400, hii ina maana kwamba ikiwa ni kwa kwenda na kurudi ni kati ya Sh 500 na 1,000 hiyo kama mhusika ana usafiri wa moja kwa moja.

Hii ikijumlishwa kwa mwezi inamaanisha kuwa nusu ya kipato itaondoka kwa usafiri tu, bado chakula, bado watoto hawajaenda shule, bado hawajaugua na bado mlolongo mrefu wa vitu vinavyohitajika kwa maisha ya kila siku.

Yote hii inafanyika kwa kivuli kwamba bei ya mafuta imepanda, ukosefu wa mvua na umeme, ingawa sasa tatizo la ukosefu wa mvua limeondoka na limeingia jingine la maafa ya mafuriko.

Haya yote yanatoa kitu kinachoitwa,Mshtuko wa moyo kwa wakazi siyo wa mijini tu bali hata wale wa vijijini sasa, ule wakati wa kuishi bila senti kwa muda hata wa miezi sita unakwisha na sasa kila kitu pesa tena pesa nyingi.

Mfumuko huu wa bei umefanya watu wengi wawe na mawazo kama ya rafiki yangu mmoja aliyeibuka na aina yake ya kaulimbiu, yeye ameigeuza kauli mbiu akisema : Ari Mpya, Kasi mpya, maisha magumu kwa kila Mtanzania.

Kwa ufupi, maisha ya Mtanzania halisi maisha yake yamekuwa taabu tupu wakati hakuna dalili zozote za kuleta matumaini kesho itakuwa vipi! Yaani, inakuwa afadhali jana kuliko leo.

Kuna watu miongoni mwetu wameshakata tamaa ya kaulimbiu au maneno matamu matamu, kwa kuwa wanaona kila mtu amepotea, kila mtu anajali maisha yake binafsi na hakuna anayewatetea.

Watu kama hawa ni wengi siyo wa kuhesabu wanalalamika chini chini kwani hawana pa kusemea wanaishia kunong’ona na siku zinatokomea bila huruma.

Wakati kuna wajanja wanabugia au kula raha kwa fujo, wanawanyonya damu hawa hawa wenye kipato cha chini, wanaopata kipato kwa kutukanwa na kunyanyaswa.

Hata kama ni wachache, hao hawana budi wadhibitiwe ili wapunguze unyonyaji huo, wanatumaliza wenzao taratibu, kwa mfano kuna haja gani ya kupanga njama kuuza vitu kwa bei ya juu wakati mnaouza mnanunua shambani kwa bei ya chini.

Mbona mahindi yapo mengi. Mbona mchele upo mwingi. Mbona mafuta mnanunua kwa bei ya chini kwanini muuze kwa bei ya juu. Hata kama ni soko huria hii itakuwa ni soko hulia. Lile la kihuni, ambalo halina huruma.

Friday, May 12, 2006

Nani kakudanganya, maskini hana mtetezi!

SIJUI mambo haya yataisha lini? Tunasikia na kupata taarifa kwamba tumesamehewa madeni, tumepata mikopo nafuu, tunasifiwa kwa uchumi mzuri na ‘siasa safi’ , lakini maskini hatuoni ndani.

Wafadhili nao wanatukanganya kwa mbinu zao nyingi, eti wanatusamehe madeni, huku wanatupa mikopo kwa masharti magumu. Potelea mbali hata wakitukanganya, lakini iwapi nafuu?

Hivi nani alisema kuwa tajiri anaweza kumhurumia maskini, akamtengenezea programu za kumsamehe madeni na kutoa unafuu bila ya kuona uwezekano wa kujipatia faida, tena kubwa!

Wafadhili wanatusamehe madeni huku wanatumwagia mikopo,tena inayotoka kwa walipa kodi wao tunadhani wanatupenda sana! Halafu wanajifanya kusisitiza sana maendeleo ya maskini. Maskini wenyewe hawafaidiki. Mikopo huishia, ama katika mgawo au kujenga matumbo na nyumba za wajanja kule Mbezi Beach, Masaki, Capri Point, Uzunguni, Area C na kwingineko huku maskini wakiendelea kutaabika.

Miaka miwili iliyopita Benki ya Dunia, naambiwa ilifikia uamuzi kuifutia Tanzania deni lake ambalo inadaiwa na wanachama wa klabu ya Paris, tukaambiwa maisha yatanyooka, tujiulize, sasa tunashuhudia nini?

Rais wetu mstaafu, Benjamin Mkapa alikuwa hodari sana wa kutaja takwimu za mikopo tuliyochukua na hata misamaha, lakini faida zake bado maskini halisi wa Kitanzania hawajaziona ukiacha wachache wanaopata ‘bahati’ ya kuonwa na watawala.

Wakuu wetu wa kaya yetu hii, tunayoipenda sana, sijui kwa moyo wote kwa sababu tu hatuna pa kukimbilia, sasa wanatueleza maelezo yote hayo na sifa hizo hayana maana kwamba serikali itatuwekea fedha mfukoni! Mbona wengine tunawaona wanajiwekea mifukoni mwao tena kwa fujo.

Wanapora maskini mashamba, wanawapora pia mali zao, wanawadanganya kwa pesa ya nyanya na matokeo yake kunakuwa hakuna maendeleo.

Wanafaidika kwa jasho letu, wanajineemesha kwa ujanja ujanja , wa kututega kwa kauli nzuri na mipango hewa isiyokamilika kila uchao.

Wakishapata wanaanza kututukana kwamba sisi wananchi hatuna akili, hatujishughulishi, hatuna mbinu, tumebweteka. Ebo! Hivi ni nani aliyetufikisha hapa tulipo!

Kila kukicha kundi la vijana wasio na kazi linazidi kuongezeka, linaingia mitaani huku malalamiko ya wananchi kushindwa kuweza kufikia huduma za umma sababu ya kusambaa kwa rushwa yanazidi, ukosefu wa usalama wa umma na wa raia mmoja mmoja unaongezeka, tabia ya ukandamizaji ya dola, hususan polisi na mahakama inazidi, wakati hivyo ndivyo vyombo vya kukimbilia.

Maelfu ya wananchi wanazidi kumiminika katika miji mikubwa hasa Dar es Salaam kila siku kutoka katika kila kona ya nchi, ili kujinusuru na umaskini wakiamini hapo ndipo kuna unafuu wa fursa za ajira. Ni kweli, lakini, wengi wao wanaishia katika kazi za kijungu jiko zinazouwezesha mkono uende kinywani.

Wengine wanazidi kuwa maskini kutokana na ukosefu wa hatimiliki za nyumba zao, ardhi, maghala na mambo mengine kama hayo. Maskini hawezi kuuza raslimali yake au kukopa kwa kuitumia kama dhamana.

Umaskini unawafanya kutoweza kujimudu kupata malazi wanayoyataka, hivyo wengine wenye uwezo kidogo, wanaishia kujitwalia ardhi kwa njia mbalimbali na kuanza kujiendelezea kiholela, kwa kujenga makazi, kuweka biashara na kufanya lolote linalowezekana.

Kitu ambacho serikali inashindwa kukielewa japo ilijitahidi kumwelewa mtaalam wa uchumi, raia wa Peru, Hernando De Soto na au pengine kufanya makusudi ni kutotilia maanani kwamba hawa maskini pia wanachangia katika uchumi na ni jukumu la serikali kuwapatia mahitaji ya msingi.

Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba kwanini maskini wanakosa uwezo wa kufanya mapinduzi hata kama wapo wengi, wakati katika miaka ya karibuni kumekuwapo kuongezeka kwa demokrasia?

Matokeo ya milolongo hii ndiyo yote inayowafanya maskini kuona kwamba serikali haiyatilii maanani masuala na vilio vyao. Ingawa sera nyingi zimejiegemeza katika kunyanyua maisha ya maskini, mengi yaliyomo katika sera hizo hakika hayatekelezeki na matokeo yake maskini wanakuwa maskini wa kutupwa huku matajiri wakizidi kuukata.

Monday, May 08, 2006

Zuma amepakwa mafuta!!!!

Ile kadhia ya kubaka iliyodumu muda wa miezi kadhaa iliyomkumba Makamu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye ni mtu muhimu anayeangaliwa na baadhi ya Waafrika Kusini kama mrithi wa Thabo Mbeki ya imemalizika baada ya Jaji Willem van der Merwe kutoa maamuzi kuwa yule mwanamama aliyedai kubakwa na Zuma alifanya vile kwa ridhaa yake. Lakini bado kuna suala la rushwa na mengineyo. Vijana wa ANC wengi wao mategemeo yao ni yeye hebu bonya hapa Mashtaka ya ubakaji yaliyokuwa yakimsibu Bwana Zuma,yaliweka ufa mkubwa ndani ya chama tawala cha ANC,ambapo kiongozi huyo alionekana kupewa nafasi kubwa ya kuwa Urais mara Rais wa sasa Thabo Mbeki atakapong’atuka.
Jaji Merwe,akisoma hukumu iliyokuwa ikitangazwa na kuoneshwa moja kwa moja katika radio na televisheni, alieleza kwamba Bwana Zuma pamoja na mwanamke aliyekuwa mlalamikaji,walikubaliana kwa hiyari yao kufanya mapenzi nyumbani kwa Zuma mwezi wa Novemba mwaka jana.
Wanaharakati wa mapambano dhidi ya ukimwi walikuwa wanatokwa na machozi baada ya kutolewa hukumu hiyo.
Wakati kesi hiyo ikiendela wanaharakati hao,walimshutumu Zuma kwa kutoa ushahidi kwamba hakutumia kondom wakati alipozini na mwanamke aliyekuwa amemshtaki,huku Zuma akifahamu kuwa mwanamke huyo alikuwa mwathirika wa ukimwi.

Friday, May 05, 2006

Hongera sana Waziri MK

JAMANI msishangae hii templeti ya blogu yangu nimeipata wapi, siyo ufundi wangu ni utundu, ugunduzi, kipaji na sijui tuseme nini cha ndugu yangu MK ambaye kupitia rafiki yangu Makene, ameweza kufanya mamboz bureeeee! Sikununua mimi, nilichofanya nilipokutana na Waziri MK nilizungumza naye mtandaoni na kisha baada ya muda nikaona kama miujiza vile mambo yakabadilika!
Nakupa pongezi ndugu yangu MK, Mungu akujaalie ujasiri huu huu wa kutuinua wabongo wenzako hivi sasa. Blogu zetu zina touch ya kibongo zaidi. Nilitamani sana blogu zetu ziwe zinalenga lenga maisha yetu kule bushi kwani hayo ndiyo maisha yetu hayo. Nirudie tena hongera saana ndugu yangu MK sijui tukupe nini!

Wednesday, May 03, 2006

Takrima chali, bado zingine ili kustawisha demokrasi

WIKI iliyopita ile sheria angamizi iliyoanza kijichimbia mizizi, iliyokuwa nia ya kuingiza wakora na matajiri madarakani na kuzuia kabisa haki na nafasi ya walalahoi kupata nafasi za uongozi, takrima, ilitupiliwa mbali.

Sheria hiyo iliyokuwa na nia na madhumuni ya kuwapora wananchi uhuru wa kuchagua viongozi kwa utashi wao, na kuwazuia kuhoji uporaji huo, kutokana na kuweka masharti magumu ya kuhoji njia ya kujipatia madaraka hayo ya uwakilishi.

Hii ni sheria nayothubutu kuiita ya ajabu ajabu ambayo chama tawala iliiunda kwaajili ya kujilindia maslahi yao kwa madai eti inaendana na ukarimu na utamaduni wa Watanzania.

Hivi nani asiyejua kwamba kwa mujibu wa desturi za Kiafrika, mwenyeji huwa ndiye mwenye wajibu wa kuwakirimu wageni na sio mgeni kukirimu wenyeji, sasa ilikuwaje mpaka hawa watunga sheria wakajipangia utaratibu huu dhalimu!

Mgeni kukirimu mwenyeji siyo kawaida sana (ukiacha ndugu, jamaa na marafiki), ingawa imeanza kujiotesha mizizi siku za karibuni. Ni rushwa.

Sheria yenyewe iliyotupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Tanzania, ni inayohusu vifungu vya 119(2) na 119(3) vya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kama ilivyorekebishwa mwaka 2000 vinavyoruhusu matumizi ya takrima katika uchaguzi.

Mahakama ilifikia uamuzi huo kwa kuwa vifungu hivyo vinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.

Hakuna kati yetu (labda watoto wadogo) ambaye hajashuhudia namna serikali zilivyojibadili, badala ya kuwa watetezi wa wanyonge na au wajenzi wa taifa, wakabadilika na kuwa wakandamizaji wa raia na waliopenda kujitajirisha wenyewe. Na wakatamani kubaki hivyo milele.

Ukarimu wa kupeana chumvi, kanga , vitenge na pombe na kisha kuyapeleka kiupogoupogo maisha ya watu hao kwa miaka mingine mitano!

Ukarimu wa kujidai kuoneana huruma wakati wa kutafuta ulaji, na mkishaingia katika chombo cha kutunga sheria mnakaa kimya, wengine hata miaka mitano! Hivi hamna namna ya kukarimu wenzenu? Kwanini isiwe wakati wa shida.

Wengine wakishamaliza ‘ukarimu’ wao huo wanahama kabisa majimbo yao kwa miaka mitano na kisha kujificha Dar es Salaam na Dodoma na inapofika miaka mitano wanarejea ‘ukarimu’ wao huo.

Tunaweza tukawa angalau tumevuta pumzi wapenda demokrasia, lakini bado kuna sheria nyingine ambazo zinaendelea kuturejesha kulekule, mathalani sheria ya uchaguzi inayokataza ugombea binafsi.

Itakosa nini ikiruhusu wagombea binafsi zaidi ya kupata faida, kwanza malalamiko yatapungua, lakini pili wananchi wasio na upenyo wa kugombea watapata fursa ya kuitumia haki yao ya kidemokrasia.

Hivi tutakosa nini au serikali ambayo iko chini ya chama tawala itabadili sheria na mfumo mzima wa uchaguzi ambao unachochea tabia chafu kama rushwa.

Au pia tutakosa nini tukirekebisha sheria za usajili wa vyama kuwa huru kuungana ili kusudi wakichoshwa na CCM wanaunda umoja wao chap chap na kisha wanashinda. Hapa sina maana miunganiko kama ile ya Kenya la hasha namaanisha miungano endelevu.

Kama Tanzania tunataka kustawi, tunatakiwa kuondokana na dhana za kujiona sisi ni bora kuliko wengine kwani wapo wengi wanaweza kutenda au kuendesha nchi vyema kuliko sisi.

Cha msingi pia kwa upande wa wananchi ni kubadili mitazamo, fikra, desturi ili hata akija tajiri wananchi tuwe tumejiandaa kisaikolojia kukataa rushwa ya chumvi na kanga kwa mustakabali mwema wa taifa letu.

Rais wa Sierra Leone Awasili nchini

Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone, Mheshimiwa Julius Maada Bio, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kilele wa Wak...