Thursday, December 26, 2024

Furahia Utulivu wa Asili Katika Hifadhi ya Mpanga/Kipengere Msimu Huu wa Sikukuu














Katika kipindi hiki cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaendelea kuwakaribisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea hifadhi zake mbalimbali. Moja ya vivutio vya kipekee vinavyopatikana ni Hifadhi ya Mpanga/Kipengere, iliyoko katika mikoa ya Mbeya na Njombe, eneo ambalo limebeba uzuri wa asili wa nadra unaofaa kwa kupumzisha akili na kuburudisha moyo.

Uzuri wa Maporomoko ya Maji

Hifadhi ya Mpanga/Kipengere inajivunia maporomoko ya maji yenye mvuto wa pekee, ambayo yamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotafuta utulivu na uzuri wa mandhari ya asili. Maporomoko haya yanatoa nafasi ya kipekee kwa wageni kupiga picha, kufanya matembezi ya miguu, na kufurahia upepo mwanana huku wakisikiliza sauti ya maji yakitiririka.

Utajiri wa Mimea na Wanyamapori

Mbali na maporomoko ya maji, hifadhi hii ni makazi ya aina mbalimbali za mimea na wanyamapori. Wageni wanapata nafasi ya kushuhudia uzuri wa mandhari ya milima, misitu, na mabonde yanayovutia, huku wakikutana na viumbe hai vinavyoifanya hifadhi hii kuwa hazina ya kipekee ya mazingira nchini Tanzania.

Sababu za Kutembelea Mpanga/Kipengere

Hifadhi ya Mpanga/Kipengere si tu mahali pa kuona vivutio vya asili, bali pia ni eneo maalumu linalofaa kwa wale wanaotafuta utulivu wa kiakili na kimwili. Hifadhi hii inatoa nafasi ya kukwepa pilikapilika za maisha ya mijini, kuondoa msongo wa mawazo, na kufurahia mazingira tulivu yaliyojaa amani.

Kwa wale wanaopenda matembezi ya kiutalii, kupiga kambi, au kujifunza kuhusu uhifadhi wa mazingira, Mpanga/Kipengere inawakaribisha kwa mikono miwili. Wageni wanahakikishiwa uzoefu wa kipekee ambao hautasahaulika.

Fursa ya Kufurahia Fahari ya Nchi Yako

Kwa moyo wa dhati, TAWA inawaalika Watanzania wote na wageni wa kimataifa kuja kushuhudia na kufurahia uzuri wa Hifadhi ya Mpanga/Kipengere. Hii ni nafasi ya kuungana na familia na marafiki, kuunda kumbukumbu za kudumu, na kufurahia fahari ya utajiri wa asili wa Tanzania.

Kwa maelezo zaidi na kupanga ziara yako, wasiliana nasi kupitia nambari +255 682 673 761 au +255 676 475 541.

Hifadhi ya Mpanga/Kipengere: Mahali Maalumu kwa Watu Maalumu kama Wewe.


Monday, December 23, 2024

WAZIRI KOMBO APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA MWAKILISHI MKAZI WA UMOJA WA MATAIFA NCHINI

 







Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thatib Kombo amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Bi. Susan Namondo katika Ofisi Ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam Desemba 23, 2024.

Akipokea nakala hizo Waziri Kombo amempongeza Bi Nomondo  kwa uteuzi aliuopata na amemuahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi atakachokuwa nchini kuuwakilisha Umoja wa Mataifa.

Aidha, Mhe. Kombo ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa mchango wake katika kuiwezesha Tanzania kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 kupitia Mfumo wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF) wa mwaka 2022-2027. 

Kwa upande wake Mwakilishi huyo Mkazi wa Umoja wa Mataifa ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezzi mazuri na amehaidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania ili kuwezesha utekelezaji wenye matokeo mazuri wa malengo ya maendeleo endelevu nchini Tanzania.

RC CHALAMILA ATOA SALAAM ZA CHRISTMAS NA MWAKA MPYA 2025



Kuelekea sikukuu za Chrismas na Mwaka mpya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amesema ulinzi na usalama umeimarishwa ili kuhakikisha wananchi hususani wakazi wa Mkoa huo wanakuwa salama katika kipindi chote cha sikukuu na baada ya sikukuu, pia amewataka wazazi na walezi kusimamia vema usalama wa watoto kwa kutowapeleka kwenye maeneo hatarishi.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Disemba 23,2024 katika Hotel ya Johari Rotana jijini Dar es salaam wakati akitoa salamu za sikukuu za Chrismas na Mwaka mpya amesema Mkoa kupitia jeshi la polisi umeimarisha ulinzi ambapo ameitaka jamii kushirikiana na serikali kudumisha amani ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla

Aidha Kupitia salamu hizo za sikukuu  RC Chalamila amewatoa shaka wananchi wa Mkoa huo kuhusiana na miradi ya ujenzi wa barabara kupitia DMDP ambayo imeonekana kuchelewa ambapo amesema miradi hiyo imeshakabidhiwa kwa wakandarasi na inatarajia kuanza mapema januari mwaka 2025 huku pia akieleza mipango ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi.

Vilele RC Chalamila amezungumzia mkakati wa kuanza kwa shughuli za kibiashara saa 24 eneo la Kariakoo ambapo amesema zoezi hilo litazinduliwa rasmi mwezi januari 2025 ambapo wakuu wa wilaya,wakurugenzi na maafisa biashara wanapaswa kuainisha maeneo ambayo biashara zinaweza  kufanywa saa 24  ikiwwmo eneo la kariakoo 

Sanjari na hayo Chalamila amezungumzia mikakati ya Mkoa huo kupokea wanafunzi wa chekechea, darasa la kwanza na kidato cha kwanza na kueleza kuwa serikali imeendelea kuwekeza fedha ili kufikia malengo ya elimu hivyo ambapo amehimiza wafanyabiashara kulipa kodi ili malengo hayo yaweze kutimia

Mwisho akijibu maswali ya waandishi wa habari RC Chalamila ameeleza mipango ya kuboresha huduma za usafiri wa mwendokasi maarufu BRT ambao kwa sasa  amesema idadi ya mabasi haitoshelezi , pia amehimiza madereva kutoingilia njia za mabasi ili kuepuka ajali na amesisitiza wananchi kutovamia maeneo kiholela kufanya biashara

Ifahamiki kuwa utaratibu huu wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam kutoa salamu za sikukuu za mwisho wa mwaka imekuwa na nafasi kwa mkuu wa mkoa kuelezea maendeleo ya mkoa huo na changamoto zilizopo

Saturday, December 21, 2024

RC CHALAMILA AKUTANA NA VIONGOZI WA WAFANYABIASHARA KARIAKOO PAMOJA NA WADAU WENGINE



-Wajadili hali ya usalama katika Soko la Kariakoo.

-Aeleza dhamira ya Mkoa kuwa na mpangilio mzuri wa wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Disemba 21, 2024 amekutana na wadau mbalimbali wa Biashara katika eneo la Kariakoo pamoja na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO, TANROAD, LATRA, DAWASA, Taasisi za fedha na Kamati ya Usalama ya Mkoa

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili maswala mbalimbali yenye lengo la kuboresha ufanyaji biashara Kariakoo unaokidhi viwango vya kimataifa hususani hali ya usalama ambayo itawezesha biashara kufanyika saa 24, ambapo RC Chalamila ameipongeza Halmashauri ya Jiji kwa kuanza mchakato wa ununuzi wa Camera ambazo zinatarajiwa kufungwa maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kariakoo.

Aidha Katika kupunguza msongamano kwenye eneo la kariakoo RC Chalamila amesema kupitia kikao hicho wamejadili mpango maalum shirikishi wa kuzuia aina zote za magari,bajaji na pikipiki kuingia katikati ya mitaa ya soko la kariakoo wakati wa asubui, mchana na jioni. 

Vilevile RC  Chalamila amesema eneo la kariakoo ni muhimu kibiashara linahudumia Tanzania na nchi jirani hivyo magari yataruhusiwa kuingia nyakati za usiku pekee ili kupunguza msongamano na kuruhusu biashara kufanyika bila usumbufu asubuhi hadi jioni

Sambamba na hilo Mhe Mkuu wa Mkoa amesema ifike wakati Kariakoo iwe ni "Special Zone ya Kibiashara" mtu akitaka kufanya biashara lazima awe amekidhi vigezo vitakavyowekwa.      

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara na wadau wengine ikiwemo taasisi za fedha kuona namna ya kuongeza muda wa kufanya kazi hadi usiku hususani katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi

Sanjari na hilo amelitaka jeshi la polisi kuimarisha ulinzi kwa wafanyabiashara na wananchi katika kipindi hiki cha sikukuu ambapo amesema kwenye kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka uhitaji wa bidhaa mbalimbali huongezeka kwa wananchi hivyo mpango huu wa kuongeza muda wa kufanya kazi utawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi

NAIBU WAZIRI LONDO AWATAKA WATUMISHI WANAOTOA HUDUMA MIPAKANI KUFANYA KAZI KWA BIDII WELEDI NA UADILIFU








Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. DENNIS L. LONDO (Mb.) amewataka watumishi wanaotoa huduma mipakani kufanya kazi kwa bidi, weledi na uadilifu. Mhe. Londo ametoa rai hiyo alipokuwa akiongea na watumishi wanaotoa huduma katika Kituo cha Utoaji Huduma kwa Pamoja cha Holili/Taveta, Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani (OSBPs).

Akiwa katika mpaka huo, Mheshimiwa LONDO alijionea shughuli za biashara zinazofanyika mpakani hapo, miundombinu ya kituo hicho pamoja na kuongea na wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwenye mpaka huo. 

Waziri LONDO amewasihi wafanyakazi hao kufanya kazi kwa maarifa, jitihada na kujiepusha na vitendo viovu ambavyo vinaweza kuchafua taswira ya nchi nje ya mipaka, pamoja na kukwaza ufanyaji biashara. Ametaja baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na rushwa na lugha zisizo na staha kwa wafanyabiashara na watumiaji wengine wa mipaka hiyo.

"Nyinyi watumishi wa mpaka huu wa Holili pamoja na mipaka yote nchini ni kioo cha nchi yetu katika kuhudumia wageni hivyo mnapaswa kufanya kazi zenu kwa weledi, bidii na maarifa makubwa ili kulinda taswira ya nchi yetu nje na ndani ya mipaka". Alisisitiza Mhe. LONDO.

Aidha, Mheshimiwa Londo amewakumbusha watumishi hao wajibu wao katika kuwasaidia wafanyabiashara za mipakani kufikia malengo yao badala ya wao kuwa sehemu ya vikwazo na lugha zisizofaa wakati wa kuwahudumia. Vilevile, Mhe. LONDO amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano kwa taaisi zote za mipakani.

Kuhusu ushirikishwaji wa Halmashauri katika kuwezesha wafanya biashara wadogo kunufaika na fursa za Mtangamano wa Afrika Mashariki, Mhe. LONDO amezitaka Halmshauri kubuni mikakati ya jinsi kuwashirikisha wananchi wao kunufaika na uwepo wa mipaka hiyo katika Mikoa na Halmashajri zao. Mheshimiwa Londo amezitaka Halmashauri zilizo mipakani kujumuisha katika mipango na bajeti zake mikakati ya kuongeza tija na kuwawezesha wafanyabiaashara wa mipakani hususan vijana na akina mama kutumia kikamilifu fursa za Mtangamano wa Afrika Mashariki.

Akiwa katika mpaka huo wa Holili, Mhe. LONDO amekutana pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe, RAYMONDI MANGWALA, wawakilishi  kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Mawakala wa Forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Holili wa upande wa Tanzania na Kenya

Awali, akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mhe. RAYMOND MANGWALA alimwelezea Mhe. LONDO kuwa Mpaka wa Holili upo salama na shughuli za biashara katika mpaka huo zinaendelea vizuri ambapo kumekuwa na ushirikaino mzuri miongoni mwa Taasisi zinazofanya kazi katika mpaka huo kiasi cha kupelekea mpaka huo kuwa miongoni mwa mipaka inayofanya vizuri katika kufikia malengo ya kiforodha. 

Aidha, Mhe. MANGWALA hata hivyo alieleza changamoto kadhaa ikiwemo uwepo wa vipenyo vingi vinavyochochea biashara ya magendo na kubainisha kuwa pamoja na jitihada za Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya katika kukabiliana na vitendo hivyo, kuna umuhimu wa kutumia njia za kisasa za kitekenolojia katika kukubaliana na biashara  za magendo katika Wilaya hiyo.

Waziri Chana afungua Same Festival, atoa maagizo mazito ya sekta





Na John Mapepele 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe, Balozi.Dkt. Pindi Chana ( Mb) amezitaka Halmashauri za wilaya zote nchini kuanzisha matamasha ya Utalii na Uhifadhi huku akielekeza suala la kuwalinda wananchi dhidi ya  wanyamapori wakali na waharibifu kuwa ajenda ya kudumu.

Mhe. Chana ametoa kauli hiyo leo Desemba 21, 2024  wakati akimwakilisha Mhe. Waziri Mkuu kufungua rasmi msimu wa pili wa Tamasha la Utalii la Same ambapo pia ametoa zawadi  na tuzo kwa wadau mbalimbali kutambua mchango wao katika kufanikisha Tamasha hilo 

"Wakati leo tunasherekea  Tamasha la pili la Utalii la Same ni lazima  tuhakikishe tunawalinda wananchi kutokana na wanyama wakali wakati huo huo tunahifadhi rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu ili zitusaidie kutuletea watalii zaidi " amefafanua Mhe Chana. 

Amesema Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI na  wananchi itaendelea kuhifadhi rasilimali kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha amefafanua kuwa usemi wa kiswahii usemao "Tunza mazingira yakutunze"  unadhihirisha kuwa mazingira yakitunzwa vizuri ikiwemo misitu na maliasili yatasaidia kujenga uchumi.

 "Tukitunza mazingira tutapata mvua, tutapata maji, tutalima, tutapata vyakula na mazao ya biashara, hakutakuwa na njaa wala umaskini wa kipato na pia tutaishi kutokana na Kuvuta hewa safi.Usemi huo una mashiko ni vyema tukarithisha watoto wetu kuanzia wawapo shuleni ili waweze kutambua umuhimu wa kutunza mazingira"ameongeza Mhe. chana

 Amesema ni muhimu klabu za mazingira zilizopo katika maeneo yetu kuendelea  kuzisimamia ili zilete tija kwani kupitia klabu hizo wanafunzi watajifunza hifadhi ya mazingira, utalii na pia watajenga uelewa wa kutosha kutenda popote wawapo kwa falsafa ya "Jenga kesho iliyo bora (BBT)".  

Amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuandaa Filamu ya Tanzania the Royal Tour na Amazing Tanzania ambapo amesema kuanzishwa kwa Tamasha la Utalii la Same ni  kufuata maono ya Mhe. RAIS katika kutangaza utalii.

Akifafanua kuhusu faida ya Tamasha hilo amesema limesaidia kuwaletea wageni, pia kutoa elimu mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji kama misitu wa Chome.

Pia kuhusu kuboresha na Tamasha hilo, Mhe. Chana ametaka kuwepo na mikakati madhubuti ya kuendeleza Tamasha hilo kwa  Halmashauri kutenga   bajeti kuliko kuwaachia wadau wachache na uongozi wa Wilaya hiyo huku akisisitiza kuwa suala la uhifadhi na utalii lipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

"Ndugu zangu suala hili ni la msingi sana hata baba wa Taifa Mwalimu  Nyerere alisisitiza kuwa rasilimali hizi lazima zilindwe na ndiyo maana  tuna Jeshi la Uhifadhi"amefafanua Waziri Chana

Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kuwabaini watu waovu, wanaotaka kuhujumu  rasilimali za watanzania.

"Kuna changamoto za maingiliano  tuliangalie ili wasilete madhara".

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Metheusela Ntonda amesisitiza kuendelea kufungamanisha Utalii na utamaduni kwenye matamasha hayo.

 Tamasha hilo limepambwa na wasanii mbalimbali na linatarajiwa kumalizika hapo kesho.

Friday, December 20, 2024

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA TUZO ZA UHIFADHI NA UTALII KATIKA HAFLA KUBWA JIJINI ARUSHA




 



Arusha, Desemba 20, 2024 - Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo amewasili katika Ukumbi wa Hoteli ya Mt. Meru jijini Arusha kwa ajili ya kushiriki hafla kubwa ya uzinduzi wa Tuzo za Uhifadhi na Utalii, hafla inayokusudia kutambua na kuthamini mchango wa taasisi na watu binafsi katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwasili akiwa ameambatana na mwenyeji wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana. Hafla hii ya kihistoria imewaleta pamoja viongozi wakuu wa Serikali, wadau wa uhifadhi na utalii, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayohusika na uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya utalii endelevu.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Majaliwa alisisitiza umuhimu wa sekta ya uhifadhi na utalii kama injini muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania, huku akibainisha kuwa sekta hiyo imeendelea kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na kuchangia sehemu kubwa ya mapato ya taifa. Alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinaendelea kulindwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo.

“Mnatambua kwamba uhifadhi si kazi ya mtu mmoja au taasisi moja, bali ni jukumu letu sote kama Watanzania. Leo tunawapongeza wote waliofanya juhudi kubwa kulinda mazingira, kuhifadhi wanyamapori, na kuendeleza utalii. Hii ni heshima kubwa kwao na kwa taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alibainisha kuwa tuzo hizi ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa kuhamasisha uwajibikaji na ubunifu katika sekta ya uhifadhi na utalii. Alieleza kuwa hafla hii itasaidia kuvutia uwekezaji zaidi, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na kuendeleza juhudi za kupambana na changamoto zinazokabili sekta hiyo, kama ujangili na mabadiliko ya tabianchi.

Hafla hiyo imepambwa na burudani za asili zinazojumuisha nyimbo na ngoma za kitamaduni kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania, kuonyesha urithi wa kiutamaduni wa taifa ambalo linaongoza kwa vivutio vya kitalii barani Afrika.

Pia, viongozi waandamizi wa Serikali na wadau waliotambuliwa kwa mchango wao wamepewa nafasi ya kueleza jinsi walivyofanikiwa kuleta mabadiliko chanya katika uhifadhi na utalii. Washindi wa tuzo mbalimbali, wakiwemo wahifadhi bora, watoaji huduma bora za kitalii, na wabunifu wa miradi ya uhifadhi, wamepongezwa kwa mafanikio yao makubwa.

Tuzo za Uhifadhi na Utalii zimeibua hisia kubwa, huku washiriki wakionyesha matumaini makubwa kuwa hafla hii itakuwa chachu ya maendeleo zaidi katika sekta ya utalii. Tukio hili linatarajiwa kuleta athari chanya kwa kuongeza mwamko wa umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za taifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kinara wa utalii duniani.

Hafla hii imehitimishwa kwa chakula cha jioni cha kifahari, ambapo viongozi na wadau wamepata fursa ya kubadilishana mawazo, kuimarisha mtandao wa ushirikiano, na kuadhimisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa.

MTUHUMIWA WA “KUFUTA MADENI” YA MIKOPO AKIRI KOSA, AHUKUMIWA KIGOMA

KIGOMA, Septemba 4, 2026 — Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu Nicholaus Komba Mahitana maarufu kama Abdallah Mahimbo baad...