Na Mwandishi Wetu, Riyadh
Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, umefika nchini Saudi Arabia kushiriki katika Mkutano Mkuu wa 26 wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) unaofanyika mjini Riyadh, kuanzia wiki hii.
Akizungumza na wataalamu wa Tanzania katika kikao cha maandalizi kilichofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini Riyadh, Dkt. Abbasi alisema Tanzania iko tayari kushiriki kikamilifu katika mkutano huo muhimu unaojumuisha mawaziri, makatibu wakuu na wadau wakubwa wa utalii kutoka zaidi ya nchi 150 duniani.
“Tanzania ni mwanachama hai wa Shirika hili na ni miongoni mwa nchi wachache zinazoshiriki katika Kamati ya Utendaji ya UN Tourism, hivyo tunakuja tukiwa na sauti na mchango mahsusi katika mijadala mikubwa kuhusu mustakabali wa sekta ya utalii duniani,” alisema Dkt. Abbasi.
Aliongeza kuwa mkutano huo ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonyesha mafanikio yake katika kukuza sekta ya utalii, hususan kupitia kampeni za kimkakati kama “Tanzania Unforgettable” na utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa diplomasia ya uchumi kupitia utalii.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi, pamoja na ajenda kuu za kikao, moja ya mambo muhimu yatakayojadiliwa ni uchaguzi wa Katibu Mkuu mpya wa UN Tourism, atakayeanza kazi rasmi Januari 2026, kuchukua nafasi ya uongozi wa sasa na kuendeleza mageuzi katika sekta hiyo duniani.
Aidha, ujumbe wa Tanzania utashiriki pia katika mikutano ya kando (side events) itakayohusisha majadiliano ya uwekezaji, ubunifu, matumizi ya teknolojia katika utalii, na uendelevu wa mazingira – maeneo ambayo Tanzania imepiga hatua kubwa kwa miaka ya karibuni.
Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa Tanzania inaingia katika mkutano huo ikiwa na dhamira ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa kimataifa, kuvutia wawekezaji, na kuongeza idadi ya watalii kutoka mataifa mbalimbali, hasa kutoka Mashariki ya Kati, Asia, na Ulaya.
“Lengo letu ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kinara wa utalii wa asili na kipekee barani Afrika, tukitumia vivutio vyetu vya kimataifa kama Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, na Visiwa vya Zanzibar kama nyenzo za kiuchumi na diplomasia,” aliongeza.
Mkutano huo wa 26 wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism General Assembly) unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii, ukitoa dira mpya ya kimataifa ya kukuza utalii endelevu, ujumuishi, na unaolenga maendeleo ya watu.




No comments:
Post a Comment