Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah Hamad akitoa ufafanusi wa jambo kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda leo hii Kambarage House Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda akitia saini kitabu cha wageni leo hii Kambarage House Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuwasili.
Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika la Nyumba la Taifa, Fatma Chillo akifafanua hoja kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda wakati wa mkutano na Naibu Waziri Kambarage House Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda akizungumza na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) leo Kambarage House Jijini Dar es Salaam.Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda ametaka kuwapo mabadiliko makubwa katika nyanja zote za utoaji huduma kwa Watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa ili waweze kuleta tija kubwa kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri Pinda aliyasema hayo baada ya kufanya ziara ya siku moja kufahamu kazi zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuzungumza na Wafanyakazi wa Makao Makuu kwa niaba ya Wafanyakazi wote wa Shirika.
“Nichukue nafasi hii kuwapongezeni kwa kazi kubwa mnazozifanya kawa maendeleo ya Taifa, lakini niwachagize kuwa tunataka mabadiliko makubwa ya utoaji huduma ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa kila mmoja kufanya kazi apaswayo, mpendane, mheshimiane na mthaminiane na sisi kama Serikali tutawaunga mkono kama mlezi wenu,”amesema.
Ameutaka uongozi wa Shirika hilo kuutumia ujuzi wa Mkurugenzi Mkuu ambaye ameteuliwa akitokea katika uongozi kwenye taasisi ya sekta binafsi ili Shirika liweze kukua kwa kasi kibiashara kama linavyotakiwa.
“Fanyeni sensa ya kutambua nyumba zenu nchi nzima na mpitie mikataba yenu na wapangaji kuwe na utafiti wa mahitaji ya nyumba maeneo mbalimbali nchini kuna wapangaji wenu wanawapangisha watu wengine kwa fedha nyingi huku wakilipa NHC fedha kidogo, hili siyo jambo jema,”amesema.
Ametaka kuongezwa kasi ya kudai kodi kwa wadaiwa sugu wa Shirika hilo na kwa zile taasisi za Serikali ambazo nazo ni wadaiwa sugu orodha yao iwasilishwe Wizara ya Ardhi ili kusudi Wizara isaidie kudai kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Amependekeza pia uanzishwaji wa vijiji vya mfano vyenye kuleta tija lakini vyenye kuwasaidia Watanzania waliopo pembezoni mwa nchi pamoja na kwamba Shirika linaendeshwa kibiashara.
Ameelekeza ushirikishwaji wa Wafanyakazi wote kwa Menejimenti inapoamua kuyabuni mawazo ya maendeleo “Mimi nataka ustawi wa watumishi pia muwape malengo, watekeleze majukumu yao wanayotakiwa kuyatekeleza, lakini pia wapewe motisha ya kutosha ili kuwa na tija kwa nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah alielezea umuhimu wa Serikali kulisaidia Shirika ili kuhakikisha kwamba Watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora.
“Kadri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka, uhitaji wa makazi unaongezeka pia. Idadi ya Watanzania inaongezeka kwa asilimia 3.1 kila mwaka ambayo inapelekea kuzidi kwa upungufu wa nyumba za makazi nchini. Hadi sasa kuna uhitaji wa nyumba milioni tatu na laki nane za makazi nchini,” amesema Hamad.
Hamad amesema kuwa miaka ijayo asilimia 48 ya Watanzania wote watakuwa wanaishi mijini hivyo kuna haja kubwa ya kuongeza idadi ya makazi katika miji na nchini kwa ujumla.
Amesema kuwa Serikali haina budi kuunga mkono juhudi za Shirika katika uendelezaji wa miliki kwani kwa kupitia utekelezaji wa shughuli tofauti za Shirika kuna manufaa tofauti kama vile upatikanaji wa ajira kwa Watanzania, kuongezeka kwa pato la Shirika kupitia uuzaji na upangishaji wa nyumba na taasisi nyinginezo kama vila Tanesco na Mamlaka za maji na pia inachangia kwa kiasi kikubwa katika uendelezaji wa viwanda nchini kwani ujenzi wa nyumba unajumuisha matumizi ya bidhaa za ujenzi kama vile nondo, mabati, saruji n.k
“Riba kubwa zinazotozwa na mabenki pindi wananchi wanapochukua mikopo ya ujenzi asilimia 14 hadi 20 pamoja uwezo mdogo wa kiuchumi wa Watanzania wengi ni mojawapo kati ya changamoto zinazozuiya ukuaji wa sekta ya nyumba,” alisema Hamad.
Alieleza kwamba idadi kubwa ya Watanzania wana vipato vidogo hivyo, riba ya asilimia 14 hadi 20 ni kubwa kwao pindi wanapochukua mikopo benki.
Pia hakusita kueleza jinsi Shirika lilivyomudu kuwapatia wanunuzi wake mikopo ya nyumba kwa riba ya asilimia 9 kwa Watanzania wanaonunua nyumba Iyumbu, Dodoma.
No comments:
Post a Comment