Friday, April 27, 2018

MTOTO WA MIEZI TISA AFA AJALINI BAADA YA BASI LA POLISI, NOAH KUGONGANA USO KWA USO MOROGORO


 Pichani ni  gari aina ya Noah iliyokuwa ikitokea Kizuka Ngerengere kuelekea Morogoro Mjini ikiwa imegongana uso kwa uso na basi la jeshi la polisi lililokuwa likitokea mkoani Dodoma kuelekea Dar es Salaam eneo la Mikese Maseyu mkoani Morogoro.
Pichani ni  Baadhi ya Askari wa JWTZ na Jeshi la Polisi wakishiriki kutoa msaada kwa majeruhi wa ajali ya gari aina ya Noah iliyokuwa ikitokea Kizuka Ngerengere kuelekea Morogoro Mjini ikiwa imegongana uso kwa uso na basi la jeshi la polisi lililokuwa likitokea mkoani Dodoma kuelekea Dar es Salaam eneo la Mikese Maseyu mkoani Morogoro. 
 Baadhi ya Askari wa JWTZ wakitoa msaada kwa majeruhi mara baada ya ajali hiyo kutokea.*Dereva wa Noah naye afariki, askari JWTZ, Polisi wajeruhiwa

Na Ripota Wetu,Morogoro 

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Morogoro Ulrich Matei amethibitha kufariki dunia kwa watu wawili akiwamo mtoto wa miezi tisa Amina Hassan baada ya kutokea kwa ajali iliyohusisha gari ndogo aina ya noah pamoja na basi la Jeshi la Polisi.

Akizungumza kwa njia ya simu na Michuzi Blog jioni hii kuhusu ajali hiyo Kamanda Matei amesema imetokea saa saba mchana eneo la Mikese Maseyu mkoani humo, ambapo Noah iliyokuwa ikitokea Kizuka Ngerengere kuelekea Morogoro Mjini kugongana uso kwa uso na basi hilo ambalo lilikuwa likitokea mkoani Dodoma kuelekea Dar es Salaam.

Amefafanua mbali ya kufa kwa mtoto huyo dereva wa Noah hiyo iliyopata ajali ambaye amemtaja kwa jina la Zimbao Cornel huku akielezea kujeruhiwa kwa askari Polisi wanne na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) nao wanne na wanaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

Alipoulizwa kuhusu idadi ya watu waliokuwa kwenye Noah amesema bado haijathibitika walikuwa wangapi lakini wanaendelea kufuatilia na kisha watatoa taarifa kamili.

Kuhusu hali za majeruhi Kamanda Matei amesema wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika, hivyo kikubwa ni kuwaombea ili wapone haraka na kurejea kwenye ujenzi wa nchi.

Kabla ya kuthibitishwa na kamanda kuhusu ajali hiyo, Ripota Wetu ameshuhudia gari hiyo ya Noah ikiwa imeharibika vibaya na baada ya ajali kutokea waliopoteza maisha na majeruhi walikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Kwa upande wa Muuguzi wa zamu kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoani Edwine Damas amekiri kupokea mwili wa mtoto huyo na majeruhi na wanaendelea kuwapatia matibabu.



No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...