Diwani na Babu
*AOA WANAWAKE SITA, AJENGA SHULE KUSOMESHA FAMILIA YAKE
KWA mara ya kwanza niliposikia habari za mzee Nterege Nyigana Mutari ana umri wa miaka 103, ana watoto 57, wajukuu 200 na vitukuu 70, sikuamini.
Nilijiuliza maswali mengi moja likiwa ni kwanini mzee huyo asiwemo katika kitabu cha maajabu ya dunia? Hiki ni kitabu ambacho huchapishwa kila mwaka kikiwa na mkusanyiko wa rekodi za dunia kuhusu mafanikio ya binadamu pamoja na maajabu mbalimbali.
Kuishi miaka 103 na kuwa na watoto 57 sio jambo dogo, watoto ambao nao wanakuletea wajukuu 200, na wajukuu nao wanakuletea vitukuu 70.
Na kama hiyo haitoshi, unaamua kujenga shule ili wapate elimu bora, tena katika shule hiyo yenye wanafunzi 744, wanafunzi 200 wanatoka katika familia yake, wakiwemo wajukuu na vitukuu. Sasa mzee kama huyu, kwanini asiwemo katika maajabu ya dunia?
Baada ya kufikiria mambo mengi niliamua kumtafuta mzee Nterege ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Nyamaitagi, kijiji cha Nyamakobiti, kata ya Majimoto Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Mzee huyu mcheshi ambaye ni wa kabila la Wangoreme anaishi umbali wa kilometa 70 kutoka makao makuu ya wilaya ya Serengeti, mjini Mgumu.
Historia ya Mzee huyo imejaa mengi yakiwemo machungu na raha, lakini kwa upande wake anasema vikwazo katika maisha ni jambo la kawaida.
“Nina miaka 103, wajukuu zaidi ya 200 na vitukuu zaidi ya 70, nilizaa watoto 57 lakini ninachoweza kuieleza jamii ni kwamba watoto wangu nimeamua kuwapa elimu bora kwa kuwa elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu hapa duniani,” anasema Nterege.
Maisha yake
Nterege alizaliwa mwaka 1908 lakini akajulikana kwa jina la "Reterenge’’, jina ambalo anasema alipewa na daktari raia wa Ujerumani.
Anasema alizaliwa katika eneo la Kyehonda -Kimeli ambalo kwa sasa ni eneo la kijiji cha Nyamutita na kwamba wakati huo baba yake alikuwa na wake wawili.
“Kwa upande wa mama yangu tulizaliwa wawili tu, mimi na dada yangu ambaye anaitwa Nyakimaiga, mama yetu alikuwa mke wa pili wa baba,” anasema Nterege.
Anasema mwaka 1918 baada ya baba yake kufariki dunia, ndugu wa baba yake walichukua mifugo yote iliyoachwa na baba yake wakiwemo Ng’ombe zaidi ya 100, na kuwanyang’anya nyumba waliyokuwa wakiishi na mama yao.
“Walitufukuza pamoja na mama kwa kuwa alikuwa mke mdogo wa marehemu baba, walisema kuwa mama yetu wa kambo ambaye alikuwa mke mkubwa ndio alikuwa na haki ya kupata kila kitu. Kuanzia hapo tulianza kuishi kwa shida.”
Anasema baada ya tukio hilo alianza maisha ya kujitegemea ambayo yalimfanya ashindwe kwenda shule na kujikita katika kilimo na wakati mwingine kufanya kazi ya kuchunga mifugo ya watu mbalimbali ili kupata fedha za kuweza kujikimu.
“Mwaka 1937 nilioa mke wa kwanza, Wansama Moremi ambaye kwa sasa ni marehemu nilihamia eneo la Nyamakobiti kuanza maisha mapya ya ndoa…, mke wangu nilimtolea maali ya Ng’ombe kumi niliowanunua baada ya kuuza Ulezi niliolima kati ya mwaka 1935 na 1936,” anasema Nterege.
Wazo la kuwa na familia kubwa
Anasema katika maisha yake mapya baadhi ya mambo yaliyokuwa yanamsumbua, ilikuwa ni jinsi gani angeweza kupata watoto wengi kwa kuwa alizaliwa yeye na dada yake tu.
“Wakati ule kuwa na familia au ukoo mkubwa kilikuwa kitu cha heshima katika mila zetu,” anasema Nterege.
Pia, anasema ukubwa wa familia ulikuwa muhimu ili kuweza kupambana na vitendo vya wizi wa mifugo ambapo mara kwa mara kuliibuka mapigano ya kikabila kati ya kabila lake na Wakulya na Wangoreme.
“Maisha ni mapambano. Nilianza kufanya biashara ya mifugo mwaka 1940 nikishirikiana na Chifu Makongoro wa Waikizu. Nilipata Ng’ombe 800 wa kwangu mwenyewe ila kwa sasa wamebaki 220 baada ya kuwapa watoto wangu kwa ajili ya kuanza maiasha yao ya kujitegemea,”
Kuoa
Akizungumza wanawake aliowaoa Nterege anasema,
“Nilioa wanawake saba lakini niliodumu nao ni sita, wanawake hao sita walizaa watoto 57, ila watoto waliopo hai ni 37,”.
Anaongeza, “Watoto wangu 20 walifariki kutokana na kwamba wakati huo vituo vya kutoa huduma ya afya vilikuwa mbali,”.
Anasema kuwa ana wajukuu zaidi ya 200, vitukuu zaidi ya 70 na anafafanua ,” Wengine siwatambui hata kwa majina,”.
Anasema mwaka 1937 alimuoa mke wake wa kwanza, Wansama Moremi, Gasawa Mayengo (1939),Mandala mwita (1953), Nyamhanga Nyamani (1963), Odela Osole (1969), Nyambura Paka (1965) na Mkami Myangosira (1974) ambaye waliachana bila kuzaa mtoto.
Anasema mpaka sasa wake zake walio hai ni wawili ambao anaishi nao na anawataja kuwa ni Nyamhanga Nyamani na Nyambura Paka.
Nterege anasema jambo kubwa analojivunia ni kumwona mtoto wake wa mwisho, Julius akisoma elimu ya sekondari ambapo alimaliza mwaka juzi.
Anasema kaka yake Julius anayeitwa Nyamanko alimaliza sekondari mwaka 1990, na wajukuu zake watano nao wamemaliza elimu ya sekondari ambao ni Gesile(2003), Bonifasi (2009), Nyakimaiga (2011).
“Kuna mmoja anaitwa Nyamitari bado yupo kidato cha tatu kwenye shule ya Sekondari ya Busawe, shule ambayo nilichangia ujenzi wake,” anaeleza kwa kujivunia kwa kitendo chake cha kuchangia maendeleo ya jamiii.
Anasema watoto wake 19 ambao wako hai ni wa kike na wa kiume 18. Mtoto wake wa kwanza anaitwa Mayengo na alizaliwa mwaka 1942.
Kujenga shule
Mzee Nterege ambaye bado ana kumbukumbu ya mambo mengi licha ya kuwa na umri mkubwa anasema kuwa mwaka 1988 baada ya kuona wajukuu zake wakipata usumbufu wa kwenda shule zilizokuwa vijiji vya mbali, aliamua kubuni wazo la kuanzisha shule ya msingi kuondoa usumbufu huo.
Anasema alianza ujenzi wa shule kwa kutumia magari yake kubeba mchanga na kokoto huku akiwahamasisha wakazi wa kijiji hicho kuchangia ujenzi.
“Ilikuwa ngumu kuwashawishi kwa kuwa kipindi hicho watu walikuwa hawapendi kuelezwa habari za kuchangia fedha kwa ajili ya jambo fulani.
Anasema kwamba mwaka 1990 alifanikiwa kumaliza ujenzi wa jengo la utawala kwa nguvu zake pamoja na wananchi.
“Licha ya kuwa mimi sikusoma niliamua kujenga shule ili wajukuu zangu wapate elimu. Elimu ndiyo kila kitu. Huwezi kufanikiwa katika maisha ya sasa bila elimu. Niliona wajukuu zangu wasiposoma watakuwa watumwa na tegemezi,” anaeleza Nterege.
Anasema mwaka 1991 shule hiyo ya msingi iliyopewa jina la Nayamakobiti ilifunguliwa kwa usajili namba PS 0904080 ikiwa na eneo la ukubwa wa Hekta 9.5.
“Shule hii niliamua kuiita jina la kijiji badala ya jina langu kwa kuwa sikutaka sifa katika suala hili, mtu unatakiwa usifiwe ukiwa umekufa si ukiwa hai,” anasema Nterege.
Mkuu wa shule hiyo anasemaje
Akizungumzia historia ya shule hiyo mkuu wa shule hiyo, Machumbe Mairo anasema kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya shule hiyo bila kumtaja mzee Nterege.
Anasema shule hiyo ina wanafunzi 744 na anafafanua kwamba pamoja na changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na uhaba wa walimu.
Pamoja na matatizo hayo alisema inafanya vizuri ambapo wanafunzi wengi hufaulu kuendelea kidato cha kwanza.
“Katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010 shule hii imeweza kufaulisha wanafunzi 122 kwenda sekondari, wasichana wakiwa ni 41 na 81 wakiwa ni wavulana,” anasema Mairo.
Anasema wanafunzi 200 wa shule hiyo kati ya wanafunzi 744 wanatokea katika familia ya mzee Nterenge wa kiwemo wajukuu na vitukuu.
“Familia yake ni kubwa kweli yaani hapa kijijini wako wengi. Ukienda vijiji jirani pia wapo,” anasema.
Imeandikwa na Renatus Masuguliko. SOURCE: MWANANCHI.