Saturday, April 01, 2006

Kutandawazishwa kusituondolee utu wetu

SIPENDI kusikia na wala kuona mambo yanavyoendelea katika jamii zetu hapa Afrika na hasa Tanzania licha ya kwamba katika baadhi ya mambo tunajitahidi kujikongoja angalau tuonekane nasi ni watu.

Nasema sipendi kwa sababu nyingi, mojawapo ikiwa ni kutojiamini wenyewe (Waafrika au Wabongo) kufanya mambo hadi wanapokuja watu weupe ndipo tunapoona kwamba eti ndiyo tumefanya vizuri sana.

Hebu angalia, kwa mfano tunaambiwa kuwa uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki kwa Afrika mpaka Ulaya na Marekani waseme au waangalie, kwani demokrasia maanake nini?

Hapa kwetu, wakati ule wa uchaguzi hawa watu weupe kutoka Marekani na Uingereza walijaribu kutuchanganya kidogo, taasisi ya NDI ikasema haukuwa huru, Jumuiya ya Ulaya ikasema haukuwa huru, lakini baadaye ikabadilika na kusema ulikuwa huru. Bahati nzuri hatukuyumba sana.

Waafrika tumekuwa tukitaabika na tatizo la kufutiwa lugha zetu, tuna lugha za kubahatisha, lugha zetu tulizo nazo sasa ni mchanganyiko tu wa zile zetu asilia kabisa na hizi za dunia ya sasa.

Tunajaribu kuumba aina mpya za lugha na aina mpya za utamaduni na hata mifumo 'feki' ya kiutawala popote pale tunapokuwa.

Tunao wasomi wa kutosha, lakini nao bahati mbaya wameshaingizwa katika utandawazi, yaani wametandawazishwa na sasa mawazo yao yamekaa kimshiko mshiko. Wanawaza kuandika 'paper' ili kuweza kujipatia mlo.

Vyuo vikuu vilikuwa chem chem ya fikra pevu, komavu au huru, zilizopikwa zikapikika na ilikuwa linapotoka wazo ndani ya jamii kama hiyo linaogopwa linafanyiwa kazi na linaaminika kwa sasa haya hakuna! Hakuna fikra tena za kiuanamapinduzi!

Hali hii imefanya baadhi ya watu kukata tamaa na kujiona na kusema kama unataka kufa maskini au kupata kichaa, basi jaribu kubadilisha mifumo ya 'Kiafrika', kisha uirudishe katika mstari.

Kule Marekani wenzetu matokeo ya tatizo hili yalizaa Unegro, Blues, Jazz, Hip-hop na tamaduni za ajabu ajabu zisizokuwa na mwanzo wala mwisho.

Miongoni mwetu weusi tunavyo visima vya busara au wanaharakati kama kina vile, Sylvester Williams, Marcus Garvey, George Padmore, CLR James, Cesarie, Stokely Carmichael (Kwame Toure) na Frantz Fanon.

Lakini sisi tunakwenda kinyume kabisa na wenzetu tunajaribu kadri tuwezavyo tuonekane Wazungu zaidi kwa kuzungumza Kiingereza “sanifu” au Kifaransa "fasaha" au Kispaniola "fasaha" au Kireno "fasaha".

Cha kushangaza zaidi baadhi yetu wanadiriki kujiita 'wazungumzaji wazuri au fasaha wa Kiingereza au wa Kifaransa wakati wao ni Waafrika wanazo lugha zao na wana kila la kwao.

Lakini, tujiulize tunavyofanya hivi tuseme kujifanya Wazungu zaidi kuliko wazungu wenyewe ndiyo maana nao wanatudharau kupita kiasi, wanafanya kila wanachojua kuhakikisha sisi tunakua kama wao na tunajisahau kabisa kama tuna nafsi.

Hatuwezi kuwa washiriki wazuri wa uamsho wa kuitetea Afrika mpaka tutakapoweza kwanza kujitambua sisi ni nani na majukumu yetu ni yapi katika kuendeleza vizazi vyetu.

Ni lazima kwanza tuangalie katika historia ya kisiasa, kifikra na kiutamaduni.

8 comments:

Christian Bwaya said...

Nimekuwa nikijiuliza kwa nini huyu bwana (wewe) hafungui blogu? Hivi ina maana Makene hajamshirikisha jambo hili?
Utaona furaha ya kukutana na wewe katika baraza hili ni kiwango gani. Hongera sana.
Makala hii nimeisoma gazetini. Imenivutia. Imetulia kama nyingine zilizopita. Nadhani ujio wako ni changamoto kwa waandishi wengine.

Vempin Media Tanzania said...

Ahsante sana muzee nashukuru si unajua tena kisima hiki cha maarifa kimenifurahisha kwa jinsi ambavyo watu wanatoa mawazo, michango yao na marekebisho pale panapotakiwa.

Laiti kama ningelijua mapema ningelikuwa nimejitosa toa muda huo na bila shaka ningekuwa nimefaidika zaidi na fikira za watu makini wa mtandaoni.!

boniphace said...

Bwaya alikuwa anasoma kwanza template na sasa unaona amekuja kwa kasi sana. Na wewe Bwaya mbona hatukusomi sasa, mbona kimya hivyo.

Jeff Msangi said...

Charahani,
Ni muhimu sana tukapambana kufuta dhambi waliofanya wakoloni ya kutuambia chetu hakifai,kitupwe na chao ndio kinafaa.Mimi huita gonjwa hili kansa ya fikra.Ni ugonjwa mbaya sana na unaambukiza kwa kasi sana.
Tufanye nini basi?Tukumbushane na kuwezeshana kifikra kama hivi.Tuwafikie na wale wote walio chini na juu yetu ili nao wawafikie wenzao,hususani kizazi kipya.Nia ni kujenga msingi mpya na imara.Kazi nzuri

Vempin Media Tanzania said...

Msangi,

Hicho unachokisema ni barabara maana bila ya kuondoa hii kansa ya fikra kweli tutaendelea kujidanganya kwa karne nyingi zijazo na hatutafanikiwa. Cha muhimu ni kuamka sasa na kupandikiza moyo wa kujiamini, moyo wa kujituma, moyo wa kutoogopa kushindwa bila shaka nadhani tutafika mbali.

Ndesanjo Macha said...

Tatizo unalozungumzia hapa Charahani ni msingi wa matatizo yetu. Huwezi kujua una tatizo gani iwapo fikra za kukuwezesha kujua kuwa una tatizo zimetekwa na zimepondwapondwa na itikadi zinazokufanya uamini kuwa huwezi na kuwa wanaoweza ni wengine ambao unawaabudu. Waafrika tuna ugonjwa mbaya sana. Kansa ya fikra na nafsi. Ndio maana katika majibu yote tutakayopata lazima yajumuishe elimu ili kusafisha fikra na nguvu zetu kubwa lazima zilenge kwa watoto. Ndio maana kuna umuhimu mkubwa wa kuandika vitabu vya watoto. Kama tunataka kumaliza utumwa wa kimwili na akili tulio nao leo lazima tuwekeze kwa vizazi vijavyo kwa kuelimisha watoto. Tukiacha watoto waelimishwe na sinema za hollywood, nyimbo zisizo na mbele wala nyuma, magazeti yanayopumbaza badala ya kuelimisha, wazazi wanaowanunulia watoto midoli ya bunduki au midoli ya kizungu (kama vile midoli ikiwa mieusi inakuwa sio midoli mizuri...watoto hao wakija kujichubua tunalalamika!).

Kuna mahali umesema jambo ambalo sijakuelewa, naomba ufafanuzi. Umesema:
"Unegro, Blues, Jazz, Hip-hop na tamaduni za ajabu ajabu zisizokuwa na mwanzo wala mwisho."

Unamaanisha nini?

Christian Bwaya said...

Makene, mbona unakuwa kama hujui! Umeme unakatika sana Bongo! Mgao kwenda mbele, hujapata habari? Afu so ni kwamba ukirudi, linajitokeza suala la kuchangia gharama za Cafee...nini matokeo yake. Kimya!
Baada ya mwezi huu ntakuwa nimeondolewa "spidi gavana" huenda na umeme utakuwa haukatiki tena(tumeahidiwa na Kasi Mpya) "zeafo" ntakuwa hewani vya kutosha.

Vempin Media Tanzania said...

Ndesanjo

Kwa :"Unegro, Blues, Jazz, Hip-hop na tamaduni za ajabu ajabu zisizokuwa na mwanzo wala mwisho. Nilikuwa nikimaanisha kuwa wenzetu angalau wamepata cha kujivunia kwamba ule mkutaniko wa mwafrika, msaniola, muzungu, mchina na wengine kibao umezaa tamaduni au tuseme vitu hivyo nilivyoamua kuviita vya ajabu ajabu japo wamefaidika. Hiyo ndo maana yangu!

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...