Friday, April 28, 2006

Kijiji cha Mwananchi kimewaka moto

Haya tena wanablogu wenzangu kumekucha tena safari hii nawaleteeni wanablogu wawili matata kweli kweli. Wa kwanza huyu ni bosi wangu katika masuala ya spoti afahamika sana kama Angetile Osiah au Mzee wa Ujerumani, amebobea katika fani hii wengine hupenda kumwita kisima cha fikra michezoni, nadhani hata kuwa mgeni kwenu waweza kumtembelea kwa kubofya hapa. Na mwingine ni mwanamama huyu, Mzanzibari ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, ni hazina tosha ya fikra za kisiasa na kijamii, aweza kukusisimua kwa kuipata vyema historia ya Zanzibar na maeneo mengine, jinale Hawra Shamte, waweza kumpata kwa kubonya hapa. Haya mambo yanazidi kuwa mambo bloguni.

Tuesday, April 25, 2006

Ujambazi Ubungo ulipangwa ndani ya NMB

INAWEZEKANA kipindi kifupi kijacho tukawa tunavuna matunda adimu ya uhuru wa taifa letu ambalo wazee wetu wamelisotea kwa kutaabika, kuunguzwa, kuumizwa na kunyanyasika.

Nasema inawezekana hivyo kwa dalili moja au mbili zinazojionyesha katika serikali yetu ya awamu ya nne. Kwanza ni kwa sababu ya ujasiri wa viongozi wa sasa, lakini pili kwa sababu ya kuthubutu kwao kutenda mambo.

Wameingia madarakani katika kipindi ambacho baadhi ya polisi wamekuwa majambazi, madaktari kadhaa wamekuwa wauaji, walimu wengi wamekuwa wafelishaji, wahandisi lukuki wamekuwa wabomoaji, wazuia rushwa kuwa walaji, walinzi wa amani kuwa wachafuzi na mambo mengi.

Kipindi ambacho mwizi anasifiwa kwa ujemedari, muadilifu anadharauliwa kwa moyo wake, mhalifu anasujudiwa anaonekana shujaa asiye mhalifu anaonekana mbumbumbu asiyefaa kabisa.

Wengi wetu tumekuwa tukivuna machungu ya uhuru, pengine kutokana na utamaduni huu wa ulafi, hofu, kulindana na kuogopana kulikokuwapo na au kuliopo katika mikono ya watawala.

Tumekuwa mabawabu na washuhudiaji tu wa utajiri wa wenzetu wanabeba kila kilicho chetu wanapeleka katika mataifa yao, sisi wanatuachia madhila, wanatuachia mashimo, wanatuachia balaa. Mbaya zaidi wanabeba mpaka akili zetu, tunabakia na akili za kushikiwa.

Mengi yamekua yakifanyika hivyo huku wanaofanya hivyo wakitumia zaidi 'ujomba' wa kisiasa na wakati mwingine kujificha katika kivuli cha utaifa.

Kitu ambacho ni kinyume kabisa na ninavyoufahamu utaifa unaotokana na shauku ya kujiambatanisha na kundi unaloshirikiana nalo historia na uzoefu.

Hisia hizi hutokana mara nyingi na utashi wa makundi yaliyodharauliwa kujikomboa kutoka katika minyororo ya ukandamizaji na kutamani kunufaika na matunda ya uhuru.

Hisia hizi zimekuwa zikipotea na mara chache sana kujirejesha. Zinapotea kwa sababu wapo wajanja wanatujazia ujinga kwamba huu ni wakati wa dunia huria na sisi kujisahau kabisa na kuiacha mipaka yetu wazi bila ulinzi wa kutosha matokeo yake ni kuletewa madhila mengi lakini leo nitazungumzia hili la ujambazi.

Kwao wenzetu pamoja na kwamba wapo hulia lakini wapo makini kuilinda mipaka yao, kuwajaza watu wao utaifa na kuwaimarisha kisaikolojia ili wanapokutana na masuala yasiyoendana na utaifa wao hupinga na kushirikiana kwa namna zote na kuondokana nayo.

Hebu kumbuka matukio mengi ya mabaya ya kihalifu likiwamo hili la juzi pale Ubungo la ujambazi ni dhahiri yanatokana na kuyeyuka na pengine kushuka kwa ari ya utaifa ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuwaribisha na kuwatunza raia wasio wema wa nchi jirani.

Imeripotiwa mara kadhaa kuwa wanaopora fedha mara nyingi huwa si watanzania si kwa muonekano bali hata kwa lafudhi. Wengi wanatoka nchi jirani za Kenya, Burundi na au Rwanda, sasa hapa kunakuwa na faida gani ya kuzembea?

Na mara zote hizo wanazopora wanapotea na hawapatikani na hata fedha wanazopora hazipatikani hii tafsiri yake nini? Ni kwamba tunawapokea na kuwalea na kuwatunza humu ndani ya nyumba zetu, wengine miongoni mwetu kwa posho kidogo sana, badala ya kuwashughulikia.

Aina hii ya uzembe itatupeleka pabaya tutakuwa hata hatuwezi kutembea kwa amani kwani iwapo sasa hivi upitaji wa baadhi ya maeneo ni matatizo je tunavyoendelea 'kuwabeba' wahalifu tunategemea nini?

Nyingine inatokana tu na ubinafsi uliosheheni miongoni mwetu kwani haiwezekani kabisa wale waliopora pesa na kuua watu wakawa wamejiamulia tu, ni mpango uliosukwa aidha ndani ya NMB au BoT.

Hivyo cha msingi ni kuhakikisha wale wote waliosuka mchoro wa uporaji wa pesa hizo wakakamatwa na kufikishwa panapohusika kama Rais Jakaya Kikwete alivyoagiza kwani wote ni wauaji.

Jitihada zilizoonekana juzi Ubungo wakati majambazi yalipopora Sh 150 milioni zinatakiwa kupongezwa na kutiwa nguvu kwa kuwa sasa kama nilivyotangulia kusema hapo juu, zimeonyesha ipo serikali.

Hatujazoea kuona helikopta ikifanya doria, wala kusikia risasi zikimiminwa mtaani kama cheche za moto majumbani kwetu, lakini uzembe wetu (raia) ndiyo unaosababisha yote haya.

Kwa hiyo uchungu wetu kwa taifa letu, kutopenda kuwatunza wahalifu kutatufanya tujiokoe na mengi yanayofanana na haya yanayotokea sasa, tusiogope kuwaumbua wahalifu wanapopanga mikakati ya uhalifu.

Wednesday, April 19, 2006

Huyu sijui ni Nyarubanja au vipi?

Haya tena kumekucha uwanja wa blogu unazidi kuvamiwa tena kwa nguvu ya ajabu, tunaye mwanablogu mpya kutoka hapa katika kijiji chetu cha Mwananchi, huyu si mwingine ni Midraji Ibrahimu, huyu kwa wasiyo mfahamu alishiriki kwa kiasi kikubwa kumpigia debe Mzee wa Standard and speed, lakini bahati mbaya akabwagwa katika kambi yake nyingine ya Mzee Malecela, waweza kumpata kwa kutembelea hapa

Saturday, April 15, 2006

Kwanini rushwa haiwezi kuondoka?

KWA kipindi cha karibu miezi mitatu sasa suala kubwa linalotikisa katika kila pembe za Afrika limekuwa ni rushwa. Tanzania Rushwa. Kenya Rushwa. Uganda hivyo hivyo na kwingineko kwingi Afrika.

Vyombo vya habari, jumuiya ya Wanadiplomasia na jumuiya za hiyari katika maeneo yote hayo zimekuwa zikijaribu kupigia kelele suala hilo kwa uwezo wao wote, lakini wapi.

Kote huko rushwa inakuwa ni kwa kiasi kikubwa inatokea katika ofisi za umma. Wapo wanaodhani kuwa watumishi wa umma wanakula rushwa sababu wanalipwa kidogo, lakini kwa upande mwingine hoja hii inaonekana kulemewa.

Rushwa inakuja kwa aina nyingi, ya kwanza ikiwa utoaji "kitu kidogo"; Upendeleo kwa kuweza kupatiwa nafasi, huku wanaostahili wakiachwa, ukabila au rushwa ya ngono.

Aibu gani hii! Bila shaka siku ambapo rushwa itaondoka nadhani siku hiyo hiyo ndiyo itakuwa mwisho wa umasikini, vita, Ukimwi, uhalifu n.k. Hata hivyo habari mbaya ni kwamba suala hili hadi sasa limeshindikana.

Kule Kenya serikali ya Mwai kibaki imepata kashfa ya kula mamilioni ya pesa ya walipa kodi wa Kenya. Maafisa wa ngazi za juu wa serikali hiyo, wamegundua namna ya kutafuna pesa kwa staili ya kisasa kwa kutengeneza makampuni bandia kama ya Anglo Leasing.

Siri ambayo imejitokeza ni kuwa katika kashfa hizo, viongozi wa serikali wamehusika kwa kuwekeza katika makampuni kwa kuficha utambulisho wao.

Huko Zambia, Rais mstaafu Fredrick Chiluba anakabiliana na mashitaka ya rushwa anayodaiwa kuyatenda akiwa madarakani.

Kwetu Tanzania vita dhidi ya rushwa imeendelea lakini kwa staili tofauti si kama ile ya Kenya. Serikali imetangaza rasmi kuanza kupitia upya mikataba ya kuchimba madini eneo mojawapo linalolalamikiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa.

Akitangaza haya wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete akiwa ziarani Gaborone, Botswana, alisema serikali yake itaongeza kasi ya kupambana na rushwa na jambo la kwanza ambalo imelifanya ni kuangalia upya mikataba mbalimbali iliyoingiwa kwa sababu, ndio chimbuko la rushwa kubwa ya kujineemesha.

Alisema tayari Baraza la Mawaziri limeanza kulizungumza suala hilo na kuangalia namna ya kupitia mikataba ya kuchimba madini na ili sekta hiyo iweze kunufaisha Watanzania pia. Na siyo kwa upande huo peke yake bali maeneo yote yanayohusishwa na rushwa.

Hatuwezi kufanana na Kenya, Lakini hata hapa kwetu kama ukweli utasemwa na haki itatendeka, basi wengi wa wale waliopo madarakani na walijificha katika kivuli cha uadilifu, watajikuta katika orodha ya aibu.

Kwamba, kama itakuwa ni suala la wanasiasa kuumbuana. Basi ni afadhali kusubiri kizazi kingine cha wanasiasa.

Jambo liletalo huzuni ni kwamba, kama 'mapapa' wa rushwa hawaondolewi, kama inavyojulikana, mamilionea watarajiwa wanaopata utajiri kwa njia za rushwa hawatajifunza wala kupata somo lolote. Wanalindwa kama vile wamekuwa miungu watu. Jambo jingine kubwa ni 'kuabudu' rushwa ambako kumo ndani ya bongo za watu. Kulijejenga hivyo na kutaendelea kuwa hivyo.

Kwa maana hiyo kutokana na mtindo huu, vijana masikini waliotoka vijijini kwa wazazi makabwela na hata kama wakiwa na vijipesa kidogo, wanaoingia katika ofisi za umma watalazimika kufuata nyayo za watangulizi wao ambao wanachota pesa za umma na kutokomea na hawaulizwi.

Rushwa haitatokomea kama hatutaachana na na utamaduni wa kutoa kitu kidogo kama ahsante. Rushwa kwa Afrika imekuwa kama ndiyo utamaduni na imekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

Ni lazima pia mtindo wa kuwaabudu na kuwasifia waliotajirika kwa kuiba mali za umma au za matajiri wao uachwe, ionekane kama dhambi isiyo mfano, tuwafundishe watoto wetu kuwa utajiri unatokana na kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika na si wizi wa mali ya umma na si vinginevyo na tujenge utamaduni huo kweli.

Friday, April 07, 2006

Mzee wa fikra pevu atinga mtandaoni

Haya tena kumekucha nawaleteeni mwanablogu mwingine ambaye anatoka katika hiki kijiji chetu cha Mwananchi kama anavyopenda kutuita bwana Mwaipopo. Si mwingine bali ni Absalom Kibanda, ambaye nadhani wengi mnamfahamu. Yeye si mgeni sana katika anga hizi, lakini ameamua kuibuka tena.

Kwa wasiomfahamu huyu ni mtu mmoja makini katika uchambuzi wa masuala ya kisiasa, kijamii na kitaaluma. Pamoja na hayo yote pia ni mwanamichezo matata sana kwa hiyo pia masuala ya michezo hayamsumbui hata kidogo. Makene, Ndesanjo, Reginald, Mpoki na wengineo wengi wanamfahamu hivyo namleta kwenu.

Anuani yake ni absalomkibanda.blogspot.com. Mtaniwia radhi masuala ya kublogu bado yananipiga chenga sijaweza kulink moja kwa moja hivyo welcome

Wednesday, April 05, 2006

Huu ni ustawi au ubeberu wa kiutamaduni?

KAMA kijana naweza kujiita wa makamu hivi sasa, niliyekulia katika mazingira ya utanzania halisi yale ya kutaabika, kuhangaika, kuvuja jasho na kupatikana na kila aina ya madhila.

Mazingira yaliyojikita katika utamaduni wa kushangaza kidogo ambayo kila kitu, kuanzia watu hadi wanyama kuheshimu wakubwa.

Kwetu sisi 'shikamoo' au salamu ya kawaida basi inaweza ikatawanyika kuanzia na kusalimia hadi mifugo, wajomba, shangazi mababu na hata kukumbushana mambo ya miaka iliyopita.

Salamu hizi mara nyingi huendana na kushikana mikono na hata wakati mwingine kukumbatiana.

Hapa jijini Dar es Salaam ni jambo la kawaida kabisa watu kupishana bila hata kusemezana hata neno moja na kisha kudai au kudhani wamesalimiana.

Na inapokuja kwa watoto ndiyo mbaya zaidi sababu wengi hawana hata habari hata kama wakubwa wanapita, wawapo kwenye daladala wanataka wao ndiyo wapishwe na anayethubutu kuwagusa huibuka na maneno ya kila aina huku wakisaidiwa na 'wanaharakati wa haki za watoto.

Bila shaka wazee waliopoteza uhai wao miaka ya mwanzoni mwa 1970 wangefufuka leo hii wangelipata taabu kubwa kuweza kumeza mabadiliko ya tamaduni zilivyo sasa.

Yawezekana kabisa hii inatokana na ujio wa wakoloni waliokuja kwa staili tofauti lakini wa karibu zaidi wakiwa ni Wamisionari na wakoloni makatili ambao siyo tu walitawala kisiasa kwa kutumia mabavu Afrika bali pia kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Nakumbuka nyakati hizo wakubwa au waliozishuhudia sherehe nyingi za Krismasi duniani, mkubwa aliposhikwa mkono na mdogo basi alibakia akitarajia kusalimiwa.

Na hii ilijionyesha hata kwa wadogo kiumri kwa wenzao wadogo zaidi yao.

Namna ya kusalimiana ilikuwa imejijenga kabisa kisaikolojia sababu mtu akishajihisi kuwa mdogo kuliko mwingine basi moja kwa moja atatoa salamu ya 'shikamoo' na mkubwa atajibu 'marahaba'.

Au kwa wengine 'Assalam Alleykum' na mwingine hujibu 'Wa alleykum salam'. Zikimaanisha amani iwe juu yako na mwingine akijibu iwe pia juu yako.

Tangu tamaduni za magharibi zianze kuingia nchini kwa fujo kupitia njia kuu za televisheni, intaneti, utandawazi na vinginevyo kama hivyo mambo yamebadilika, lakini baadhi yamebakia kuwa yale yale. Silaumu na wala sipingi.

Hebu fikiria kuporomoka kwa maadili kunavyoingia kwa kasi mtoto hamjui baba. Hii ina maana wapo wanaojamiiana na wazazi wao hivyo hivyo kwa wazazi wa kike!

Sisemi hivi sababu ni dikteta au nina wivu sana, lakini nakumbuka enzi hizo masuala haya hatukupata kuyasikia sana kwa wingi, labda sababu hakukuwa na mawasiliano ya vyombo vya habari.

Siku hizi umeingia utamaduni wa kujenga mahusiano ya jinsia moja yaani madume kwa madume na wanawake kwa wanawake. Na hii inasambaa kwa kasi isiyokuwa ya kawaida!

Hali hii inatishia ndoa zinakuwa siyo kitu cha kukimbilia. Zinakuwa kama fasheni au aina fulani ya hovyo ya mahusiano. Vijana sasa wanataka mahusiano ya kimikataba.

Unapofiwa Dar ni kama wapi sijui. Makamera ya Video, sare kibao, gharama kibao, miziki tena ile ya blast na mengine kedekede.

Sitozungumzia mavazi sababu huo ni mjadala mzito nimeamua nigusie tu haya mawili matatu yanayoitikisa 'brain' yangu.

Tunapoiga tamaduni za kigeni ni muhimu tukawa wachaguzi na wenye welewa mpana ili kuepuka kuwa watu wa kuokota okota hovyo hata visivyofaa.

Saturday, April 01, 2006

Kutandawazishwa kusituondolee utu wetu

SIPENDI kusikia na wala kuona mambo yanavyoendelea katika jamii zetu hapa Afrika na hasa Tanzania licha ya kwamba katika baadhi ya mambo tunajitahidi kujikongoja angalau tuonekane nasi ni watu.

Nasema sipendi kwa sababu nyingi, mojawapo ikiwa ni kutojiamini wenyewe (Waafrika au Wabongo) kufanya mambo hadi wanapokuja watu weupe ndipo tunapoona kwamba eti ndiyo tumefanya vizuri sana.

Hebu angalia, kwa mfano tunaambiwa kuwa uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki kwa Afrika mpaka Ulaya na Marekani waseme au waangalie, kwani demokrasia maanake nini?

Hapa kwetu, wakati ule wa uchaguzi hawa watu weupe kutoka Marekani na Uingereza walijaribu kutuchanganya kidogo, taasisi ya NDI ikasema haukuwa huru, Jumuiya ya Ulaya ikasema haukuwa huru, lakini baadaye ikabadilika na kusema ulikuwa huru. Bahati nzuri hatukuyumba sana.

Waafrika tumekuwa tukitaabika na tatizo la kufutiwa lugha zetu, tuna lugha za kubahatisha, lugha zetu tulizo nazo sasa ni mchanganyiko tu wa zile zetu asilia kabisa na hizi za dunia ya sasa.

Tunajaribu kuumba aina mpya za lugha na aina mpya za utamaduni na hata mifumo 'feki' ya kiutawala popote pale tunapokuwa.

Tunao wasomi wa kutosha, lakini nao bahati mbaya wameshaingizwa katika utandawazi, yaani wametandawazishwa na sasa mawazo yao yamekaa kimshiko mshiko. Wanawaza kuandika 'paper' ili kuweza kujipatia mlo.

Vyuo vikuu vilikuwa chem chem ya fikra pevu, komavu au huru, zilizopikwa zikapikika na ilikuwa linapotoka wazo ndani ya jamii kama hiyo linaogopwa linafanyiwa kazi na linaaminika kwa sasa haya hakuna! Hakuna fikra tena za kiuanamapinduzi!

Hali hii imefanya baadhi ya watu kukata tamaa na kujiona na kusema kama unataka kufa maskini au kupata kichaa, basi jaribu kubadilisha mifumo ya 'Kiafrika', kisha uirudishe katika mstari.

Kule Marekani wenzetu matokeo ya tatizo hili yalizaa Unegro, Blues, Jazz, Hip-hop na tamaduni za ajabu ajabu zisizokuwa na mwanzo wala mwisho.

Miongoni mwetu weusi tunavyo visima vya busara au wanaharakati kama kina vile, Sylvester Williams, Marcus Garvey, George Padmore, CLR James, Cesarie, Stokely Carmichael (Kwame Toure) na Frantz Fanon.

Lakini sisi tunakwenda kinyume kabisa na wenzetu tunajaribu kadri tuwezavyo tuonekane Wazungu zaidi kwa kuzungumza Kiingereza “sanifu” au Kifaransa "fasaha" au Kispaniola "fasaha" au Kireno "fasaha".

Cha kushangaza zaidi baadhi yetu wanadiriki kujiita 'wazungumzaji wazuri au fasaha wa Kiingereza au wa Kifaransa wakati wao ni Waafrika wanazo lugha zao na wana kila la kwao.

Lakini, tujiulize tunavyofanya hivi tuseme kujifanya Wazungu zaidi kuliko wazungu wenyewe ndiyo maana nao wanatudharau kupita kiasi, wanafanya kila wanachojua kuhakikisha sisi tunakua kama wao na tunajisahau kabisa kama tuna nafsi.

Hatuwezi kuwa washiriki wazuri wa uamsho wa kuitetea Afrika mpaka tutakapoweza kwanza kujitambua sisi ni nani na majukumu yetu ni yapi katika kuendeleza vizazi vyetu.

Ni lazima kwanza tuangalie katika historia ya kisiasa, kifikra na kiutamaduni.

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...