Saturday, April 11, 2026

MFUMO MPYA WA MAFUTA WAONGEZA MAPATO, WAFANYABIASHARA WAFURAHIA

 


KAMPUNI ya Uingizaji na Usambazaji wa mafuta Jamii ya Petrol nchini ya ‘MOIL Energies’ imesema imefurahishwa kwa kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ulipaji kodi ya nishati hiyo kabla ya kuyatoa vituoni na kwenda sokoni (BIL)kwa kiasi kikubwa umesaidia kudhibiti ‘ujanja ujanja’ uliokuwepo hapo awali

Akizungumza Dar es Salaam Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo nchini, Dkt Sajad Habib Rai amesema wao kama Kampuni ya kwanza nchini kutoa mapendekezo ya kuanzishwa kwa mfumo huo kwa EWURA na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na baadae kuanzishwa rasmi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanajivunia kuona umetekelezwa kwa kuwa dhamira yao ilikuwa kuona huduma ya usambazaji wa mafuta nchini na nje ya nchi unaleta tija kwa Taifa.

“Tumefurahi kuona TRA wameusimamia kikamilifu mfumo huu kwa kuwa unazuia ukwepaji kodi ambao hapo awali ulikuwa ukifanywa na wafanyabiashara, hivi sasa TRA inapata kodi yake mapema kabla ya kuyaingiza mafuta sokoni” amesema Dk Sajad ambaye pia ni Meneja MKAZI wa ‘Mansoor Industry Limited’

Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza rasmi kuanza kutumika kwa mfumo huo ambao kwa kiasi kikubwa unalezwa kuleta tija kwa Serikali kwa kuwa umesaidia kudhibiti upotevu wa mapato unaotakana na Kodi za uingizaji wa mafuta hayo nchini.

Kupitia mfumo huo mpya na wa kisasa, kila mwagizaji au muingizaji wa mafuta atalazimika kutaja kiasi cha mafuta alichokiingiza nchini ambapo kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) watayataweka vinasaba kama alama ya kila mwagizaji kwa lengo la kuwatambua wahusika wote na kiasi alichoagiza ili kuwakadiria viwango vya Kodi wanavyopaswa kulipa.

“Nawapongeza TRA kwa kuona tija na umuhimu wa kuutumia mfumo huu, sisi kama wafanyabiashara tunaozingatia taratibu halali za uingizaji na Usambazaji wa mafuta tunaiona kuwa hatua hii ni kubwa na inayostahili kupongezwa kwa kuwa italeletea manufaa Taifa” ameongeza Dkt Sajad.

Utaratibu huo wa kikodi unawataka wamiliki wa mafuta hayo kuyalipia kodi kabla ya kuyaingiza sokoni ili yanapoingizwa sokoni yanaendelea na taratibu za uuzwaji hali ambayo inarahisisha usambazaji na kuwafikishia wateja huduma ya mafuta kwa wakati sambamba na kudhibiti kubaki nchini mafuta ambayo kimsingi yanapaswa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Aidha akizungumza wakati wa ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika bohari za kuhifadhia mafuta zilizopo Jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda pamoja na mambo mengine alisema lengo la TRA kuweka utaratibu huo ni kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi na kuondoa changamoto zilizokuwepo hapo awali huku akitoa wito kwa wafanyabiashara watakaokutana na changamoto zozote kuwasiliana na TRA.

Pamoja na mambo mengine pia Kamishina Mwenda alisema Mamlaka hiyo pia umeweka utaratibu wa kufanya kazi kwa Saa 24 ili kuharakisha utolewaji wa huduma kwa walipakodi ambao ni waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa mafuta hayo.



DKT. AKWILAPO AKUTANA NA MTENDAJI MKUU WA SHELTER AFRIQUE

 


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Shelter Afrique Bw.Thierno-Habib Hann wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao chao jijini Nairobi, Kenya, walipokutana pembezoni mwa Kongamano la pili la Miji Afrika lilofanyika nchini humo.

Na Munir Shemweta, WANMM Nairobi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Leonard Akwilapo, amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shelter Afrique Bw. Thierno-Habib Hann jijini Nairobi, nchini Kenya.

Viongozi hao wawili wamekutana pembezoni mwa Kongamano la Miji Afrika (2nd Africa Urban Forum) lililofanyika kuanzia Aprili 8 hadi 10, 2026 nchini Kenya, na kukutanisha mataifa mbalimbali Barani Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu na suluhisho bunifu katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya miji na makazi.

Dkt Akwilapo na Bw.Thierno-Habib Hann katika kikao chao walijadili masuala mbambali yanayohusu uimarishaji wa upatikanaji wa makazi nafuu kwa wananchi pamoja na ushirikiano kati ya serikali na taasisi za kifedha katika kufanikisha azma hiyo. 

Shelter Afrique ni taasisi ya kifedha ya kimataifa inayolenga kusaidia maendeleo ya makazi Barani Afrika, huku makao makuu yake makuu yakiwa jijini Nairobi nchini Kenya.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Kulia) akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Shelter Afrique Bw.Thierno-Habib Hann jijini Nairobi, Kenya walipokutana pembezoni mwa Kongamano la pili la Miji Afrika (2ND Africa Urban Forum) lilofanyika nchini humo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Kulia) akitambulishwa baadhi ya maafisa wa taasisi ya Shelter Afrique alipokutana na Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Bw.Thierno-Habib Hann pembezoni mwa Kongamano la pili la Miji Afrika (2nd Africa Urban Forum) lilofanyika jijini Nairobi nchini Kenya. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

MSD Yawanoa Watumishi Kanda ya Kilimanjaro Kuboresha Huduma za Afya

 






Watumishi wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kilimanjaro wanashiriki mafunzo maalum yenye lengo la kuimarisha uwajibikaji, mshikamano na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku—hatua muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa sekta ya afya nchini.

Mafunzo hayo yanafanyika mkoani Arusha, yakihusisha watumishi kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Lengo kuu ni kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kupitia misingi ya ushirikiano, umoja na maadili bora ya kazi.

Katika mafunzo hayo, washiriki wanapatiwa maarifa muhimu kuhusu mikakati ya utoaji huduma bora kwa wateja, maadili na uadilifu kazini, pamoja na uelewa wa kina wa mpango mkakati na mwelekeo wa taasisi. 

Aidha, wanajengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto za msongo wa mawazo na namna ya kudumisha uwiano kati ya kazi na maisha binafsi—mambo yanayochangia kuongeza tija kazini.

Kanda ya Kilimanjaro ya MSD inahudumia takribani vituo vya afya 991 vilivyopo katika mikoa hiyo mitatu, hivyo juhudi hizi zinatarajiwa kuongeza ufanisi katika usambazaji wa dawa na vifaa tiba, na hatimaye kuboresha huduma kwa wananchi.

Sambamba na vipindi vya kitaaluma, mafunzo hayo pia yamejumuisha michezo na shughuli za kijamii zinazolenga kujenga timu imara, kuimarisha mawasiliano na kukuza mshikamano miongoni mwa watumishi.

Hatua hii inaonesha dhamira thabiti ya MSD ya kuwekeza katika rasilimali watu wake ili kuhakikisha huduma bora, za haraka na zenye viwango vya juu zinawafikia Watanzania wote.

Thursday, April 09, 2026

TUTABORESHA BAJETI YA ELIMU – WAZIRI MKUU




▪️Asema Serikali itaimarisha vitengo vya tathmini na ufuatiliaji kila wizara

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya elimu wakati ikitekeleza mtaala mpya wa elimu ili kuziba mianya ya mahitaji shuleni.

“Kwa kuwa tunaenda katika mtaala mpya wa elimu, tutaendelea kuboresha bajeti. Tutaendelea kuboresha bajeti kwa sababu mahitaji yanaongezeka kila wakati katika kumfanya mtoto asome vizuri,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, leo (Alhamisi, Aprili 9, 2026) wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambert Kaiza, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali juu ya kukomesha michango holela inayotozwa shuleni.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali haina shida na michango ya chakula ambayo imekuwa ikitolewa shuleni lakini akasisitiza kuwa endapo kutatokea michango mingine yoyote, ni lazima ifuate miongozo ya serikali na ipate baraka za Wakuu wa Mikoa husika.

Akitoa mfano wa michango ambayo haikubaliki, Waziri Mkuu amesema akiwa ziarani mkoani Katavi, alipokea malalamiko ya Mama mmoja ambaye mwanaye alizuiwa kujiunga na shule ya sekondari hadi atoe sh. 50,000/- ya dawati.

“Nilielekeza yule mtoto arudishwe shuleni na nimpongeze Mkuu wa Mkoa ambaye amenijulisha kuwa yule mtoto amesharudi shuleni. Lakini pia nilielekeza yule mwalimu mkuu naye aitwe na mamlaka za nidhamu, ahojiwe kwa uzembe wa kuona mtoto anakosa masomo kwa miezi miwili na wao wakaendelea na maisha kana kwamba hakuna jambo lililotokea,” amesema.

Mbali na changamoto hiyo, Waziri Mkuu amewapongeza walimu nchini kwa kujitoa bila kuchoka ili kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora. “Sote tunatambua kuwa walimu wengi wamejitoa sana katika baadhi ya maeneo. Licha ya wingi watoto na uchache wa walimu, kwa juhudi zao wamehakikisha wanakamilisha syllabus zao ili watoto wetu wapate elimu bora.”

Akielezea kuhusu uwepo wa walimu wa kujitolea katika baadhi ya shule, Waziri Mkuu amesema alishatoa maelekezo kwamba malipo ya walimu wa aina hiyo yatoke kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri husika badala ya kuwataka wazazi wachangie malipo yao.

“Wazo la kuwa na walimu wa kujitolea ni jema, na sisi wakati tunasoma tulipata mafunzo ya ziada (tuition) kwa walimu wa aina hii. Wazo la kuwa na walimu wanaojitolea ni jema lakini malipo yao yasilipwe na wazazi, badala ya kwenda kwenye michango, Mamlaka za Serikali za Mitaa watumie mapato ya ndani.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha vitengo vya tathmini na ufuatiliaji katika kila wizara ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. “Kwenye kila wizara, kuna hivi vitengo vya ufuatiliaji na tathmini. Tunapanga kuongeza bajeti zao ili viweze kutimiza wajibu wao katika ufuatiliaji wa miradi na shughuli zote za Serikali.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Monduli, Isack Joseph Copriano aliyetaka kujua  Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha timu ya tathmini na ufuatiliaji ili kuharakisha majibu ya wananchi na hususan kero zao. 

Alisema katika kuimarisha mawasiliano na wananchi, Serikali imeanzisha kituo cha kupokea simu (Call Centre) yenye namba 190 ambapo mwananchi mwenye shida yoyote anaweza kupiga simu na kutoa kero yake na kwamba atajulishwa majibu yake kupitia kituo hicho.

Amesema Serikali inataka kurejesha utaratibu wa kila kiongozi kubeba hoja za wananchi kupitia rejesta ambazo zitakuwa zinatumika kwenye ofisi za viongozi kurekodi kero za wananchi na kutoa mrejesho serikalini kila mwisho wa mwezi.

“Utaratibu wa kupokea kero siyo wa kwenye ziara tu, kila mwezi viongozi watapaswa kutoa taarifa ya idadi ya wananchi waliowahudumia na majibu waliyowapa wakionesha hoja zipi walipokea, namba za simu za wananchi waliohudumiwa na hizo hoja zimetatuliwa vipi.” 

“Tunataka kurejesha utaratibu wa kila kiongozi kubeba hoja za wananchi na siyo kuacha wananchi waende kutafuta majibu kwa viongozi,” alisisitiza.


Wednesday, April 08, 2026

RAIS SAMIA ASHIRIKI DUA MAALUM KUMUENZI HAYATI KARUME, MIAKA 54 BAADA YA KUUAWA KWAKE











Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, jana tarehe 07 Aprili 2026 aliungana na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi katika dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Abeid Amani Karume, ikiwa ni kumbukizi ya miaka 54 tangu kuuawa kwake.

Dua hiyo ilifanyika katika Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui, Zanzibar, mahali penye historia kubwa katika harakati za kisiasa na mapinduzi ya Zanzibar. 

Tukio hilo limeambatana pia na zoezi la uwekaji wa shada la maua katika kaburi la hayati Karume, kama ishara ya heshima, kumbukumbu na kutambua mchango wake mkubwa katika kuijenga Zanzibar ya kisasa.

Katika tukio hilo lenye uzito wa kihistoria na kiimani, viongozi wa dini waliongoza dua maalum ya kumuombea marehemu Karume, wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza amani, mshikamano na uzalendo aliouasisi. 

Viongozi wa serikali, chama na wananchi waliohudhuria walipata fursa ya kutafakari mchango wake katika kuimarisha misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Hayati Karume anakumbukwa kama kiongozi shupavu aliyesimamia mageuzi makubwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, akijenga misingi ya usawa, haki na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar. Urithi wake unaendelea kuenziwa na viongozi wa sasa pamoja na vizazi vipya, kama sehemu ya historia muhimu ya Taifa.

Maadhimisho haya yanaendelea kuwa chachu ya kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa—misingi ambayo hayati Karume aliisimamia kwa dhati katika uongozi wake.

Friday, April 03, 2026

TANZANIA NA URUSI ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Urusi zimeingia hatua mpya ya ushirikiano wa maendeleo baada ya kusaini hati ya makubaliano katika sekta ya uchukuzi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza miundombinu ya kisasa na kuongeza ufanisi wa usafirishaji nchini.

Makubaliano hayo yalisainiwa tarehe 03 Aprili 2026 jijini St. Petersburg, Urusi, pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Uchukuzi na Usafirishaji, yakihusisha Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania na Wizara ya Uchukuzi ya Shirikisho la Urusi.

Kwa upande wa Urusi, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Andrey Nikitin, alieleza kuwa nchi yake ipo tayari kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Russia–Africa 2023. Alibainisha kuwa ushirikiano huo utahusisha uwekezaji katika miundombinu ya kisasa, msaada wa kiufundi, pamoja na ushiriki katika miradi ya kimkakati yenye tija kwa pande zote mbili.

Naye Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, alisema makubaliano hayo yanaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kushirikiana na mataifa yenye uzoefu mkubwa na teknolojia ya hali ya juu.

Alifafanua kuwa kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika na ubadilishanaji wa utaalamu, mafunzo kwa wataalamu, pamoja na uhamishaji wa teknolojia utakaosaidia kuongeza ufanisi, ubora na ushindani wa miundombinu ya uchukuzi. Aidha, alisisitiza kuwa hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kujijengea nafasi imara kama kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

Kwa mtazamo mpana, makubaliano haya yanafungua ukurasa mpya wa fursa za uwekezaji, utafiti na ubunifu, huku yakichochea maendeleo ya rasilimali watu na kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.

#Tanzania #Urusi #Uchukuzi #Maendeleo #Uwekezaji #Diplomasia #Miundombinu #HabariZaLeo








UPATIKANAJI WA DAWA WAIMARIKA NCHINI

 OWM-TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (OWM– TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya, Mhe. Dkt. Jafari Seif, amesema kuwa hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya katika ngazi ya huduma za afya ya msingi nchini imeendelea kuimarika na kufikia kiwango cha kuridhisha ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Akizungumza Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi kilichoongozwa na Waziri wa Afya, Mhe.Mohamed Mchengerwa, pamoja na wadau wa sekta ya afya, katika ofisi za Bohari ya Dawa (MSD), Mhe. Dkt. Seif amesema kuwa tathmini ya mwaka 2026 inaonesha hali ya upatikanaji wa dawa imefikia asilimia 89 katika hospitali, asilimia 88 katika vituo vya afya, na asilimia 88 katika zahanati.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi vilikusanya takribani Shilingi Bilioni 108, huku makusanyo hayo yakitarajiwa kuongezeka hadi kufikia Shilingi Bilioni 192 katika mwaka 2025/26.   

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuandaa na kusimamia miongozo, taratibu na miundo ya usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya. Lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa wafamasia kote nchini wanakuwa sehemu muhimu ya timu za menejimenti katika vituo hivyo, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.




SAMIA APEPERUSHA BENDERA YA USHIRIKIANO EAC, AKUTANA NA KATIBU MKUU IKULU CHAMWINO

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ...