Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2115 katika eneo la Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Nishati kusimamia ukamilishaji wa haraka wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kote nchini, ili umeme unaozalishwa katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere uweze kufika katika maeneo yenye mahitaji ya uzalishaji na uwekezaji.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo, tarehe 22 Agosti, 2026, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere, Rufiji, mkoani Pwani.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kunapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika uzalishaji, viwanda, biashara, madini, kilimo cha kisasa, huduma za kijamii, uwekezaji na ajira.
Kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, kinachangia takribani nusu ya umeme unaoingizwa katika Gridi ya Taifa, hatua inayoongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji na uhakika wa nishati nchini.
Rais Dkt. Samia amesema kukamilika kwa mradi huo ni matokeo ya fikra na maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, yaliyoendelezwa katika awamu mbalimbali za uongozi hadi sasa.
Katika hilo, ametambua mchango wa Marais waliomtangulia, hususan Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye katika awamu yake ya uongozi alichukua hatua thabiti za kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo muhimu mwaka 2019.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka Watanzania kulinda amani na utulivu wa nchi, sambamba na kuimarishwa kwa ulinzi wa miundombinu, mazingira na vyanzo vya maji vinavyotegemewa na kituo hicho ili kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Dkt. Mostafa Madbouly, ameipongeza Tanzania kwa kukamilisha kituo hicho, akisema mafanikio hayo yamedhihirisha uwezo wa ushirikiano wa Afrika katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
Ameongeza kuwa kukamilika kwake kunafungua nafasi ya kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Misri katika biashara, uwekezaji, ujenzi, barabara, bandari, kilimo, umeme na nishati.
Naye, Waziri wa Nishati, Mhe. Deo Ndejembi, amesema Serikali inaendelea kujenga njia ya kusafirisha umeme ya Kilovolti 400 ya Iringa–Mbeya–Songea–Rukwa, pamoja na njia za Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika na Tanzania–Uganda ili kuunganisha vituo vya uzalishaji, maeneo ya shughuli za kiuchumi na masoko ya kikanda.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina, amesema kituo hicho kinaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa nishati na shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ujenzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere ulianza mwaka 2019 kwa gharama ya shilingi trilioni 7.452. Kituo kina mitambo tisa yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 2,115, jengo la mitambo, transfoma 27 na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwa msongo wa Kilovolti 400.









No comments:
Post a Comment