Wednesday, December 10, 2008

Huduma za ndege ATCL zasitishwa ndani, nje ya nchi


Moja ya ndege za Shirika la Ndege Tanzania ambalo sasa huduma zake zimesimamishwa.

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL), ambalo limekuwa na matatizo makubwa tangu ndoa yake ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) ivunjike, limenyang’anywa cheti cha kuruka angani na Mamlaka ya Anga (TCAA) baada ya kukosa viwango vya ubora kuruka angani.

Taarifa kutoka ndani ya ya ATCL zimeeleza kuwa shirika hilo limenyang’anywa cheti hicho tangu Desemba 8 mwaka huu na hivyo litashindwa kusafirisha abiria hadi hapo litakapokidhi masharti ya usalama wa anga na kurejeshewa cheti hicho.

Miongoni mwa viwango hivyo vya usalama ni ukaguzi wa mara kwa mara wa ndege zake, kuwa na wataalamu wa kutosha kama marubani na wahandisi, vitu ambavyo vimeonekana kukosekana kwenye shirika hilo la serikali.

Kufungiwa huko kumekuja huku kukiwa na uwezekano wa shirika hilo kufungiwa na Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA) kufanya safari zake baada ya kubaini zaidi ya makosa 500.

Mwishoni mwa wiki iliripotiwa kuwa ATCL ilikaguliwa mwezi Oktoba na kubainika na makosa hayo ya usafiri wa anga, lakini ikashindwa kuyarekebisha na ndipo IATA ilipoanza mchakato wa kutaka kuizuia kufanya safari.

“Ni kweli ATCL imenyang’anywa cheti cha viwango kwa kukosa ubora wa kuruka angani hivyo haitafanya safari za nje wala ndani ya nchi,” alisema mmoja wa watu wa ndani TCAA alipohojiwa na Mwananchi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ndege za ATCL zilizokuwa zikifanya safari zake ndani na nje ya nchi haitaweza kufanya tena safari hizo na vigogo wa ATCL jana walikuwa na vikao na TCAA kuzungumzia suala hilo.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo katibu mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo alisema hana taarifa kuhusu kunyang’anywa cheti kwa ATCL na kudai kuwa mkurugenzi wa shirika hilo, David Mataka ndiye anayeweza kueleza suala hilo.

“Sina taarifa kuhusu suala hilo... hayo ni mambo ya ATCL na anayeweza kukueleza ni Mataka, hivyo wasiliana naye... haiwezekani toka tarehe nane hadi leo mimi sijui,” alisema Chambo.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...