MUDA wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unamalizika Desemba mwaka huu huku ikiwa imeweza kufanya mengi yakiwamo ya kuwashangaza hata wakubwa kutoka mataifa makubwa wanaoamini siku zote kwamba hakuna mweusi anayeweza kupanga jambo na kulitimiza.
Katika kipindi kifupi cha miaka miwili tangu Tanzania iwe mwanachama asiye wa kudumu wa baraza hilo kuanzia Septemba, 2004 hasa sasa, imesukuma ajenda nyingi, ikiwamo ya kupitisha azimio la kuhakikisha kunakuwapo amani ya kudumu kwenye eneo la maziwa makuu, kuanzishwa kwa kamati ya kusimamia mchakato wa amani katika nchi zilizotoka kwenye migogoro (PBC) n.k
Siri hiyo ya mafanikio ya Tanzania imemegwa na mwakilishi wake wa kudumu huko UN, Dakta Augustine Mahiga wakati akitoa mhadhara wa wazi katika Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa Kurasini, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Dk Mahiga alisema kuwa pamoja na kufanikiwa kupiga hatua hizo kwa muda mfupi umoja huo (UN) bado unakabiliwa na changamoto kadhaa kubwa. Naiunga mkono kauli hii ya Balozi Mahiga.
Kwa jumla, katika ramani ya dunia, siyo siri kwamba jina la Tanzania limeweza kujitokeza katika kila sehemu wanakotafuta usuluhishi, ingawa changamoto inabakia kwamba pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea, bado umoja huo unahitaji mabadiliko makubwa ili kuweza kukifanya kuwa chombo cha demokrasia na kilicho zaidi karibu na watu wake.
Yupo mwandishi mmoja mheshimika sana Uingereza ambaye usemi wake umenivutia na nalazimika kunukuu unaosema hivi: “Inafurahisha kuchekesha kwamba kifupi cha Umoja wa Mataifa kinabakia kuwa ni UN. Hii inanipa shida na kufikiri kila mara kama kitu hasi .
Kisichosaidia , cha kufikirika. Kisichokuwa na msaada.” Sina mtazamo kama wake, lakini nikiangalia mambo yanavyokwenda Mashariki ya Kati na kwingineko duniani, inanishawishi kukubaliana na mwelekeo wa fikra za mzungu huyu japo sipendi sana kushabikia masuala ya aina kama yake.
Sitaki kujiingiza moja kwa moja katika masuala yanayotokea katika vita kali kati ya Israel na kikundi cha Hezbollah iliyoharibu kabisa miji ya Lebanon na Israel na jinsi ambavyo umoja huo umechukua hatua au kushindwa kufanya hivyo, lakini inanibidi kwa sababu kama taifa mwanachama yanayomkabili Lebanon yaweza kabisa kuitokea nchi yetu.
Hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa yakifanyika katika umoja huo tangu aingie madarakani Katibu Mkuu wake wa sasa, Koffi Annan, lakini wengi wetu tungali tunajiuliza hivi mabadiliko haya yanayolenga katika mambo yaliyopitwa na wakati katika ushiriki wa mataifa wanachama kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndicho kitu pekee tunachokihitaji?
Kwanini Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani wapate fursa ya kutumia kura ya veto katika kupitisha maazimio ambayo hawana hata haja ya kufanya marekebisho?
Kwanini China wawe na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini siyo Tanzania, India au Nigeria eti kwa sababu Tanzania ni sehemu ya ‘koloni’ la Waingereza tangu miaka ile, kwanini Japan na Ujerumani wanatengwa kuingia ndani ya ‘chungu’ sababu tu eti walipigania upande mbaya wakati wa vita kuu ya pili ya dunia?
Hata hivyo, hata kama uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utaongezeka kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea kufanyika ndani ya umoja huo hivi sasa, tunadhani kutakuwa ufanisi katika ulinzi wa amani wa dunia?
Hivi tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo utayari wa kukabiliana na migogoro na mauaji ya watu wengi kama yale ya Rwanda au Bosnia utaongezeka? Inavyoonekana siyo rahisi. Lakini, tunahitaji UN inayoweza kubadilika na kwenda na wakati.
No comments:
Post a Comment