Wednesday, September 27, 2006

Tutaosha miguu ya bodi hii ya mikopo hadi lini?

Mheshimiwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Vijana humu nchini tunaipata joto ya jiwe. Kwanza joto ya kwanza ya jiwe ni ya kupata ajira ukiachilia lile la kupata ajira nzuri suala ambalo linaonekana kama vile ni miujiza au bahati au uwe na mtu wa kukupigia debe. Kataeni huo ndiyo ukweli.

Na upatikanaji wa ajira nzuri yenye kulipa ambayo angalau itakusukuma leo, kesho na keshokutwa inabidi uwe na elimu ya juu ambayo kwa kiasi kikubwa hapa kwetu inakimbilia chuo kikuu.

Tangu mwaka 1995 na nyuma ya hapo serikali yetu imekuwa ikifanya mabadiliko makubwa katika utoaji wa elimu ya juu, walianza na awamu ya kwanza ya pili na sasa ya tatu ya mikopo.

Ni mikopo! Mikopo tuu! changia! changia! Sawa hatuwezi kukwepa, lakini hali hii inakwenda tofauti kabisa na hali halisi ya Mtanzania kwani wakati gharama za tuisheni zikikwea juu, kipato cha Mtanzania masikini mvuja jasho ambaye ndo mwenye watoto wengi kinashuka sana tena vibaya.

Na hadithi hii inakuwa chungu zaidi. Wakati tuisheni ikilipuka juu, fedha ya mikopo ya serikali inazidi kuwa finyu na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi wakiwa watoto wa wakulima na wafanyakazi kubeba zigo zito la kulipa tuisheni.

Tumesikia serikali ikijikakamua angalau kuongeza kabajeti ka kusomesha vijana elimu ya juu na hapana shaka kwamba, baada ya mikopo hii watoto wa walala hoi wengi watabakia hoi kweli kweli.

Tuchukulie kwa mfano kulipa deni la mkopo wa kusoma kwa asilimia 10- 15 tu kwa miaka 10, itamaanisha gharama za ulipiaji deni ambao hauko chini ya sh. 15,000 kwa mwezi.

Hii itafanya vijana wengi wanaohitimu elimu ya chuo kikuu kuchagua kutoenda katika ajira zinazolipa mshahara mdogo, licha ya kuwapo tatizo sugu la ukosefu wa ajira. Wanaweza kujishikiza, lakini katu hawatofanya kazi kiufanisi.

Hakuna jinsi kwa hili kwa sababu, bodi ni moja tuu hakuna mbadala, labda kungekuwa na uwezo watoto wa walalahoi wangekimbilia mbadala mwingine huko wangepata mkopo kwa wakati wakaacha kuwekewa mikwara na vijana wakasoma kwa nafasi.

Wimbo huu wa kila siku bodi! bodi! haijafanya hiki au kile mpaka wafuatwe katika ofisi zao wastuliwe kidogo ‘ waoshwe miguu’ , wabembelezwe ndo watoe pesa, unaturudisha nyuma saana unatujengea wasomi wa hovyo wasiokuwa na utulivu wala busara.

Wakati mwingine huwa nakaa kufikiria huenda kuna watu wanakaa wakifurahia wengine wakitaabika. Haipendezi umefikia wakati kuwe na options kwaajili ya watu kwenda huko ili kusudi isielemewe bodi moja tu.

Wednesday, September 13, 2006

Hayawi hayawi sasa yamekuwa

Nasema kumekucha jogoo limekwishawika huku mwananchi tumeshaingia hewani jamani, kwa habari za kitaifa, kimataifa, biashara na michezo na makala zilizosadifiwa na kuandikwa na watu wenye fikrapevu, wenye upeo mpana sana katika maisha ya jamii ya kitanzania unaweza kutupata kwa kubonya hapa tupo katika majaribio na tutaanza rasmi muda si mrefu!!

Tuesday, September 12, 2006

Mzee wa Sumo amerejeaaaa

Jamani nadhani kuna wale ambao mlikuwa mmeshaanza kukata tamaa nakumbuka rafiki yangu Jeff Msangi alisema amechoshwa kuingia mtandaoni na kukuta mipicha au makala za zamani, sasa Mzee wa Sumo karudi waka waka na mapicha kibaooo ya kila aina kuanzia yale ya kitaifa, kimataifa, michezo, burudani na hata mambo mengine utakayohitaji hebu mcheki kwa kubonya hapa

Tanzania imeweza, lakini UN inahitaji mtazamo mpya

Hiki ndo chungu chenyewe cha maamuzi duniani yaani Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa maamuzi yote duniani yanatoka hapa, unaweza kumuona Waziri Asha-rose Migiro kwa mbali akiendesha kikao


MUDA wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unamalizika Desemba mwaka huu huku ikiwa imeweza kufanya mengi yakiwamo ya kuwashangaza hata wakubwa kutoka mataifa makubwa wanaoamini siku zote kwamba hakuna mweusi anayeweza kupanga jambo na kulitimiza.
Katika kipindi kifupi cha miaka miwili tangu Tanzania iwe mwanachama asiye wa kudumu wa baraza hilo kuanzia Septemba, 2004 hasa sasa, imesukuma ajenda nyingi, ikiwamo ya kupitisha azimio la kuhakikisha kunakuwapo amani ya kudumu kwenye eneo la maziwa makuu, kuanzishwa kwa kamati ya kusimamia mchakato wa amani katika nchi zilizotoka kwenye migogoro (PBC) n.k
Siri hiyo ya mafanikio ya Tanzania imemegwa na mwakilishi wake wa kudumu huko UN, Dakta Augustine Mahiga wakati akitoa mhadhara wa wazi katika Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa Kurasini, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Dk Mahiga alisema kuwa pamoja na kufanikiwa kupiga hatua hizo kwa muda mfupi umoja huo (UN) bado unakabiliwa na changamoto kadhaa kubwa. Naiunga mkono kauli hii ya Balozi Mahiga.
Kwa jumla, katika ramani ya dunia, siyo siri kwamba jina la Tanzania limeweza kujitokeza katika kila sehemu wanakotafuta usuluhishi, ingawa changamoto inabakia kwamba pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea, bado umoja huo unahitaji mabadiliko makubwa ili kuweza kukifanya kuwa chombo cha demokrasia na kilicho zaidi karibu na watu wake.
Yupo mwandishi mmoja mheshimika sana Uingereza ambaye usemi wake umenivutia na nalazimika kunukuu unaosema hivi: “Inafurahisha kuchekesha kwamba kifupi cha Umoja wa Mataifa kinabakia kuwa ni UN. Hii inanipa shida na kufikiri kila mara kama kitu hasi .
Kisichosaidia , cha kufikirika. Kisichokuwa na msaada.” Sina mtazamo kama wake, lakini nikiangalia mambo yanavyokwenda Mashariki ya Kati na kwingineko duniani, inanishawishi kukubaliana na mwelekeo wa fikra za mzungu huyu japo sipendi sana kushabikia masuala ya aina kama yake.
Sitaki kujiingiza moja kwa moja katika masuala yanayotokea katika vita kali kati ya Israel na kikundi cha Hezbollah iliyoharibu kabisa miji ya Lebanon na Israel na jinsi ambavyo umoja huo umechukua hatua au kushindwa kufanya hivyo, lakini inanibidi kwa sababu kama taifa mwanachama yanayomkabili Lebanon yaweza kabisa kuitokea nchi yetu.
Hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa yakifanyika katika umoja huo tangu aingie madarakani Katibu Mkuu wake wa sasa, Koffi Annan, lakini wengi wetu tungali tunajiuliza hivi mabadiliko haya yanayolenga katika mambo yaliyopitwa na wakati katika ushiriki wa mataifa wanachama kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndicho kitu pekee tunachokihitaji?
Kwanini Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani wapate fursa ya kutumia kura ya veto katika kupitisha maazimio ambayo hawana hata haja ya kufanya marekebisho?
Kwanini China wawe na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini siyo Tanzania, India au Nigeria eti kwa sababu Tanzania ni sehemu ya ‘koloni’ la Waingereza tangu miaka ile, kwanini Japan na Ujerumani wanatengwa kuingia ndani ya ‘chungu’ sababu tu eti walipigania upande mbaya wakati wa vita kuu ya pili ya dunia?
Hata hivyo, hata kama uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utaongezeka kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea kufanyika ndani ya umoja huo hivi sasa, tunadhani kutakuwa ufanisi katika ulinzi wa amani wa dunia?
Hivi tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo utayari wa kukabiliana na migogoro na mauaji ya watu wengi kama yale ya Rwanda au Bosnia utaongezeka? Inavyoonekana siyo rahisi. Lakini, tunahitaji UN inayoweza kubadilika na kwenda na wakati.

Saturday, September 09, 2006

Ipo siku tutakuja kununua mchele gengeni kwa dola

Benki Kuu chimbuko na mdhibiti mkuu wa pesa.

MAJUZI gazeti la Mwananchi liliripoti kuporomoka kwa kasi kwa sarafu ya Tanzania, hali ambayo lilielezwa kuwa unazusha hofu kama mkakati wa kuwapatia Watanzania maisha yenye neema zaidi.

Habari za kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa dola ya Marekani zimeleta si tu hofu, bali balaa kwa wananchi wa kawaida.

Kwanza kwa kuwa wajanja wachache wanaojua kucheza na mahesabu wameanza kuutumia mwanya huu kujipatia mamilioni ya shilingi kutokana na ujinga wa wengi.

Wanauza bidhaa walizonunua mwaka au miezi mingi iliyopita nje ya nchi kwa thamani ya sasa ya dola badala ya kutumia bei ya chini ya wakati walipopata bidhaa hizo.

Mtindo huu wa kuthaminisha bidhaa ulizonunua zamani kwa bei ya sasa ni dhahiri kwamba ni wizi usiofaa na unawanyonya wengine kinyume kabisa cha utaratibu

Vyovyote iwavyo, lakini kwa mantiki ndogo tu ni dhahiri kwamba iwapo utanunua bidhaa kwa fedha za kigeni kuna hatari kubwa sana ya kupata hasara, hasa kama pesa haina nguvu kama hii yetu.

Kwa hapa kwetu kwa kuwa wananchi wengi wanapata pesa baada ya kufanya kazi, ambapo hulipwa au kwa lugha nyingine hufidiwa nguvu zao iwe zaidi au kidogo, lakini mara nyingi hupunjwa na huzitumia kwaajili ya matumizi ya kila siku maishani mwao.

Inakuwa vipi kwa vijisenti hivyo eti uende kuvibadilisha hivi utapasa senti ngapi, ili uweze kununua bidhaa unayotaka? Tuachane na mtindo huu unatufanya kujitia uzungu zaidi huku tunajibomoa!

Ndiyo nakubali kwamba wapo wenye vijiakiba, lakini ni wachache sana ambao hawatumii fedha zao kabisa, ambao huziwekeza ili ziweze kuongezeka.

Hivi kwanini huduma na bidhaa ziuzwe kwa dola? Kwanini printers zilizonunuliwa mwaka juzi ziuzwe kwa thamani ya sasa ya dola? Kwa mtindo huu ipo siku wafanyabiashara wa mchele na viazi watauza bidhaa hiyo kwa dola na watatoa visingizio vingi tu. Hatutakubali!

Nafikiri kinatakiwa kifanyike kitu ili kuweza kunusuru balaa hili, sababu kama kunakuwa na uchezeaji akili za watu na kisha kuwapunja kwa staili hii inakuwa siyo sawa.

Fedha hasa noti ni utambulisho muhimu sana wa taifa na ni kitu kikubwa kinachowaunganisha wananchi wa taifa husika na hivyo kuondoa mianya ya kufanyika kwa biashara isiyo halali.

Muda si mrefu uliopita, tulikuwa tukinunua muda wa maongezi katika simu kwa kutumia fedha zetu lakini tulikuwa tukiuthaminisha kwa dola. Hivi nini dola, mbona Wapakistan, Wahindi, Wachina wanajivunia vya kwao kwanini isiwe sisi?

Alinifurahisha Waziri mmoja wa Pakistan kipindi hicho nikiwa New York, Marekani hotelini, Waziri yule alifika katika jiji lile kuhudhuria kikao kimojawapo cha Umoja wa Mataifa.

Alipotakiwa alipie gharama za chumba akatoa bulungutu la rupia za kwao. Mhudumu alimshangaa sana, lakini naye waziri yule alimshangaa sana yule mhudumu.

Kila mmoja kati yao alikuwa akijifanya kuwa yeye zaidi. Yule Waziri akamuona yule mhudumu mpuuzi, lakini naye mhudumu akamuona waziri mshamba, lakini ukweli wa mambo waziri alionyesha uzalendo na utaifa wa hali ya juu.

Hata hivvyo hatimaye waziri alizunguka akaenda kubadilisha bulungutu la rupia zake, lakini bado alikuwa akilalamika kwanini rupia za kwao hazitumiki Marekani!

Hadithi hii ingepaswa nasi tukawa angalau tunaifikiria hivi kwa mfano hawa wanaojifanya biashara ni huria kwanini tunalazimika tukiwa kwao kutumia pesa zao na kwanini siyo zetu.

Hata hivyo kikubwa kinachotakiwa ni kama serikali yetu inavyofanya sasa kuwawezesha wananchi mmoja mmoja wawe na uwezo wa kujimudu kujiendesha kimaisha vinginevyo aina hii ya unyonyaji itatumaliza!

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...