Wednesday, July 29, 2026

WANANCHI WALIPONGEZA JESHI LA POLISI KATAVI KWA KUFANYA USAFI MAENEO MBALIMBALI.

Wananchi wa eneo la soko kuu la Manispaa ya Mpanda mjini, Mkoani Katavi wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la usafi lililofanyika sokoni hapo, ambapo wamesema hatua hiyo imechangia kuboresha mazingira ya biashara na afya ya jamii kwa ujumla.

Zoezi hilo limefanyika Julai 29, 2026 likiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kamishna msaidizi Mwandamizi (SACP) Kaster Ngonyani ambapo, amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu lenye lengo la kuhamasisha wananchi kutunza mazingira huku akiwataka wafanyabiashara na wananchi kuendelea kushirikiana katika kudumisha usafi wa soko na maeneo mengine yanayowazunguka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Kashaulili Ndugu Johari Korongo amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa kuonyesha ushirikiano mzuri na wananchi kwa kujitolea na ametoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na huduma kwa jamii.



Tuesday, July 28, 2026

Rais Samia Akutana na Balozi wa China Nchini Tanzania



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, katika Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, tarehe 28 Julai 2026.

Mazungumzo hayo yamejikita katika kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China, hususan katika maeneo ya biashara, uwekezaji, maendeleo ya miundombinu na sekta nyingine za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tanzania na China zimeendelea kushirikiana kwa karibu kwa miongo kadhaa, ambapo ushirikiano huo umechangia utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi na kukuza mahusiano ya kirafiki kati ya mataifa hayo mawili.

Mkutano huo unaakisi dhamira ya pande zote mbili ya kuendeleza ushirikiano unaojengwa juu ya kuheshimiana, maslahi ya pamoja na maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na China.

VIONGOZI WATEULE WAAPA KIAPO CHA UADILIFU MBELE YA RAIS SAMIA







Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaapisha viongozi mbalimbali walioteuliwa kula Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.

Rais Samia Suluhu Hassan, aliwaapisha Dkt. Latifa Mohammed Khamis kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Ndugu Prisca Burton Lwangili kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Hafla hiyo ya uapisho imefanyika Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026, ambapo viongozi hao wameapishwa rasmi kuanza kutekeleza majukumu yao katika nafasi walizoteuliwa.

Kiapo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya sheria na utaratibu wa utumishi wa umma, kikilenga kuimarisha uwajibikaji, uadilifu, uzalendo na uzingatiaji wa maadili katika utekelezaji wa majukumu ya viongozi wa umma.

Hafla hiyo imeashiria mwanzo rasmi wa viongozi hao kuanza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uongozi bora na kutoa huduma zenye tija kwa wananchi.

Monday, July 27, 2026

WAZIRI NDEJEMBI AWASILI SHINYANGA KUSHUHUDIA MRADI MKUBWA WA UMEME WA JUA WA MEGAWATI 100





Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.), leo Julai 27, 2026, amewasili mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi, ambapo amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, tayari kwa shughuli muhimu ya uzinduzi wa hatua mpya ya maendeleo katika sekta ya nishati nchini.

Katika ziara hiyo, Waziri Ndejembi ataongoza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kushuhudia utiaji saini wa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Jua chenye uwezo wa Megawati 100, kitakachojengwa katika eneo la Ngunga, wilayani Kishapu.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu na kuendelea kuiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo kupitia uwekezaji katika vyanzo safi vya nishati.

Katika ziara hiyo, Waziri ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu (Mb.), na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Simon Songe Lusengekile, wakionesha dhamira ya pamoja ya Serikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati kwa maendeleo ya Taifa.

Thursday, July 23, 2026

DKT. ABBASI AKAGUA MIRADI YA UTALII PORI LA AKIBA LA PANDE, ATOA MAAGIZO YA KUKAMILIKA KABLA YA AFCON 2027







Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Julai 23, 2026, ametembelea Pori la Akiba la Pande jijini Dar es Salaam na kukagua maendeleo ya miradi ya kuboresha miundombinu na huduma za utalii inayotekelezwa katika eneo hilo.

Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa la kuogelea (swimming pool), bwawa la watoto (Kids Playing Grounds), uwanja mdogo wa mpira wa miguu na uwanja wa beach volleyball, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kupokea wageni na mashabiki wa AFCON 2027, ambayo Tanzania itaandaa kwa ushirikiano na Kenya na Uganda.

Dkt. Abbasi amesisitiza miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa ili kuhakikisha wageni watakaofika nchini wanapata fursa ya kutembelea na kufurahia vivutio vya utalii vilivyopo Pori la Akiba la Pande.

Pori la Akiba la Pande linapatikana takribani kilomita 45 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam na linaendelea kuimarishwa kuwa moja ya vivutio muhimu vya utalii wa asili nchini.

Wednesday, July 22, 2026

MIAKA 99 YA JESHI LA CHINA IWE CHACHU CHA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA ULINZI NA TANZANIA- DKT RHIMO NYANSAHO






Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na China katika diplomasia ya ulinzi ili kuimarisha usalama, maendeleo na uchumi endelevu wa mataifa hayo. Dkt. Nyansaho amesema hayo tarehe 21 Julai, 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka 99 ya kuanzishwa kwa Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA), yaliyoandaliwa na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian.

Katika hotuba yake kwenye maadhimisho hayo, Waziri wa Ulinzi na JKT ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa China, Xi Jinping, kwa kuendeleza urafiki wa kihistoria ulioasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Zedong, hususan katika sekta ya ulinzi. 

Kwa upande wake, Balozi Chen Mingjian aliahidi kuwa China itaendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kihistoria na Tanzania katika masuala ya ulinzi, ikiwemo mafunzo ya kijeshi.

Tuesday, July 21, 2026

WACHIMBAJI WADOGO WAISHUKURU SERIKALI KWA USAMBAZAJI WA UMEME MIGODINI







*Nyang’hwale, Geita*

Wachimbaji wadogo wa madini wilayani Nyang'hwale, mkoani Geita, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye maeneo ya migodi, hatua inayopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji.

Shukrani hizo zimetolewa wakati Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alipozindua mradi wa kuzalisha nishati ya umeme wenye uwezo wa KVA 500 kwenye Mgodi wa wachimbaji wadogo katika eneo la Igalula, wilayani Nyang'hwale. Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 426 na ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya nishati katika maeneo ya uchimbaji wa madini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Mavunde amesema Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na uzalishaji katika sekta ya madini kwa kusambaza umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati.

Amesema Serikali tayari imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 7 kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya migodi nchini, hatua iliyowezesha wachimbaji kupunguza utegemezi wa mitambo inayotumia mafuta na hivyo kushusha gharama za uzalishaji huku ikiongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji.

Katika kuendelea na ziara yake, Waziri Mavunde amekagua mradi wa maji safi na salama unaotekelezwa katika Kijiji cha Kakola, ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 24,801

Amesema mradi huo unatekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi, hususan wanawake, wanaondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

"Ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani inaendelea kutekelezwa kwa vitendo kupitia miradi ya maji kama huu wa Kakola ambao utaboresha afya, ustawi na shughuli za kiuchumi za wananchi,"  amesema.

Katika sekta ya elimu, Waziri Mavunde amezindua Shule ya Msingi Imara Baruti iliyojengwa ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa takribani kilomita nne kwenda kusoma katika Shule ya Msingi Shabaka.

Amesema ujenzi wa shule hiyo unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayosisitiza ujenzi wa shule karibu na makazi ya wananchi ili watoto wapate elimu katika mazingira bora.

"Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuthibitisha kuwa ahadi zinazotolewa kwa wananchi si maneno ya kampeni pekee, bali ni mipango inayotekelezwa kwa vitendo kwa manufaa ya Watanzania," amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amempongeza Waziri Mavunde kwa kufanya ziara ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo mkoani humo, akisema hatua hiyo imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuimarisha ufuatiliaji wa huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja.

Shigella amebainisha kuwa uwekezaji unaoendelea katika sekta za madini, elimu, maji na nishati unaendelea kuifanya Geita kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa madini na maendeleo ya kijamii nchini.

NIRC YAFUNGUA SURA MPYA YA KILIMO: MIRADI 30, PAMPU 2,000 NA AJIRA 4,000

  Na Mwandishi Wetu, Dodoma Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) inatarajia kuanza utekelezaji wa miradi mipya zaidi ya 30 ...