Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.), leo Julai 27, 2026, amewasili mkoani Shinyanga kwa ziara ya kikazi, ambapo amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, tayari kwa shughuli muhimu ya uzinduzi wa hatua mpya ya maendeleo katika sekta ya nishati nchini.
Katika ziara hiyo, Waziri Ndejembi ataongoza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kushuhudia utiaji saini wa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Jua chenye uwezo wa Megawati 100, kitakachojengwa katika eneo la Ngunga, wilayani Kishapu.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu na kuendelea kuiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo kupitia uwekezaji katika vyanzo safi vya nishati.
Katika ziara hiyo, Waziri ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu (Mb.), na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Simon Songe Lusengekile, wakionesha dhamira ya pamoja ya Serikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati kwa maendeleo ya Taifa.





No comments:
Post a Comment