Tuesday, February 16, 2010

Msekwa ammwagia sifa Spika Sitta


Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) Pius Msekwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma leo. Kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC, John Chiligati. Picha na Jube Tranquilino.

*************************************************

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa amemmwagia sifa Spika wa Bunge Samuel Sitta kwa kile alichoeleza kuwa amefanikiwa kumaliza sakata la Richmond kwa busara kubwa.
 
Akizungunza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma leo, Msekwa alisema sababu ya uhasama wa wabunge wa CCM, Msekwa alisema yalitokana na sakata lililoibuliwa mwanzoni mwa mwaka 2007 na kusababisha mtikisiko mkubwa ndani ya serikali ya awamu ya nne.

CCM iliingia kwenye mtafaruku uliotengeneza makundi mawili makubwa mwaka 2008 baada ya sakata la Richmond kutinga bungeni na kisha kuwakumba baadhi ya makada wa juu wa chama hicho, waliotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo ya kifisadi iliyotokana na zabuni tata ya uzalishaji umeme wa dharura iliyoipa ushindi kampuni hiyo(Richmond).

Baadhi ya makada wa chama ngazi za juu katika chama na serikali, akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wawili walioitumikia Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti wakati wa mchakato wa zabuni hiyo, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujizulu kutokana na kudaiwa kuhusika katika sakata hilo, huku maofisa wengine wa umma wakitakiwa kuchukuliwa hatua na serikali.
 
Alisema baada ya sakata hilo kulipuka kulitokea mgawanyiko mkubwa katika chama uliozaa makundi mawili. Alitaja vinara wa makundi hayo kuwa ni mbunge wa Monduli Edward Lowassa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
 
Kwa mujibu wa Msekwa makundi hayo kila moja lilikuwa likituhumu kundi jingine kuwa lina nia ya kuwang’oa wenzao madarakani, jambo hilo lilileta mtafaruku mkubwa.
 
“Tumewaita vinara wa makundi hayo na kukaa nao meza moja. Lakini hatukuwa na nia ya kutaka kuwatoa kafara kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, bali tulitaka amani idumu jambo linaloonyesha kuwa tumefaulu,” alisema Msekwa na kuongeza:
 
“Pamoja na kukaa nao kwa muda wa saa nne katika moja ya kumbi za pale bungeni, kila mmoja alikuwa na kero zake jambo tulilogundua kuwa kila mtu alikuwa akifagilia kitumbua chake kisiingie mchanga”.
 
Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama ni kumtonesha kidonda jana Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Msekwa alimfagilia spika Sitta kwa kumaliza sakata la Richmond na kisha kuonya kuwa watakaoliendeleza watachukuliwa hatua.
 

Miss Tanzania apata dhamana


Miss Tanzania, Miriam Gerald, akiwa na ndugu zake kuelekea nyumbani baada kudhaminiwa na mkurugenzi wa mashindano hayo Hashim Lundenga kwenye mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Miriam pamoja na rafiki yake wa kiume Kenedy Victor wanashtakiwa kwa kosa la kujeruhi na kuharibu mali na wote wamekewa dhamana. Picha na Silvan Kiwal

******************************************************************************************************************

HATIMAYE Miss Tanzania 2009, Miriam Gerald ameachiwa kwa dhamana baada ya kukaa rumande kwa siku tatu, kuanzia Ijumaa mchana kwa kukosa dhamana.

Mrembo huyo wa mwaka jana, alipelekwa rumande kwa kile kilichoelezwa kushambulia pamoja na kuharibu mali.

Katika shtaka la kwanza, wanatuhumiwa kumshambulia Shaaban Moshi kwa vitu vyenye ncha kali shtaka lililosomwa na mwendesha mashtaka Inspekta wa Polisi, Nassor Sisiwahy, mbele ya Hakimu, Kwey Lusemwa.

Shitaka la pili, watuhumiwa kufanya uharibifu wa mali yenye thamani ya Sh laki 720,000. Mali iliyoelezwa ni vifaa vya muziki. Ijumaa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa Gereza la Segerea.
Hata hivyo, jana alipata dhamana pamoja na rafiki yake, Kennedy Victor.

Baada ya kuruhusiwa na mahakama, Mratibu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliwaomba radhi Watanzania kwa yanayotokea kwa washindi wa taji hilo.

Lundenga aliyasema hayo jana nje ya Mahakama ya Kinondoni baada ya kumwekea dhamana mrembo wake na kusema: "Hayo ni mambo ya kimaisha na yanaweza kumtokea yeyote."

Mrembo huyo aliwasili mahakamani hapo saa 5.15 asubuhi akiwa kwenye gari aina ya Land Cruizer STK 4253 ambalo liliingia Mahakamani hapo kwa kasi akiwa na wenzake wawili na Miriam alishuka akiwa amejifunika mtandio usoni.

Baada ya hapo, saa 11.30 washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na Hakimu Richard Kabate ambaye aliwaachia kwa dhamana kwa niaba ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kwey Lusema.

Wote walitimiza masharti ya dhamana yao na kuwataka kurudi tena mahakamani Februari 25 .

Lundenga alitoa dhamana hiyo kwa mrembo wake Miriam huku Kennedy akitolewa dhamana na rafiki yake Omary Juma Idd ambaye ni mfanyakazi wa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.

'' Siwezi kuongea mengi kwa kuwa kesi bado ipo mahakamani ila naweza kusema kuwa yaliyomtokea Miriam ni matatizo tu ya kimaisha hatutakiwi kumlaumu kwani mpaka sasa bado hatujajua kama kosa hilo katenda au la,'' alisema Lundenga.

Aidha Lundenga alisema kuwa kwa kitendo alichofanyiwa Miriam si cha kistaarabu na kamati yake inawatafuta warembo hao wanasheria na wanapopatwa na matatizo wawe wanaongea na sio warembo wenyewe. SOURCE: MWANANCHI

Monday, February 15, 2010

Bia za TBL sasa bei juu


WANYWAJI wa bia zinazotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Breweries Limited (TBL) sasa itabidi wajitutumue zaidi kugharimia starehe hiyo kutokana na bei ya bidhaa hizo kuongezeka.

Afisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu alisema kwamba bei hiyo mpya itaanza kutumika kuanzia leo.

Malulu alisisitiza wauzaji wa rejareja kuuza kwa bei iliyoidhinishwa na TBL ili kuepuka dhuluma na kuwaongezea mzigo wanywaji.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kama bei hiyo mpya itazingatiwa hasa kwa jiji la Dar es Salaam, huenda isiwe ni jambo la ajabu kwa sababu baa nyingi tayari zilianza kutumia bei hiyo tangu Julai, mwaka jana.

TBL walijaribu kupambana na walanguzi hao tangu mwaka jana kwa kusambaza vibao ili vibandikwe kwenye mabaa na kuonyesha bei halisi, lakini baadhi ya mabaa walivitupilia mbali na kuuza kwa bei wanazotaka wao.

Kwa mujibu wa bei hiyo mpya iliyotangazwa na TBL jana, bia za Safari, Kilimanjaro, Tusker, Bingwa na Balimi ambazo zinauzwa kwa ujazo wa mililita 500, sasa bei yake halisi ni Sh1,400 badala ya bei ya zamani ya sh1,300.

Aina ya bia hizo, ambazo zinauzwa katika ujazo wa mililita 330, badala ya Sh1,100 sasa zitauzwa kwa Sh.1,200, isipokuwa Balimi ambayo itakuwa Sh1,000.

Akifafanua zaidi juu ya bei hiyo mpya, Malulu alisema kwa ujumla bei ya bia zote kwa rejareja zimeongezeka kwa Sh100.

Bei mpya ya aina nyingine za bia za TBL pamoja na kiwango cha ujazo wa mililita kwenye mabano ni Ndovu Special Malt (375) Sh1,400, Castle Lager (500) Sh1,500, (330) 1,300, Castle Milk Stout (500) Sh1,600 na (375) Sh1,300.

Guinness (500) Sh1,800, Redd’s Premium Cold (330) na (375) Sh1,400 wakati bia zinazopatikana zaidi Kanda ya Kaskazini za Eagle (500) Sh1,100 na (300) Sh700.

Kwa mujibu wa bei hizo mpya, Kinyaji kisicho na pombe cha Guinness Malt (300) kitauzwa kwa Sh900 na (330) Sh1,100.

Malulu alizitaja sababu za kupanda kwa gharama za vinywaji wanavyozalisha kuwa ni kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji.
“Bei zimepanda kutokana na sababu mbalimbali miongoni ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za malighafi, usafirishaji, kupanda kwa bei ya mafuta na kushuka kwa thamani ya shilingi,” alisema Malulu.

Alisisitiza kwamba matangazo ya viwango vipya vya bei ya jumla na rejareja tayari wameyachapishwa na yatasambazwa kwenye baa na maduka yote ya jumla nchini. imeandikwa na Leon Bahati. SOURCE MWANANCHI

watano wafa kwa kuangukiwa na kifusi

Watano wafariki dunia
kwa kufukiwa na kifusi

Israel Mgussi, Dodoma

WATU watano wamefariki dunia papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kufunikwa na kifusi kwenye machimbo ya kokoto yaliyopo katika kijiji cha Ntyuka, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Salum Msangi, waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Mwajuma Mnubi, Monika Chizumi, Mbeleje Ndigomba wote wakazi wa kijijini hapo na Jonasi Mnubi (2) na jina la marehemu mmoja halikupatikana. Hata hivyo, majina ya waliojeruhiwa hayakuweza kupatikana.

Msangi alisema tukio hilo lilitokea mnamo saa 5 asubuhi, lakini polisi walipata taarifa majira ya saa 6 mchana na kwamba, uokoaji ulianza saa 7 mchana hadi saa 10 jioni.

“Tulifika eneo la tukio kwenye saa 7 mchana na kuanza kufukua kifusi tukisaidiana na wafanyakazi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)ambao walitoa katapila lililosaidia kwa kiasi kikubwa kufukua udongo,” alisema.

Mashuhuda hao walisema, marehemu hao ambao walisimama kwenye gema karibu na shimo hilo, walijikuta katika wakati mgumu baada ya udongo wa mahali walipokuwa wamesimama kumeguka na kutumbukia shimoni na kufukiwa kabisa.

Kutokana na shimo hilo kuwa kubwa walishindwa kutoka na wala watu wengine walishindwa kuwanusuru kutokana na kiasi kikubwa cha udongo uliowafunika.

“Tukio hili lilitokea muda wa saa tano asubuhi, lakini tulishindwa kuwaokoa wakiwa hai kutokana na kiasi kikubwa cha udongo kilichomeguka na kufunika kabisa shimo, hivyo tuliamua kuomba msaada polisi na uokoaji ulianza rasmi saa saba mchana baada ya wanausalama hao kufika,” walisema mashuhuda wa tukio hilo.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk James Msekela alishiriki kikamilifu katika ufukuaji wa shimo hilo na alitoa kiasi Sh50,000 kwa kila familia ya marehemu hao na kuwatahadharisha watu wanaojihushisha na uchumbaji wa kokoto kuwa makini ili wasije wakakumbwa na balaa kama hilo.

Kijiji cha Ntyuka ni maarufu kwa shuguli za uchimbaji wa kokoto zinazotumika katika ujenzi na asilimia 80 ya shughuli za ujenzi mjini Dodoma hutegemea kokoto za kutoka eneo hilo.

CCM mambo juu ya mambozz

Source TBC.

Mpaka sasa mkutano haujaisha ila Taarifa toka Dodoma, ni kuwa wajumbe karibu wengi kwenye mkutano wa NEC ya CCM wanapendekeza kamati ya Mzee Mwinyi iongezwe muda ili kuweza kuendelea kumalizia tofauti zilizopo baina ya wana CCM.

Katibu mwenezi wa CCM, kutoa taarifa rasmi mara tu baada ya mkutano kumalizika hata iwe saa nane ucku, atakuwa na press confrence muda huwo!!!!!!!

Lakini suala bajeti ya uchaguzi ndani ya CCM na mvutano baina ya makundi ndani ya chama ni miongoni mwa mambo yaliyozua mvutano katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (Nec) uliyomalizika jana na kushindwa kufikia hitimisho na badala yake inadaiwa kuwa walilishana yamini ili mambo yaishe.

Mazingira hayo pia yaliwafanya wajumbe wa mkutano huo kuitaka Kamati ya Mzee Ali Hassan Mwinyi iliyopewa jukumu la kuchunguza kiini cha mparaganyiko ndani ya chama hicho tawala, hivyo kuiongezea muda ili kuweka sawa baadhi ya mambo ambayo hayakuwa na majibu ya kujitosheleza.

Suala la maridhiano ya Zanzibar pia linadaiwa kuwasha moto katika mkutano huo ikidaiwa kwamba, kulikuwa na mvutano mkali miongoni mwa wajumbe, huku baadhi wakitaka tarehe ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar isogezwe mbele na wengine wakipinga.

Sunday, February 14, 2010

CCM Mambo mazito


Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wakiwa wamesimama kumkumbuka Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu hayati, Rashidi Kawawa kabla ya kuanza kwa mkutano wao Mjini Dodoma Februari 14, 2010. Kulia ni Makamu wa Rais, Dk. Ali MohamedShein na wapili kulia ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mawaziri Wakuu Wastaafu, Frederick Sumaye (kushoto ) na Edward Lowassa , wakiteta kabla ya kuanza kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM mjini Dodoma , Februari 14, 2010. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Spika wa Bunge, Samuel Sitta (kulia) akisalimiana na wajumbe wenzake ambao pia ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Frederick Sumaye (kushoto) na Edward Lowassa (katikati) kablaya kuanza kwa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mjini Dodoma Februari 14, 2010..(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

JK atangaza Malaria janga la taifa



RAIS Jakaya Kikwete ameutangaza ugonjwa wa malaria kuwa ni Janga la Taifa na kuwaambia Watanzania kuwa Serikali yake imeanza safari ya kuutokomeza ugonjwa huo nchini. Malaria ndiyo ugonjwa unaoua Watanzania wengi zaidi kuliko mwingine wowote.

Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa marais wanaopambana na malaria barani Afrika alisema kwamba, ugonjwa wa malaria ni vita ambavyo ni lazima Watanzania wavishinde kwa vile nia ipo, sababu ipo na uwezo upo.

Aliongeza kusema kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa malaria inakuwa ugonjwa wa historia kwa Tanzania kwa kuwa hata nchi nyingine zimefanikiwa kuutokomeza.

Alisema kuwa kila siku ya Mungu, kiasi cha watu kufikia 291 hufariki kwa ugonjwa wa malaria, wengi wao wakiwa watoto wadogo, vifo ambavyo alivielezea kuwa vinaweza kuzuilika na kutibika.

“Kila siku ya Mungu, hapa nchini, wanakufa watu hadi 291 kwa ugonjwa wa malaria. Kwa maneno mengine, kila saa inayopita, wanakufa watu zaidi ya 10 kwa ugonjwa wa malaria.” Rais Kikwete aliliambia taifa usiku wa kuamkia jana.

“Hawa ni watu wengi mno. Hivyo, malaria ni Janga la Taifa letu. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba malaria ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika. Ndiyo maana tumeamua kuwa wakati tunaendelea kushughulikia kutibu wagonjwa wa malaria, tuelekeze nguvu zetu katika kuzuia kwa kuanza juhudi za kutokomeza malaria nchini.”

Rais Kikwete alikuwa akizungumza moja kwa moja na taifa wakati anazindua Kampeni dhidi ya Malaria katika burudani maalumu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Leaders Club mjini Dar es Salaam juzi usiku.

Kampeni hiyo imeanzishwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini na taasisi za Malaria No More, Population Services International (PSI) na Chuo Kikuu cha John Hopkins, vyote vya Marekani.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

Wabunge wapya wateule wa Rais


Mbunge wa Kuteuliwa, Ismail Jussa Ladhu, akiapa Bungeni Mjini Dodoma juzi ijumaa

Mbunge wa Kuteuliwa, Janet Zebedayo Mbene akiapa Bungeni Mjini Dodoma juzi ijumaa. Picha za Edwin Mjwahuzi.

MKUTANO WA CATA UANGAZIE MIJADALA YA KUHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UKUSANYAJI MAPATO - MAKAMO WA RAIS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia ni chachu kati...