Serikali imeanzisha Programu ya kuendeleza miji iliyochakaa kwa kuboresha makazi pasipo kuwahamisha mwananchi hata mmoja kutoka katika eneo analomiliki.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi Aprili 04, 2025 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Makangira, Kata ya Msasani wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam wakati akitambulisha program hiyo.
“Katika program hii, hakuna mwananchi hata mmoja atahamishwa, tumedhamiria kuboresha makazi yenu pasipo kuhamishwa kwa mwananchi hata mmoja kutoka katika eneo analoishi isipokuwa kwa wananchi wachache ambao utekelezaji wa mradi utakapoanza, Serikali itawapangishia nyumba wakati mradi ukiendelea kutekelezwa na baada ya kukamilika kwa mradi mtarejea katika maeneo yenu” amesema Waziri Ndejembi.
Waziri Ndejembi amesema kwa kuzingatia matakwa Sera ya Taifa ya mwaka 1995 Toleo la mwaka 2023 ambayo imezinduliwa hivi karibuni na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Programu hiyo maalum ya uendelezaji upya maeneo chakavu katika miji ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa huduma za msingi, miundombinu, makazi duni au chakavu, ukosefu wa mifumo ya maji taka na uwepo wa changamoto ya taka ngumu zinapelekea uchafuzi wa mazingira.
Wizara imetambua jumla ya maeneo 111 katika mikoa 24 ambapo kwa kuanzia Programu hiyo itatekelezwa katika majiji ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Mwanza Mbeya na Tanga.
Waziri Ndejembi amesema program hiyo ina faida lukuki ikiwemo upatikanaji wa ardhi iliyopangwa kwa matumizi mbalimbali ambayo ni kichocheo cha ongezeko la shughuli za kiuchumi na kijamii, upatikanaji wa nyumba hususani za makazi na biashara na kutatua changamoto ya makazi duni katika maeneo ya miji nchini, kuboresha madhari ya miji yetu na kuongeza usalama wa milki za wananchi katika maeneo husika kwa kupatiwa hati za sehemu ya jengo na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kugeuza ardhi mfu kuwa na thamani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Saad Mtambule amesema program hiyo itakuwa suluhisho la changamoto ya mafuriko, magonjwa ya mlipuko, migogoro ya ardhi na itasaidia kuongeza thamani ya ardhi katika eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya maji na barabara hatua itakayoboresha makazi ya wananchi wa eneo la Makangira jijini Dar es salaam.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Songoro Mnyonge amesema ujio wa program hiyo umekuja muda mwafaka ambapo manispaa hiyo mwaka 2013 ilipitisha Mpango wa Kuboresha Makazi ili kupata nyumba bora za wananchi wa manispaa hiyo.