INAONEKANA Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kampeni za mapema kabla hata ya kuruhusiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) baada ya kuwanadi wagombea katika mikoa mitatu sasa ikianziwa na Dodoma, ikafuata Zanzibar na sasa Dar es Salaam na wasipopigiwa kelele watazunguka tanzania nzima.
Leo Rais Kikwete kama inavyoonekana pichani katika viwanja vya Mnazi Mmoja amewanadi wagombea wake na kisha akawaonya vikali wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia tiketi ya CCM, juu ya jaribio lolote la kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Aliyesema yeyote atakayekamatwa akijibusisha na vitendo hivyo, hatasemahewa na badala yake ataishia mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
''Fomu chukueni, lakini atakayebainika kupokea au kuchukua rushwa tutamkabidhi kwa Edward Hosea na timu yake wafanye kazi yao, sisi huko hatuko, tutakuwa tunafanya shughuli nyingine za kulijenga taifa,''alisema Rais Kikwete.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo kupitia CCM aliwataka watendaji wa chama hicho wanaotarajia kuanza kazi ya kukabidhi fomu leo, kufanya hivyo bila upendeleo wa aina yoyote.
Alisema watendajia hao wasikubali kuegemea upande wowote na kwamba kinachotakiwa ni kuonyesha demokrasia ya kweli katika CCM, hasa ikizingatiwa kuwa muda wa makundi umekwisha.
''Mzee Msekwa alikuwa analala saa saba usiku kule Dodoma katika jitihada zake za kumaliza migogoro ndani ya chama, hivyo hatutegemei tena kusikia kuna makundi yanajitokeza ndani ya chama na wala hatutavumiliana,''alisema.
Alisema ni kweli kuwa kulikuwa na makundi ndani ya chama hicho lakini kutokana na jitihada za viongozi, tatizo hilo limemalizika.
Rais Kikwete aliwataka wagombea wa ngazi mbalimbali wa chama hicho na wabunge wahakikishe kuwa wanaoisoma vizuri ilani ya chama hicho na kuelezea mambo watakayowafanyia wananchi.
''Someni vizuri ilani ya chama muifahamu muwaelekeze wananchi katika kampeni zenu wajue mtawafanyia nini kipindi kijacho, ili wawaelewe na kama ulifanya vizuri watakukubali tu hivyo tujipange na tuitetee ilani yetu ,''alisema.
Kwa upande wake, mgombea urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya chama hicho, Dk Ali Mohamed Shein alitumia muda wake kumpongeza Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume kwa kuwa kiongozi wa mafanikio.
Dk Shein alielezea maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya CCM na CUF, kuwa ni miongoni mwa matunda mazuri ya uongozi wa Rais Karume na kwamba atayaenzi.
Comments