Monday, December 07, 2015

RAIS MAGUFULI AVUNJA BODI YA MAMLAKA YA BANDARI

MSAMBICHAKA 1
* Atengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu TPA
* Amsimamisha kazi Katibu Mkuu Uchukuzi
* Waziri Mkuu awasimamisha kazi watumishi wengine 13 wa bandari
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amevunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Prof. Joseph Msambichaka pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Bw. Awadhi Massawe.
Dkt. Magufuli pia ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaban Mwinjaka kuanzia leo (Jumatatu, Desemba 7, 2015), na kwamba atapangiwa kazi nyingine.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika leo ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hatua hizo zimechukuliwa kufuatia ziara mbili za kushtukiza alizozifanya katika mamlaka ya bandari Novemba 27 na Desemba 3, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema Rais Magufuli amevunja bodi hiyo na kutengua uteuzi wa viongozi hao kutokana na utendaji mbovu wa muda mrefu wa Mamlaka ya Bandari na kwa kitendo cha viongozi hao kutochukua hatua kwenye vyanzo.
Pia alisema Katibu Mkuu amesimamishwa kazi kwa sababu ya kutosimamia kwa makini mashirika mawili ya Bandari na Reli ambayo yako chini ya wizara yake ambako yeye mwenyewe alizuru Shirika la Reli (TRL) Desemba 3, 2015 na kukuta kuna ubadhirifu wa sh. bilioni 16.5/-.
“Tarehe 3 Desemba mwaka huu nilifanya ziara ya kushtukiza pale TRL nikakuta wametumia visivyo sh. bilioni 13.5/- walizopewa na Serikali. Pia nilikuta wamekopa sh. bilioni 3/- kutoka benki ya TIB lakini nazo wamezitumia nje ya utaratibu. Fedha hizi zilikuwa ni za kusaidia kuboresha miradi ya shirika lakini wao wamezitumia visivyo. Uchunguzi bado unaendelea,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi kuanzia leo viongozi watano wa sekta zilizotoa ruhusa ya makontena kutoka ndani ya bandari pamoja na watumishi wanane wa bandari kavu ambao walihusika na ukwepaji kwa makontena 2,387.
“Viongozi hawa hawakuwemo kwenye ripoti ya ukaguzi lakini ni wahusika wakuu. Hawa ndiyo waliotoa ruhusa ili makontena yaende kwenye ICDs. Nao ni aliyekuwa Meneja Mapato ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu kitengo cha Fedha, Bw. Shaban Mngazija; aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD) – ambaye amehamishiwa Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi Co-operate Services, Bw. Rajab Mdoe; Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Ibin Masoud; na Meneja Bandari Msaidizi – Fedha, Bi. Apolonia Mosha
Pia amewasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICDs) ambao ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante na James Kimwomwa ambaye alihamishiwa Mwanza lakini kuanzia sasa anasimamishwa kazi huko huko aliko.
“Bila wao kuidhinisha hakuna kontena linaweza kutoka au kwenda kokote. Watumishi wote hao wawe chini ya ulinzi na waisaidie polisi kupata taarifa hayo makontena ni ya nani na yana thamani gani,” Waziri Mkuu alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Desemba 3, mwaka huu aliamua kurudi tena bandarini kufuatilia na kuangalia hatua ya udhibiti wa upitishaji wa bidhaa mbalimbali kinyume cha utaratibu. “Ziara yangu ilinipitisha hatua zote za upitishaji mizigo ambazo pia kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi wa Ndani ya tarehe 30 Julai 2015, Mamlaka ya Bandari iligundulika kuwepo kwa mianya mingi ya ukwepaji kodi ikiwemo makotena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi – Septemba 2014 kinyume cha utaratibu”.
“Vitendo hivi vinaonyesha kuwa bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Serikali haitavumilia kuona watu wachache au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia Serikali kwa namna yoyote ile kwa manufaa ya wachache kwani bandari ni eneo muhimu ambalo likisimamiwa vizuri, linaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia Pato la Taifa,” alisema.
Desemba 3, mwaka huu, Waziri Mkuu alimpa saa tatu tu Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo. Pia alimpa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment). Mwisho wa kukamilisha zoezi hilo ni Desemba 11, 2015.

No comments: